Fao watoa dozi milioni tatu za ugonjwa wa sotoka

Fao watoa dozi milioni tatu za ugonjwa wa sotoka

Muktasari:

  • Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao) limetoa chanjo dozi milioni tatu kwa wilaya saba nchini kukabiliana na ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo.

Monduli. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao) limetoa chanjo dozi milioni tatu kwa wilaya saba nchini kukabiliana na ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo.

Akizungumza leo Jumatano Juni 9, 2021  katika uzinduzi wa kutoa chanjo za mifugo katika shamba la mifugo la Manyara Ranchi wilayani Monduli, kaimu ofisa mfawidhi wa kituo cha magonjwa ya mifugo Kanda ya Kaskazini, Dk Raphael Mwampashi amesema Fao na Serikali wanataka kudhibiti ugonjwa huo.

Dk Mwampashi amesema wilaya ambazo zitapewa dozi hizo ni Monduli, Longido, Kiteto, Simanjiro, Ngorongoro, Kongwa na Serengeti.

"Huu ugonjwa ni hatari kwa mifugo na tumeanza kutoa chanjo hizi hapa Manyara ranchi kutokana na mifugo kuishi pamoja na wanyamapori wanaozunguka hifadhi za Taifa za  Manyara na Tarangire ambao baadhi wanaweza kuambukizana,” amesema

Ofisa programu wa Shirika la Uhifadhi na Maliasili la Afrika (AWF) linalosimamia ranchi hiyo, Pastor Magingi amesema msaada huo wa chanjo ya sotoka ni mkubwa kwao na wafugaji vijiji vya Esilalei na Oltukai ambavyo vinapakana na shamba hilo.

Amesema kaya 1000 zenye kondoo na mbuzi 25,000 zitanufaika na chanjo  hiyo ambayo pia itatolewa kwa mifugo iliyopo ndani ya shamba hilo na hivyo kuzuia kusambaa ugonjwa huo kwa wanyamapori na mifugo.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Monduli, Kaiza  Victor amesema chanjo hiyo itatolewa kwa vijiji vingine vya wilaya hiyo  na wanatarajia kuchanja  mifugo 350,000 na kuomba wafugaji kujitokeza kuchanja mifugo yao.

Meneja wa mifugo wa Manyara ranchi, Lemaly ole Kibiriti amesema chanjo hiyo itazuia wanyamapori na mifugo kuambukizana.

Shamba la Manyara lenye  ukubwa  zaidi ya ekali 45,000 lipo eneo la mapito ya wanyama kutoka hifadhi ya Manyara kwenda Tarangire na hadi sasa lina ng'ombe 840 na kondoo 540.