Hali tete wajawazito Temeke, uongozi wataja mikakati

Dar es Salaam. Idadi kubwa ya wajawazito wanaopokewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke imesababisha wachangie kitanda kimoja wawili hadi watatu.

Licha ya changamoto hiyo, wajawazito hao, wengi wakiwa ni wenye rufaa wanasema kikubwa kwao ni kupata matibabu ya kibingwa.

Hata hivyo, Serikali inafanya jitihada mbalimbali kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuifanyia upanuzi kwa kujenga ghorofa; kutoa huduma kwenye vituo ili kupunguza rufaa katika hospitali hiyo iliyo chini ya Wizara ya Afya na kuwafundisha wataalamu vituoni.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini wodi tatu zilizopo hospitalini hapo zina uwezo wa kupokea wajawazito 75 lakini hupokea zaidi ya 100 kila siku wanaofika kupata huduma ya kujifungua.

Wakati huohuo, makadirio ya wastani kwa kila mjamzito hutumia saa 72 akiwa hospitali ambayo ni sawa na siku tatu.

“Natokea Kilungule, nilipohudhuria kliniki mara ya tatu pale Mbagala Rangi Tatu waliniambia mtoto ni mkubwa, hivyo wakanipa rufaa ya kuja Temeke. Nilifurahi kuja hapa kwa kuwa wasiwasi uliniondoka, nilijua nitakutana na madaktari bingwa zaidi ikilinganishwa na kule zahanati nilikoanzia hudhurio la kwanza,” anasema Amina Athuman (32), aliyejifungua kwa upasuaji.

Naye, Naomi Rafael (40), anasema changamoto kubwa Temeke ni wingi wa wagonjwa, akisimulia namna alivyolala ‘mzungu wa nne’ usiku mzima akisubiri kujifungua.

“Huyu ni mtoto wangu wa tano, kitandani tulikuwa wawili; nashukuru Mungu nilijifungua salama, lakini kwa changamoto kubwa maana hata wodi za waliojifungua tumejaa. Huku huduma za kibingwa unapata tatizo ni wingi wa wagonjwa,” anasema.


Ukubwa wa tatizo

Hospitali hiyo inahudumia wananchi wa Temeke na kutoka nje ya wilaya hiyo, wakiwamo wanaotoka hospitali ya Tungi wilayani Kigamboni na ya Mkuranga mkoani Pwani. Pia inapokea wanaotoka katika vituo vya afya na Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dk Ally Mussa anasema wamekuwa wakipokea wajawazito wengi wanaohitaji huduma ya kujifungua, hivyo suluhisho pekee kwao ni kuwapeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke.

“Unaweza kuwa na kinamama wenye dharura wengi, hivyo inabidi uwapeleke Temeke na wengine wanaweza kuwa si wa dharura lakini umezidiwa vitanda vyote vimejaa inabidi unawapunguzie huko.

“Waliotibiwa wakapata changamoto nyingine zinazowafanya wakae kwa muda mrefu hospitali, inabidi tuwapeleke Muhimbili, Mloganzila au Temeke ambako kuna eneo la kuwaweka na wapo wale ambao wanakuwa wanahitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa maana sisi hatuna eneo hilo,” anasema Dk Mussa.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke ina wodi tatu; ya wanaosubiri kujifungua yenye vitanda 17 sawa na ya waliojifungua kwa njia ya kawaida na ya waliojifungua kwa upasuaji. Kila moja uhudumia kinamama takriban 50 kwa siku.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Temeke, Dk Vicent Kimaro alipoulizwa kuhusu changamoto hiyo alisema wanahudumia wagonjwa wengi kutoka vituo mbalimbali.

“Kutokana na changamoto za kukosa eneo, Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali tupo kwenye juhudi za kuangalia namna ya kupanua kwa kujenga ghorofa,” anasema.

Hata hivyo, anasema wanaendelea kutoa huduma kwenye vituo vinavyowazunguka ili kupunguza rufaa katika hospitali ya Temeke na kuwafundisha wataalamu vituoni.

“Jopo la madaktari bingwa limekuwa likitoa mafunzo kwa wataalamu katika Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu na katika vituo vya afya namna ya kufanya upasuaji na matibabu ya kibingwa, hivyo taratibu tumekuwa tukipunguza wagonjwa wengi kuletwa Temeke,” alisema Dk Kimaro.


Juhudi za Serikali

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Wakili Kanua anasema kuna jumla ya vituo 201 vya kutolea huduma za afya, kati ya hivyo vya umma vipo 28 na binafsi 166.

Kwa upande wa taasisi za Serikali, anasema viko saba vinavyojumuisha zahanati, vituo vya afya na hospitali za Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Polisi.

Anasema halmashauri ina vitanda 1,738, kwa ajili ya wodi ya wagonjwa wa ndani vipo 1,191; ya wazazi 479 na vya kujifungulia ni 68 ambavyo havitoshelezi mahitaji.

