Hapatoshi Othman, Babu Duni uchaguzi ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Watachuana kwenye mdahalo jijini Dar es Salaam kesho Machi 4, 2024, saa tisa alasiri.

Dar es Salaam. Hapatoshi ndani ya Chama cha ACT- Wazalendo kufuatia mpambano wa wazito wawili – Mwenyekiti Juma Duni Haji maarufu kama Babu Duni na makamu wake-Zanzibar, Othman Masoud Othman.

 Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo utakaowachagua viongozi wakuu wa kitaifa, wagombea hao wametambiana, wakieleza jinsi watakavyokijenga chama hicho endapo watashinda.

Mbali na uenyekiti, nafasi nyingine inayoonyesha kuwa na ushindani mkali ni ya Kiongozi wa Chama (KC) inayogombewa na Dorothy Semu (makamu mwenyekiti-Bara) na Mbarala Maharagande, katibu wa Idara ya haki za binadamu na makundi maalumu.

Mbarala Maharagande (kulia) akipokea fomu za kuwania nafasi ya Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo


Dorothy Semu (kulia) akipokea fomu za kuwania nafasi ya Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo

Wagombea wa nafasi hizo watakuwa na mdahalo jijini Dar es Salama, kesho saa tisa alasiri.

Kamati Kuu ya chama hicho, leo ilikuwa na kikao kilichokuwa na ajenda mbalimbali, ikiwemo kufanya uchambuzi wa majina ya baadhi ya makada waliojitokeza kuwania nafasi za juu zikiwemo za ujumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu.

Kesho asubuhi, kikao cha halmashauri kuu kitafanyika kwa ajili ya uteuzi wa wagombea hao watakaopigiwa kura na mkutano mkuu utakaoanza Machi 5, 2024.


Sababu Duni kutetea uenyekiti

Akizungumza na Mwananchi Digital jana jijini Dar es Salaam, mwenyekiti anayemaliza muda wake wa ACT- Wazalendo, Babu Duni, amesema anatetea nafasi hiyo kwa kuwa kuna mambo ya kukamilisha, ya kuleta mabadiliko ya msingi, hasa Zanzibar wanakopigania Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

“Inaitwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Serikali ya maridhiano, lakini mara zote tunaridhia sisi tu. Ikifika miaka mitano yanabaki yaleyale.

“Tunachohitaji ni kwamba, tumekomboa nchi yetu na tujenge nchi pamoja, lakini inaonekana kuna watu wanaamini kwamba nchi ni yao na sisi ni wasindikizaji,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu umri wake na kazi ngumu inayomsubiri, Babu Duni mwenye umri wa miaka 73 amesema; “Kwa nini nipumzike wakati na mimi nina nguvu, kwa nini nipumzike wakati bado nina hoja ya kuendeleza mabadiliko? Kwa nini useme nipumzike wakati demokrasia na katiba ya chama inaruhusu hivyo, kwamba yeyote anayetaka kugombea agombee?” amehoji.

Amesema amekuwepo kwenye mfumo wa vyama vingi kwa zaidi ya miaka 30, akili yake imekomaa.

“Ninayoyajua ni wachache sana wanayajua na waliweza kuyapitia. Kuna lipi ambalo sijafanya?” amehoji.

Akieleza aliyofanya tangu alipochaguliwa mwenyekiti mwaka 2020, Babu Duni amesema amekijenga chama hicho hasa Bara ambako kilikuwa hakijakita mizizi.

“Nimeenda zaidi ya mikoa 20, nimeshiriki chaguzi za marudio, kila utakapoenda wanasema ‘Babu Duni, ACT-Wazalendo Tanzania leo na kesho’. Imekuja Pandisha Tanga Shusha Tanga, chama tumekiibua mpaka sasa watu wote wanajenga matumaini kwa sababu wameona kuna watu wako serious (makini),” amesema.

Amesema awali chama hicho hakikuwa na ushindani katika uchaguzi, lakini sasa uchaguzi umekuwa na ushindani kuashiria kukua kwake.

Hata hivyo, Babu Duni amesema tangu ameonyesha nia ya kutetea kiti hicho, kuna watu wamekuwa wakimpaka tope.

“Mwenyekiti niko madarakani, wadogo wanatoka na kunisingizia mambo ambayo hayapo. Kwa hiyo, nilipochukua fomu, niliona ni nafasi ya kueleza wananchi kwamba haya hayatakiwi kufanyiana.

“Watasemaje kwamba Babu Duni anatumiwa CCM? Watasemaje kwamba Babu Duni amepewa mabilioni ya pesa, anatumika na dola? Iweje umpake tope mwenyekiti wako aliye madarakani?” amehoji.

