Dk Nchimbi: CCM inasimamia utawala sheria

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makala wakipokewa katika ofisi za CCM mkoa wa Katavi leo Jumamosi Aprili 13, 2024.

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wananchi kujitokeza katika mikutano hadhara kwenye ziara za viongozi na kutoa kero zao lakini kimetoa angalizo la kupokea changamoto zisizokuwapo mahakamani.

Katavi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema katika utaratibu wao wa kusikiliza kero za wananchi, hawatahusisha zilizopo mahakamani kwa sababu wana heshimu muhimili huo na utawala wa sheria.

Dk Nchimbi ameeleza hayo leo Jumamosi Aprili 13, 2024 wakati akizungumza na WanaCCM wa Mkoa wa Katavi katika ofisi za chama hicho zilizopo wilayani Mpanda mkoani hapa.

Dk Nchimbi alikuwa anatilia mkazo kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Amos Makalla ambaye katika salamu zake za utangulizi amesema katika ziara zao wanawaalika watu wote kutoa kero isipokuwa zilizopo mahakamani.

Dk Nchimbi ambaye ni mwanadiplomasia  na baadhi ya viongozi wenzake wanaounda  sekretarieti ya CCM wameanza ziara ya mikoa sita ya kuimarisha, kukagua uhai wa chama hicho na kuangalia utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi.

"Nitumie nafasi hii kumuunga mkono mwenezi wetu wa Taifa katika mambo tutakayoyashughulikia kama kero, hatutayagusa yaliko mahakamani, ndio utaratibu wa utawala bora. Moja ya sera ya CCM ni kusimamia utawala wa sheria,” amesema.

"Wakati wote wajibu wetu utakuwa kuzihamasisha mahakama zetu zitende haki bila kuziingilia katika uamuzi wake, nchi inayotaka kufanikiwa lazima isimamie utawala bora, ukijenga utaratibu wa kuingilia mahakamani siku moja, itawaumiza ... au wakija wengine watasema huyu mwenyekiti wa chama mkoa si alipenda kuagiza mahakama, acha tuagize akae mahabusu siku 90 kwanza kabla ya kuongea naye," amesema Dk Nchimbi.

Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi ambaye ni mbunge wa zamani wa Songea Mjini, amewataka WanaCCM kuwa mstari wa mbele kutangaza masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali kupitia ilani ya uchaguzi.

"Taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM inatia moyo, mmefanya kazi nzuri Katavi, kinachotakiwa ni kuwaambia wananchi kazi zilizofanyika, kinachotuponza ni kutoeleza kazi zilizofanyika. Tunatumia msemo wa tenda wema usingoje shukrani, lakini katika siasa shukrani zinatafutwa.

"Katika siasa lazima useme kama uliahidi katika miaka mitano, utafanya moja, mbili, tatu hadi nne, kadri moja inayoitekeleza lazima useme umefanya, usiposema wenzako watasema wamefanya wao kumbe sio wao," amesema Dk Nchimbi.

Awali, akijenga hoja yake, Makalla amewataka wananchi kutambua kuwa mambo yaliyopo katika mhimili wa mahakama  yanamalizwa hukohuko na hivyo wao hawatayasikiliza.

"Tunachowasaidia wananchi, yale mashauri yanayohitaji mambo ya utawala yasiingie mahakamani, kwa hiyo hata ukija katika mkutano wa hadhara usilete suala lililopo mahakamani, ukweli lazima usemwe.

"Tutakuwa tunawadanganya watu kwamba hili lipo mahakamani tutakusaidia, si kweli, lazima wakati mwingine tuwe wakweli, tunafuata utaratibu," amesema Makalla.

Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya chama hicho, Issa Ussi Gavu amewataka WanaCCM kuhakikisha wanawapata wagombea wenye sifa na malengo ya kutatua changamoto za wananchi, na kuwa wale wenye makandokando hawatakuwa na nafasi.

"Hata kama mtu mwenyewe amekaa vipindi viwili, kwa CCM hii hatutambeba tunahitaji viongozi wenye utayari wa kukitumikia chama chetu na wananchi," amesema Gavu.