Chandika: Watoto 3,000 hukosa matibabu ya moyo kwa mwaka

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa Dk Alphonce Chandika akikabidhiana hati ya makubaliano ya kutoa matibabu na Daktari bingwa wa Taasisi ya Childrens Heart Charity Association ya nchini Kuwait Dk Faisal Al-saied.
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa miongoni mwa watoto 3,4000 wanaougua maradhi ya moyo nchini, wastani wa watoto 400 hupata matibabu, huku wengine 3,000 wakikosa uhakika wa matibabu.
Dodoma. Imebainika kuwa zaidi ya watoto 3,000 nchini hukosa matibabu ya moyo kila mwaka.
Kutokana na hali hiyo, madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka nchini Kuwait wameweka kambi ya wiki moja katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kati Benjamin Mkapa jijini hapa, kwa ajili ya matibabu.
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano jana Februari 6, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika amesema wastani wa watoto 3,400 huzaliwa na magonjwa mbalimbali ya moyo kila mwaka nchini.
Chandika amesema kati ya watoto hao ni watoto 400 ndio huwa na uhakika wa kuhudumiwa katika hospitali mbalimbali huku watoto 3,000 wakikosa huduma na kusababisha kukua kwa ugonjwa na kupoteza maisha.
“Takriban kwa mwaka watoto 3,400 huzaliwa na magonjwa ya moyo nchini na sio wote wanaopata matibabu.
“Kambi hii itawasaidia watoto kupata matibabu na kuwaongezea ujuzi Madaktari wetu ambao wanashirikiana nao kwenye huduma zinazoendelea,” amesema Chandika.
Katika kambi, hiyo Chandika amesema watoto 100 watapata matibabu ya moyo kwa awamu ya kwanza, huku utaratibu wa madaktari hao kuja nchini ukiwa endelevu kwa kuwa hospitali hiyo na Taasisi ya Childrens Heart Charity Association imeingia makubaliano ya kutoa matibabu kwa miaka mitatu.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Childrens Heart Charity Association, Faisal Al-Saied amesema wataendelea kutoa matibabu kwa watoto kwa nyakati tofauti na kuwajengea uwezo madaktari wazawa ili wajitegemee kwenye huduma hiyo siku za baadae.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Said Mussa amesema ofisi yake itaendeleza ushirikiano na Serikali ya Kuwait katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Afya na uchumi.