Chadema yadai makada wake kumi wanashikiliwa na polisi

Chadema yadai makada wake kumi wanashikiliwa na polisi

Muktasari:

  • Viongozi na wanachama wa Chadema wapatao kumi wanadaiwa kukamatwa na polisi Mkoa wa Ilala wakati wakiendelea na kikao cha ndani katika Jimbo la Segerea.


Dar es Salaam. Viongozi na wanachama wa Chadema wapatao kumi wanadaiwa kukamatwa na polisi Mkoa wa Ilala wakati wakiendelea na kikao cha ndani katika Jimbo la Segerea.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Agosti 4, 2021, Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Baraka Mwago amesema makada hao walikamatwa jana jioni wakati wakiendelea na kikao cha ndani katika jimbo la Segerea.

Amesema katika jimbo hilo kuna operesheni ya Chadema Digital inayoendelea na walikamatwa wakiwa kwenye kiao cha kawaida.

“Polisi walivamia kwenye kikao cha ndani wakituhumu kuwa tunapanga kuhamasisha maandamano, kitu ambacho si kweli, kwenye jimbo hilo kuna operesheni ya Chadema Digital inayoendelea,”amesema Mwago.

Soma zaidi hapa: Chadema yatoka na maazimio

 “Bado mawakili wa chama kutoka makao makuu wanaendelea kuwafuatilia ili kuona uwezekano wa kupata dhamana,” amesema.

Amewataja viongozi waliokamatwa kuwa ni pamoja na Julius Mwita, Gerva Lyenda, Alex Massaba, Omar Mkama, Aisha Macha, Fatuma Thabit, Patrick Asenga, Jacob Bailemba, Deogratius Kajula na Abdallah Senkamba.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Debora Magiligimba kuzungumzia tuki hilo alijibu kuwa yuko kwenye kikao atafutwe baadaye.

Juzi Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro alitoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu kitakachojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyorasmi kabla na kesho wakati wa kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.