Alipoulizwa iwapo amewapeleka kwenye kamati ya maadili ya chama hicho, amesema hakutaka kufika huko, ila ametumia nafasi yake kuyakemea.

“Kama kutuhumiwa na kupakwa tope, ni hoja ya mimi kwenda kushtaki, nishtaki nini? Nimeshafungwa bila kesi, nimeshafukuzwa kazi bila kosa, nikakosa kila kitu na bado nipo kwenye mapambano,” amesema.

Babu Duni pia amesema alishakataa zawadi za uteuzi.

“Mimi ni mjomba wake Salmin Amour, (Rais mstaafu wa Zanzibar). Alishanipa madaraka niende nikawe balozi, nikakataa. Nikamwambia kila mtu na mawazo yake, baki na mawazo yako na mimi nibaki na mawazo yangu ninayoyaamini.

“Sasa leo unakuja kuniambia kwamba eti natumiwa na CCM! Nisikubali kutumiwa wakati nina mjomba yuko madarakani, nije nitumiwe sasa?” amehoji.

Babu Duni amesema hata hatua ya baadhi ya makada wa chama hicho kumchukulia fomu mpinzani wake Othman ni kinyume cha utaratibu.

“Mimi sitaki kuwakosoa, lakini utaratibu ni wrong (si sahihi), aliyetakiwa kuchukua fomu ni makamu mwenyewe (Othman).

“Mnapotoka viongozi wa mikoa na kwenda kuchukua fomu kinyume cha utaratibu ni kuonyesha kuna mkono ukimsukuma,” amesema.

Kanuni inaruhusu

Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi wa ACT-Wazalendo, Joran Bashange alipoulizwa kuhusu malalamiko ya Babu Duni amesema:

“Sisi tumeweka very clear (wazi) na kanuni yetu inaturuhusu, kwamba mwenye malalamiko atuletee sisi kamati, ili tuchukue hatua na kama hafanyi hivyo basi anangoja kukata rufaa mwisho. Wote waliotuletea malalamiko tumeyashughulikia na hakuna anayelalamika.”

Kuhusu mgombea kuchukuliwa fomu amesema: “Ni sahihi. Kanuni zetu zinasema mgombea au wakala wake, kwa hiyo vyote vinakubalika. Hata yeye anakumbuka kwamba mwaka 2022 wakati anachaguliwa kuwa mwenyekiti alichukuliwa fomu na viongozi wa mikoa.”


Othman na mpango mkakati

AKwa upande wake, Othman Masoud Othman, makamu mwenyekiti wa ACT-Wazalendo amesema anataka kutekeleza mpango mkakati wa chama hicho, ikiwemo ahadi kwa Watanzania (Brand Promise) endapo wakifanikiwa kushika dola.

“Mimi ni mmoja wa watu wanaoweza kutekeleza brand promise kwa Watanzania, lakini pia nimejipima kwa kuzingatia maoni ya wenzangu, uwezo na uzoefu wangu kuandaa maono ya chama na kuandaa ilani ya mwaka 2020 ya ACT-Wazalendo.

“Kwa uzoefu wangu wa kutekeleza shughuli za umma, nimeona nina mambo ninayoweza kuyatekeleza nikishirikiana na viongozi wenzangu, endapo nitafanikiwa kuwa mwenyekiti," amesema Othman katika mahojiano na Mwananchi Digital leo jijiniDar es Salaam.

Alipoulizwa sababu ya kuwepo ushindani mkali katika nafasi hiyo, Othman ambaye pia ni makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema ushindani kati yake na Babu Duni na katika ngazi nyingine za uongozi, unaonyesha namna ambavyo chama hicho kinavyokua tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014.

"Ni dalili ya kukua kwa chama si katika nafasi ya uenyekiti pekee, bali hata katika ngazi ya mkoa kuna watu wazito wameangushwa sambamba na kwenye ngome pia.

"Lakini pia ni maono katika chama yanayoeleza kuwa tunahitaji kusonga mbele zaidi hasa baada ya Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe kumaliza uongozi na kutaka tujenge chama kwa kuonyesha mifano ya mabadiliko na  si hadi ajali itokee," alisema.

Othman amesema kuna baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya chama hicho wakiwemo manaibu katibu mkuu wa Zanzibar na Bara, Nassor Ahmed Mazrui na Joran Bashange wamemua kustaafu baada ya muda wao kumalizika, lakini watabaki kuwa sehemu ya ACT-Wazalendo.

“Hii ni dalili chama kinakwenda kujijenga kama taasisi na msingi wa kuangalia wakati upi tunahitaji aina gani ya uongozi,” amesema Othman.


