Chaneli za ndani kuonekana bure ving’amuzi vyote

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

Siku chache zijazo watumiaji wa visimbusi nchini hawatalazima kuwa navyo vingi ili kupata maudhui mseto, hii inatokana na Serikali kubadili kanuni za miundombinu ya utangazaji kidijitali ambapo sasa chaneli zote za ndani zitapatikana kote.

Dar es Salaam. Siku chache zijazo watumiaji wa visimbusi nchini hawatalazima kuwa navyo vingi ili kupata maudhui mseto, hii inatokana na Serikali kubadili kanuni za miundombinu ya utangazaji kidijitali ambapo sasa chaneli zote za ndani zitapatikana kote.

Akizungumza leo Januari 31, 2022 wakati alipotembelea ofisi ya Multchoice Tanzania (Dstv) Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali imefanya mabadiliko hayo na yameshatangazwa katika gazeti la Serikali kuanzia jana.

Nape amesema tangu kuondolewa kwa cheneli hizo kwenye visimbusi vya kulipia kumekuwa na kilio kikubwa kwa wananchi na hata wadau wengine ndiyo maana mabadiliko hayo yamefanyika ili kulingana na mahitaji ya watu.

"Sheria, Sera na Kanuni zinapaswa kubadilika kulingana mazingira yaliyopo na mahitaji. Kanuni hizi mpya zitaongeza wigo wa Watanzania kupata habari kwani wakati ambapo chaneli za ndani zilikuwa hazipatikani watu walikuwa wanaangalia zaidi za nje jambo ambalo sio zuri," amesema.

Amesema hatua hiyo itasaidia chaneli za ndani zitapata nafasi ya kuonekana nje ya mipaka ya Tanzania, kukuza biashara zao lakini pia kuendeleza na kueneza lugha ya kiswahili ambayo hutumiwa zaidi na cheneli hizo hivyo ametoa wito kwa waandaji wa maudhui kuboresha zaidi.

"Pamojana na kupanua wigo wa habari, lengo ni kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji yanayoendana na uhalisia wa biashara ya maudhui na kuhamasisha na kuchochea utengenezaji wa maudhui ya ndani," amesema Nape.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Dstv Tanzania, Jacqueline Woiso amesema hatua hiyo si tu inaleta athari chanya kwa Watazamaji na kampuni za maudhui bali hata biashara kwa upande wao itakuwa vizuri.

"Hatua hii inatoa fursa kwa Watanzania kuziona chaneli za ndani ambazo walikuwa hazioni sasa lakini pia kwa chaneli biashara itaongezeka kwa kuwa wataongeza wigo wa kuonekana na kuuza matangazo zaidi. Kwetu sisi wakati chaneli hizi zimeondolewa kibiashara ilikuwa inaumiza kwani ni vigumu kumshawishi mtu aunge kifurushi lakini sasa tutapata nafuu," amesema Woiso.

Aidha ameongeza kuwa Dstv itawachukua wiki takribani moja kuwa wamerejesha chaneli hizo na kuanza kuonekana.