Kanua anasema halmashauri inakabiliwa na upungufu wa watumishi wa sekta ya afya akieleza waliopo ni 829 tofauti na mahitaji halisi ya 1,500. Pia anasema kuna upungufu wa wataalamu wa afya 671 sawa na asilimia 45.

Ili kutatua changamoto hiyo, anasema halmashauri inatekeleza miradi yenye thamani ya Sh13.5 bilioni kwa fedha za ndani na ruzuku kutoka Serikali kwa ajili ya ujenzi wa vituo vipya vya afya vya Goroka, Mkondogwa na Kibondemaji.

“Tunafanya upanuzi wa miundombinu katika zahanati za Toangoma na Kilakala, ujenzi wa zahanati mpya kata ya Kurasini na Kilungule. Pia ujenzi wa jengo la ghorofa sita katika Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu ambao unagharimu Sh10.8 bilioni,” anasema.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo anasema changamoto ya idadi kubwa ya wagonjwa Temeke inatatuliwa.

“Hata ukienda Mbagala Rangi Tatu utaona idadi ni kubwa, kwa maana lazima uangalie kuona watu wanatokea wapi, kule Zakhiem zile zahanati nazo zinahitajika zianze kutoa huduma bora na ndicho tunachokifanya sasa. Tunaziimarisha kwa kushirikiana na Tamisemi,” anasema.

Anasema kwa mwezi wanaojifungua wameanza kupungua kwa sababu ya kuimarishwa kwa vituo vya afya.

Profesa Rugajjo anasema wanaohitaji huduma za kibingwa wataanza kushughulikiwa katika ngazi za chini na si Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa sababu zitajengewa uwezo wa kutosha.

Anasema kwa mgonjwa anayetokea Mbagala, matibabu yake yakishindikana kwenye zahanati atakwenda kituo cha afya, hospitali ya wilaya na baadaye atapelekwa Mbagala Rangi Tatu na kisha Hospitali ya Temeke. Iwapo huko kote itashindikana ndipo atapelekwa Muhimbili.

Profesa Rugajjo anasema kwa sasa kuna mabingwa, vifaa na vifaa tiba vya kisasa na wanahakikisha kila hospitali inaona wagonjwa kulingana na uwezo wake na matarajio yao.


Kauli ya DC Matinyi

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobhare Matinyi anasema wilaya hiyo ina watu 1,356,674 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Matinyi akizungumza na Mwananchi, amesema Temeke ina wastani wa ongezeko la watu la asilimia 4.6 kulinganisha na wastani wa nchi ambao ni asilimia 3.4.

Ili kuwa na uwiano wa ongezeko hilo na utoaji wa huduma za kijamii, zikiwamo za afya anasema mbali ya hospitali za Temeke na Mbagala Rangi Tatu ambayo kwa sasa inatumika kama ya wilaya, kuna mpango wa kujenga halisi ya wilaya Chamazi. Anasema wamepewa huko sehemu ya eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Hii ya Mbagala Rangi Tatu ni hospitali yenye hadhi ya wilaya lakini siyo. Nini maana yake? Inahitaji iwe na bajeti na vifaa vinavyowezesha kuwa ya wilaya kwa sababu inahudumia watu wengi,” anasema.

Pia anasema kutokana na wingi wa watu, wanafikiria kuongeza hospitali nyingine yenye ngazi ya wilaya itakayokuwa upande wa Temeke. Kutekeleza hilo, anasema ni ama watafute kiwanja waanze ujenzi au wapandishe hadhi kituo cha afya ili kiongezwe majengo na vifaa.

Akizungumzia wingi wa wajawazito wanaofika kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Matinyi anasema kuna suala la kimuundo ambao Serikali iliamua hospitali hiyo, Amana na Mwananyamala zitakuwa chini ya Wizara ya Afya ambayo itatoa wataalamu na vifaa.

“Kwa hiyo sisi tunachokipata ni kuwa wenyeji. Tunachoweza kufanya pale ni kusaidia vitu kwa kutumia mfumo usio wa kibajeti kama vile kuwatumia wadau wa maendeleo ambao bado hawajawa wengi. Tuna mpango wa kuwaongeza kwa kuzishawishi kampuni kurejesha sehemu ya faida kwa jamii,” anasema.

Matinyi anasema kupitia mpango huo, Mamlaka ya Bandari imewahi kuchangia vitu katika wodi ya wazazi.

Anasema wanatarajia watatumia utaratibu huo kushawishi wadau wengi zaidi kufanya hivyo, kwa sababu Manispaa ya Temeke ina viwanda vingi.Matinyi anasema kuna viwanda vikubwa 45, vya kati 158 na vidogo 175, ambavyo vinatambulika rasmi lakini pia kuna wafanyabiashara takriban 40,000.

Anasema wana mpango wa kuongea na wenye viwanda ili waheshimu utaratibu wa kurejesha kwenye jamii kulingana na mwongozo wa Serikali unaowataka pia kutoa ripoti ya namna walivyotekeleza hilo.

“Mipango yetu ya moja kwa moja iko katika Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu na mpya inayotarajiwa kujengwa katika Kata ya Chamazi.


Imeandaliwa msaada wa Bill & Melinda Gates.