Daktari feki aingia tena kazini

Muktasari:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange amesema Mgalla ambaye ni mfungwa anayetakiwa kufanya kazi za jamii kwa miezi sita mfululizo mkoani Songwe, amekamatwa hivi karibuni akifanya kazi katika hospitali hiyo.
Mbeya. Polisi mkoani Songwe wanamshikilia Moses Mgalla kwa tuhuma ya kuruka kifungo cha nje cha miaka mitatu kwa kosa la kufanya udaktari bila sifa baada ya kukutwa akifanya kazi ya udaktari katika Hospitali ya Ifisi, Mbeya Vijijini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange amesema Mgalla ambaye ni mfungwa anayetakiwa kufanya kazi za jamii kwa miezi sita mfululizo mkoani Songwe, amekamatwa hivi karibuni akifanya kazi katika hospitali hiyo.
Nyange amesema Mgalla ni mfungwa baada ya kupatikana na hatia katika kesi namba 220/2016 aliyoshtakiwa kwa kosa la kujifanya daktari na kufanya kazi Hospitali ya Vwawa wilayani Mbozi.
Amesema katika kesi hiyo amehukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu kuanzia Aprili adhabu ambayo amedai kwamba hakuitekeleza.
“Kwa ujanja amekwenda kuomba kazi akitumia jina la Huruna Mgaya katika Hospitali ya Ifisi na ndiko tulikomkamata, hivyo tunamshtaki kwa kosa la kuruka kifungo, lakini Mbeya wanaweza kumshtaki kwa kosa la kujifanya daktari na kufanya kazi katika hospitali,” alisema.
Alisema Mgalla anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.