Idris Sultan asimulia mwanzo mwisho Netflix

Idris Sultan asimulia mwanzo mwisho Netflix

Muktasari:

  • Mshindi wa Big Brother –Hotshots mwaka 2014, Idris Sultan amesema haikuwa rahisi kupata nafasi ya kushiriki katika filamu zinazoandaliwa na mtandao wa filamu duniani Netflix.

Dar es Salaam. Mshindi wa Big Brother –Hotshots mwaka 2014, Idris Sultan amesema haikuwa rahisi kupata nafasi ya kushiriki katika filamu zinazoandaliwa na mtandao wa filamu duniani Netflix.

Amesema ilimchukua muda mrefu kujaribu bahati yake kwa kushiriki katika usaili wa filamu mbalimbali na kufikia katika hatua nzuri kabla ya kupata kupita usaili wa filamu ya Slay.

Ameeleza hayo leo Jumatano Aprili 28, 2021 katika mahojiano maalum kwenye kipindi cha XXL cha Clouds FM.

Amesema kufanikiwa kushiriki katika filamu za mtandao huo ni jambo gumu, “Netflix hapaingiliki pale ni pagumu fulani, watu wengi wamepambania lakini leo nimefanikiwa mimi, kesho ataingia mwingine.”

Amesema filamu hiyo iliyorekodiwa Desemba 2019, ilimfunza mambo mengi na kumpa ari ya kufanya kazi zaidi.

“Ni kazi ambayo ilifanyika mwezi mzima na kipindi kile tulimaliza kila kitu, mipango ilikuwa kufanya ziara katika nchi zote ambazo zilishiriki ikiwemo Afrika Kusini, Nigeria, Congo, Ghana, Tanzania na kwingineko.”

“Lakini kwa bahati mbaya wakati maandalizi yanaanza corona ikaingilia kati hivyo tulishindwa kuendelea na mipango kama ilivyowekwa kwa kuwa ziara zingeanza Aprili 2020,” amesema Idris.

Akielezea namna alivyosota kupata nafasi Netflix, Idriss amesema, “Nimefeli katika filamu nyingi kwamba marudio ya Coming to America hii party 2 nilishafika hatua ya mwisho ila naona mambo yalikuwa mengi hasa gharama kubwa za kunitoa huku mpaka kule kwa hiyo nikaachwa wakaamua kumchukua Mwafrika aliyepo Marekani.”

“Kabla ya kufanikiwa, nilijaribu mara nyingi kuomba nafasi kupitia barua pepe na kadri alivyojibiwa niliingia  katika hatua nyingine ikiwemo kurekodi video chache kwa scene kadhaa nilizopewa na hatua nyingine nilipewa  script nzima.”

Amesema alijaribu hivyo mara nyingi lakini alitumia nafasi na kipaji chake kuhakikisha wanamwamini zaidi kwa kuonyesha utayari.

Idris amebainisha kati ya vitu vilivyomuumiza mara nyingi ilikuwa ni kuona nchi nyingine zikifanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini Tanzania haikutajwa katika mtandao huo.

“Nilidhamiria na nimeweza. Sasa hivi mpango mzima ni kuhakikisha tunafanya Netflix ya nchi yetu wenyewe inabidi sasa hivi tuingize mzigo wetu wenyewe sokoni, kwangu mimi ndoto zangu ni kuitafuta Oscars,”  amesema.

Staa huyo amesema hajawahi kuchoka kujaribu kwani kabla ya kuwa mshindi wa Big Brother Afrika mwaka 2014, aliwahi kujaribu kushiriki mara kadhaa lakini majaji wa shindano hilo walimkataa kwa kigezo cha umri wake mdogo.