Malalamiko ya Babu Duni

Kuhusu malalamiko aliyotoa mshindani wake, Babu Duni kwamba anapakwa tope, Othman amesema hajaona kama kuna watu wamemchafua mpinzani wake na kwamba alishamwita Babu Duni wakayazungumza, lakini hakusikia tuhuma hizo.

“Hata yeye mwenyewe anajua hilo, kwamba mimi na yeye kama watu, kama viongozi hatujawahi kuwa na mkwaruzano wowote, sasa kama kuna watu wanafanya hivyo, ni bahati mbaya.

“Sisi kama chama, wale ambao tuliwajua kwamba wanatumia mbinu chafu tumewaita na mwenyewe akiwepo, kuwaambia kwamba tumepata taarifa hizi na hili jambo ni baya, kama litaendelea tutachukua hatua,” amesema na kuongeza:

“Sisi ni viongozi, kama kungekuwa na hilo nilitarajia angeniambia kwa sababu mimi nilimwita tukazungumza zaidi ya saa moja, kuhusu hilo na hajawahi kunieleza,” alisema.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na makundi ndani ya chama hicho yanayoshindana na kwa bahati mbaya yamekuwa yakihusisha wanachama wa vyama vingine ambavyo hakuvitaja.

Mwenendo wa SUK

Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Zanzibar), amesema alipoingia madarakani, mojawapo ya kazi zake ndani ya SUK ilikuwa ni kuyapitia upya makubaliano na masharti yaliyoingiwa kati ya ACT-Wazalendo, iliyoongozwa na hayati Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Hata hivyo, amesema msingi mkubwa wa tatizo lililozaa SUK ni masuala ya uchaguzi na bado hayajatatuliwa.

“Yapo mambo ambayo tunataka yatekelezwe na ndiyo maana tumewasilisha, shida imekuwa kwenye kuyatekeleza. Sasa kama hayatekelezwi hatuoni dhamira, kwa mfano kwenye uchaguzi ndiyo msingi mkubwa wa tatizo.

“Uchaguzi una mambo mawili makubwa, kwanza una chombo cha kusimamia uchaguzi lakini kuna mfumo wenyewe wa uchaguzi, sasa unapokuwa kwenye chombo cha uchaguzi unapeleka kiongozi ambaye ni msimamizi mkuu, mkurugenzi wa uchaguzi, yuleyule ambaye alikuwa kwenye Tume ya Uchaguzi na iliharibu, unapomrudisha ukasema huyu ndiyo tena anaenda kushiriki kwenye Tume hii kwa nia ya kujenga tume nzuri, hiyo ni serious contradiction (utata mkubwa),” amesema Othman.


Babu Duni ni nani?

Juma Duni Haji aliyezaliwa Novemba 26, 1950 ni mwanasiasa na mtumishi wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aliachana na utumishi wa umma mwaka 1992 na kujiunga na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).

Miaka ya 1995, 2005 na 2010 aliteuliwa kuwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa CUF ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Mwaka 1997, aligombea uwakilishi katika jimbo la Mkunazini katika uchaguzi mdogo, lakini siku ya mwisho wa kampeni alikamatwa akiwa na baadhi ya wafuasi wake na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini na alikaa gerezani karibu miaka mitatu. Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa na Mahakama ya Rufani.

Kufuatia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaliyoanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010, Duni aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na mwaka 2014 alihamishiwa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano.

Mwaka 2015 alilazimika kujiunga na Chadema na kuwa mgombea mwenza wa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa aliyegombea urais kupitia Chadema, akivishirikisha vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na NLD vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Baada ya uchaguzi huo alirejea CUF.

Mwaka 2019 yeye na wenzake wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad walihama CUF na kujiunga na ACT Wazalendo kwa kilichoitwaShusha Tanga Pandisha Tang.


Huyu ndiye Othman

Othman Masoud Othman ni mwanasheria na mwanasiasa visiwani Zanzibar aliyezaliwa mwanzoni mwa miaka 1960 katika Kijiji cha Pandani wilayani Wete Mkoa wa Kaskazini, kisiwani Pemba.

Kwa sasa ni makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na makamu mwenyekiti wa Chama cha ACT -Wazalendo upande wa Zanzibar.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Pandani na baadaye Sekondari Fidel Castrol iliyopo Chakechake Pemba.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya Kwanza ya Sheria (LLB) na kurudi Zanzibar ambako aliajiriwa Wizara ya Katiba na Sheria kama wakili.

Alisoma Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) katika Chuo Kikuu cha London na aliporejea Zanzibar aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utawala Bora na Sheria. Baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar na ksha Mwanasheria Mkuu wa Serikali chini ya Dk Ally Mohamed Shein.

Msimamo wake katika Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014 wa kupinga muundo wa Muungano ulimfanya apoteze wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu Zanzibar na hatimaye akajunga na CUF.