Kamati yashauri mikataba itakayosainiwa itaje muda wa utekelezaji

New Content Item (1)
Kamati yashauri mikataba itakayosainiwa itaje muda wa utekelezaji

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeshauri mikataba ya utekelezaji itakayosainiwa itaje muda maalumu wa utekelezaji wa miradi ambao utazingatia maslahi mapana ya nchi ya Tanzania.


Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeshauri mikataba ya utekelezaji itakayosainiwa itaje muda maalumu wa utekelezaji wa miradi ambao utazingatia maslahi mapana ya nchi ya Tanzania.

Ushauri huo umetolewa leo Jumamosi Juni 10, 2023 bungeni Dodoma na mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso wakati akitoa maoni ya kamati kuhusu azimio la Bunge kuridhia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari Tanzania.

“Kamati inasisitiza kwamba uhai wa mikataba ya utekelezaji itakayosainiwa itaje muda maalumu wa utekelezaji wa miradi ambao utazingatia maslahi mapana ya nchi.

“Vilevile, mikataba hiyo iwe na kipengele kinachoelekeza wabia kufanya tathimini ya utekelezaji wa miradi ya uwekezaji, na kuvunja makubaliano iwapo utekelezaji huo hautafanyika kama ilivyokusudiwa,” amesema Kakoso.

Amesema Kamati imeona ni muhimu Serikali ikayazingatia kwa lengo la kuweka mazingira mazuri kwenye uandaaji wa mikataba ya utekelezaji ili kuwa na tija na kukidhi matakwa ya wananchi.

Kakoso amesema kamati inashauri mikataba ya ubia kati ya mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), DP World na kampuni nyingine izingatie maslahi ya nchi. Pia, amesema Serikali iendelee kusimamia usalama kwa kuzingatia kwamba bandari ni sehemu nyeti.

Kamati imesisitiza kwamba Serikali iendelee kukaribisha wawekezaji wengine katika maeneo ambayo hayajapata wawekezaji.

“Kwa kuwa makubaliano yanayopendekezwa kuridhiwa na yana sura ya ubia, hivyo basi, Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha kwamba ajira za Watanzania zinalindwa na kuweka mfumo thabiti wa mgawanyo wa ajira baina ya nchi wabia.

“Kuwepo na utaratibu wa kuwajengea uwezo wafanyakazi wa bandari kwa lengo la kuhaulisha ujuzi, maarifa na teknolojia; na kushirikisha kampuni ya Kitanzania katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji,” amesema Kakoso.