Kesi ya Sabaya kuendelea leo, afikishwa mahakamani

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akishuka kwenye gari la Magereza kuingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Baada ya kushindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mara tatu mfululizo katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, leo amefikishwa mahakamani hapo.

Arusha. Baada ya kushindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mara tatu mfululizo katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, leo amefikishwa mahakamani hapo.

Leo Jumanne Novemba 16, 2021 Sabaya na wenzake wamefikishwa mahakamani hapo saa 9:38 asubuhi, ambapo awali kuanzia Novemba 3 hadi 5, 2021 alishindwa kufika mahakamani ambapo ikidaiwa kuwa anaumwa.

Wakili Mosses Mahuna amewaeleza waandishi wa habari nje ya mahakama kuwa mtuhumiwa huyo anasumbuliwa na vidonda vya tumbo pamoja na uti wa mgongo ambapo alidai kuwa alipata ajali akiwa kazini.

Tofauti na siku nyingine leo Sabaya ameonekana kuwa mnyonge huku akitembea taratibu.

Jana Jumatatu kesi hiyo ilishindwa kuendelea kusikilizwa baada ya watuhumiwa hao kutokufikishwa mahakamani hapo.

Hakimu Mkazi Patricia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo namba 27, 2021 aliiahirisha hadi leo ambapo shahidi wa tisa wa Jamhuri ataanza kutoa ushahidi wake.

Katika kesi hiyo watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.