Bosi wa zamani Nida akutwa na kesi ya kujibu

Muktasari:
- Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemkutana kesi ya kujibu aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake wanne na hivyo wanatakiwa kuanza kujitetea.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewakuta na kesi ya kujibu, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake wanne na wataanza kujitetea, Agosti 25 na 26, mwaka huu.
Uamuzi huo umetolewa leo, Agosti 11, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili uamuzi kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au laa.
Maimu na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 55 yakiwemo ya kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 1.175 bilioni.
Soma zaidi: Maimu, wenzake wasomewa mashtaka 100
"Nimepitia mashtaka yote na vielelezo vyote, nimeridhika kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu, hivyo wanatakiwa kujitetea" Anasema Hakimu Chaungu.
Hata hivyo, washtakiwa wamedai kuwa watajitetea kwa kiapo na watakuwa na mashahidi na vielelezo.
Soma zaidi: Shahidi akwamisha kesi ya Maimu wa Nida
Hakimu Chaungu baada ya kueelza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 25 na 26, 2021 ambapo washtakiwa wataanza kujitetea.
Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya, alieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi na wao wako tayari kusikiliza.
Itakumbukwa kuwa Agosti 4, 2021 upande wa mashtaka uliieleza mahakama hiyo kuwa wamefunga ushahidi wa mashahidi 26 na vielelezo 45, vilivyotolewa na mashahidi hao.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine ni Ofisa Usafirishaji wa NIDA, George Ntalima; Meneja Biashara wa NIDA, Avelin Momburi; Xavery Silverius maarufu kama Silverius Kayombo na Mkurugenzi wa Sheria NIDA, Sabina Raymond.
Washtakiwa Maimu, Ntalima na Kayombo wamerudishwa rumande huku mshitakiwa Momburi na Sabina wako nje kwa dhamana.
Soma zaidi: Jalada kesi ya Maimu, wenzake kurudishwa kwa DPP
Imeandikwa na Hadija Jumanne, Irene Meena na Gloriana Sulle, Mwananchi [email protected]