CCM yahamasisha wanawake kugombea uchaguzi Serikali za mitaa

Wanachama wapya wa CCM, Kata ta Mzinga wakionyesha kadi za chama hicho baada ya kukabidhiwa. Picha na Pamela Chilongola
Muktasari:
Wanawake wanachama wa CCM wilayani Ilala Dar es Salaam, wamehamasishwa kujitokeza kugombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Ilala, Nasri Wambura amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Akizungumza leo Februari 2, 2024 wakati Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), CCM Kata ya Mzinga na Kitunda walipokuwa wakiadhimisha miaka 47 ya kuzaliwa kwa chama hicho, Wambura amesema watakaojitokeza wahakikishe wanajipima uadilifu ndani na nje ya chama hicho.
Katika maadhimisho hayo, Wambura amedai kuwa tangu jana Februari Mosi, wamekusanya zaidi ya wanachama 22,000 waliowapa kadi wilayani Ilala.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu wa UWT Kata ya Mzinga, Frorah Lemu amesema wamewahamasisha wanawake zaidi ya 500 wajiunge na umoja huo.
"Upande wa CWT Mzinga tumewapata wanachama wapya zaidi ya 500 ambao ni hai tunashukuru wanawake wamehamasika sana kuingia kwenye UWT,” amesema Lemu.
Lemu amesema UWT Mzinga kwa sasa inajivunia mafanikio ya kuwa na mtaji wa kutosha wa wanachama hao kutokana na mahusiano mazuri ndani ya chama na Serikali.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mzinga, Job Isac ameunga mkono juhudi zinazofanywa na UWT, na kuwataka wanawake wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura Ili waweze kuchagua viongozi wa Serikali za mitaa na wa Uchaguzi Mkuu wa 2025.