Kazi mpya ya Profesa Kabudi, Lukuvi hii hapa...

Muktasari:

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 10, 2022 katika hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali walioteuliwa hivi karibuni ambapo amewataja viongozi hao wawili aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Dar eS Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametolea ufafanuzi kuhusu viongozi wawili walioachwa katika baraza jipya la mawaziri lililotangazwa Jumamosi Janauri 08, 2022 huku akisema amewapangia kazi maalumu.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 10, 2022 katika hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali walioteuliwa hivi karibuni ambapo amewataja viongozi hao wawili aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

“Nina kaka zangu wawili, William Lukuvi na Palamagamba Kabudi ukiwatazama hao umri wao ni kama wangu na niliowateua hamfanani kabisa kwahiyo kaka zangu hawa nimewavuta waje kwangu ili waje wanisimamie kuwasimamia nyie kwahiyo kuwaacha kwangu kwenye ile orodha hapo wote ni wadogo na mnahitaji kusimamiwa vizuri.

 “Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndiyo kazi ninayotaka nimkabidhi sasa kindakindaki aendelee na kazi hiyo ila kazi yake kwasababu haipo kwenye muundo haitangazwi, mashirika yote kazi zote zitakazoingia ubia na Seriikali yeye ataongoza hiyo timu kwahiyo yeye ni baba mikataba,” amesema Rais Samia Suluhu Hassan

Mkuu huyo wa nchi amewataka baadhi ya viongozi na Watanzania kwa ujumla kuacha kumchafua aliyekua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akisema kuwa waziri huyo ameitumikia nchi kwa uadilifu mkubwa.

Rais Samia ameweka wazi kuwa Lukuvi hana mpango wa kugombea nafasi ya uspika kama wengine wanavyodhani.

“Kaka yangu Lukuvi yeye ana kazi na mimi mtaisikia baadae lakini ninamvuta Ikulu kazi yetu ni kuwasimamia nyie, kwasababu nikiwatamazama hapo wote wanakaribia kustaafu bado miaka miwili wengine mna safari ndefu mimi na wale tulishastaafu kwahiyo kazi yetu sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na makatibu wakuu.

“Nimeona meseji nyingi wengine wanasema afadhali Lukuvi katoka, hajatoka yupo, wengine wameanza kumletea meseji za ajabu wakijua atagombania uspika, hatagombania ana kazi na mimi msianze kumchafua ametumikia taifa hili kwa uadilifu kwa muda mrefu muacheni aende na mimi tumalie kazi atakayopangiwa,” amesema Rais.