DC Lindi atoa siku 14 maji kupelekwa shule ya wasichana Kilangala

Tanki la maji ambalo likimalizika litahudumia wakazi 3931
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, ametoa siku 14 kwa mkandarasi wa RUWASA, kupeleka maji katika shule mpya ya Sekondari ya wasichana iliyopo katika kijiji cha kiangala mkoani lindi.
Lindi. Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ametoa siku 14 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), kuhakikisha huduma ya maji safi na salama, inawafikia wanafunzi wa Shule ya Wasichana Kilangala.
DC Ndemanga ametoa agizo hilo leo Ijumaa Sept 8.2023, kwenye makabidhiano ya mabomba kwa Wakala huyo, ambaye anahusika na usambazaji huduma ya maji wilayani Lindi, akisema muda huo unatosha kupeleka maji shuleni hapo ili wanafunzi wapate maji kwa ukaribu kuliko wanavyotumia chanzo ambacho hakina uhakika.
"Natoa siku 14 kwenu Ruwasa, mjitahidi ndani ya siku hizo muwe mshapeleka maji shuleni pale, kwa kuwa wale watoto ni wakike, na pia chanzo wanachotumia hakina uhakika sana, na kama mtafanya ndani ya siku 7 itakuwa vizuri zaidi," amesema DC Ndemanga.
Mkuu wa Wilaya huyo, ameendelea kusema kuwa mradi huo unafanywa na wataalam wa ndani na kuhakikisha ifikapo October 30, mradi uwe umekamilika ili wananchi waweze kuondokana na adha waliyokuwa wanaipata kwa miaka mingi.
"Ujenzi huu unakamilika ifikapo October 30, niwaombe Ruwasa mjitahidi kumaliza kwa wakati, maana wananchi wanateseka sana na maji kwa muda mrefu, huu mradi ukikamilika utawasaidia sana wananchi hawa...namshukuru Rais (Mama Samia) kwa kutuletea fedha nyingi kwa ajili ya mradi wa maji hapa kilangala," amesema DC Ndemanga.
Aidha Meneja Ruwasa wilayani Lindi, Mhandisi Iddi Pazi, amesema hadi kukamilika kwa mradi, utakuwa umegharimu Sh500 milinoni na kwamba utanufaisha wakazi 3931 wa vijiji vya Kilangala A na B.
"Mradi huu wa maji katika kijiji cha kilangala A na B utatoa lita za ujazo 196,017 kwa siku na utaweza kunufaisha wakazi 3931; na hadi sasa mradi umefikia asilimia 50. Tutahakikisha unakamilika ifikapo October 30,” amesema Pazi.
Kwa upande wake Salma Kitunguli, Mkazi wa Kijiji cha Kilangala A, ameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo kwani imekuwa ikiwalazimu wanatembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita tatu kutafuta maji.
"Kiukweli sisi wakazi wa Kilangala zote A na B, tunamshukuru Rais, Mama Samia; kwa kutuletea pesa nyingi kwa ajili ya mradi huu, na ukikamilika, hatutakuwa na shida tena ya maji. Tunatembea umbali mrefu kutafuta maji, zaidi ya kilometa tatu na wakati huo huo, huku kwetu kuna wanyama wakali," amesema Salma.
Hamidu Namponda, ambaye pia ni mkazi wa Kilangala, hakuwa mbali na maoni ya mwanakijiji mwenzake, japo ameongeza kusema, licha ya kufuata maji umbali mrefu tena kwenye vitisho vya wanyama, chanzo hicho ambacho ni kisima, siyo cha kuaminika.