Bunge laleta ahueni Sheria ya Habari

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi akiwasilisha bungeni muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2023, jijini Dodoma leo Juni 13, 2023
Dar es Salaam. Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambao ndani yake una sheria nane, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambao umekuwa ukipigiwa kelele na wadau wakitaka baadhi ya vifungu vibadilishwe.
Muswada huo uliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza Februari 10, 2023 na leo Juni 13, 2023 umejadiliwa na wabunge na kupitishwa pamoja na marekebisho katika baadhi ya vifungu vyake.
Akiwasilisha hotuba yake bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Eliezer Feleshi amesema kifungu cha 5 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 kinapendekeza kufanya marekebisho kwa lengo la kumwondolea Mkurugenzi wa Idara ya Habari jukumu la uratibu wa matangazo yote ya Serikali.
Pia, amesema marekebisho hayo yataiwezesha Serikali kuwa na uhuru wa kuchagua chombo cha habari itakachokitumia kwa ajili ya matangazo kwa kuzingatia nguvu ya ushindani katika soko.
“Inapendekeza kukifanyia marekebisho kifungu cha 38 kwa madhumuni ya kuongeza haki na uhuru wa maoni. Muswada unapendekeza marekebisho ya vifungu vya 50, 51, 53, 54, 55, 63 na 64 kwa madhumuni ya kuweka adhabu tahafifu kwa makosa yatokanayo na ukiukwaji wa sharia hii,” amesema Feleshi.
AG amesema mapendekezo ya marekebisho ya vifungu hivyo yanakusudia kuondoa adhabu kwa wamiliki wa mitambo ya uchapishaji ambao katika hali ya kawaida hawana uwezo wa kudhibiti maudhui yanayochapishwa katika mitambo hiyo ya uchapishaji.
Awali akichangia mjadala huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema katika mapendekezo 21 yaliyotolewa na wadau, Serikali ilikubali hoja nane zibaki kama zilivyo.
“Wadau walileta mapendekezo 21 ambayo walitaka tuyapitie kwa pamoja, katika mapendekezo hayo, yakagawanyika katika makundi manne, hoja ambazo tulikubaliana baada ya majadiliano kwamba zibaki kama zilivyo kwenye sheria.
“Baada ya mazungumzo ya muda mrefu na tukakubaliana kwa pamoja, karibia hoja nane kati ya 21, tukakubaliana zibaki kama zilivyo. Lakini hoja nyingine tukakubaliana zifanyiwe marekebisho ikiwemo kufutwa…ikiwemo kuondoa jinai,” amesema Nape.
Amesisitiza kwamba kwenye sheria hiyo, wameondoa jinai ili kuijenga tasnia ya habari ikue. Ameongeza kwamba baadhi ya mambo walikubaliana kwamba yakafanyiwe kazi kwenye kanuni ambazo zitatungwa hivi karibuni ikiwemo suala la leseni na muda wa leseni.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), Selemani Msuya aliipongeza Serikali kwa kuondoa jinai katika mabadiliko ya sheria hiyo kwa sababu itawawezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao bila hofu.
Pia, alipongeza kupitishwa kwa marekebisho ya kumwondolea Mkurugenzi wa Idara ya Habari jukumu la uratibu wa matangazo yote ya serikali na kuiwezesha Serikali kuchagua chombo itakachokitumia kwa ajili y matangazo kwa kuzingatia nguvu ya ushindani wa soko.
“Kwa kweli ilikuwa ni changamoto, kosa la jinai anayetafsiri ni Mahakama lakini anayeipeleka Mahakamani ni Idaraya Habari Maelezo au Wizara (ya Habari)…tafsiri hii itakuja Mahakamani kwamba hii ni jinai au si jinai kulingana na mlalamikaji alivyoleta andiko lake,” amesema Msuya.