Kibatala atumia vifungu vya Biblia kumhoji Luteni Urio

Muktasari:

  • Wakili wa utetezi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ametumia vifungu vya Biblia kumhoji shahidi wa 12.

Dar es Salaam. Wakili wa utetezi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ametumia vifungu vya Biblia kumhoji shahidi wa 12.

Leo Ijumaa Januari 28, 2022 shahidi huyo Luteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Denis Urio ameendelea kuhojiwa na mawakili wa utetezi baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake jana.

Kibatala ambaye ni kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi alilazimika kutumia kitabu hicho wakati akimhoji shahidi wa 12 wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, ambapo alimpelekea shahidi huyo kitabu hicho kizimbani na kumtajia vifungu kadhaa ambavyo alimtaka avisome kwa sauti.

Ifuatayo ni mahojiano baina ya mawakili wa utetezi na shahidi Luteni Urio

Leo Ijumaa Januari 28, shahidi wa 12, Luteni Denis Leo Urio anaendelea kuhojiwa na mawakili wa utetezi.

Mawakili wa pande zote pamoja na washtakiwa tayari wameshaingia mahakamani na sasa Jaji Joachim Tiganga ameingia na kesi inaitwa.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando anafanya utambulisho mawakili

Sasa kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala anafanya utambulisho wa mawakili wa utetezi.

Jaji anawaita washtakiwa mmoja mmoja kwa namba zao akianzia na mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne, ili kujiridhisha kama wote wapo mahakamani.

Wakili Kidando: Mheshimiwa Jaji shauri hili linakuja kwa ajili ya kuendele kusikilizwa na tuko tayari

Kibatala: Nasi pia Mheshimiwa Jaji tuko tayati kuendelea

Jaji anakumbusha shahidi kuwa bado yuko chini ya kiapo na wakili John Mallya anaendelea kumhoji shahidi. Anaiomba mahakama imkumbushe shahidi jibu lake la mwisho mahali alipoishia Jana.

Wakili Mallya:Hivi kazi ya VIP protection inafanyikaje?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kazi ya VIP protection inafanyikaje kwa mtu yeyote kwa kufuata sheria

Wakili Mallya:Ni sahihi hawa wanaomprotect wawe naye muda wote?

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Mallya:Kuwa VIP protection ni sawa na kuwa body guard?

Shahidi: Sijawahi kusikia.

Wakili Mallya:Mheshimiwa Jaji, naomba kielelezo (printout ya meseji kati ya Mbowe na shahidi).

Wakili Mallya anamtaka asome meseji inayosema hawa wawili kwa kuanzia si mbaya watakuwa na mimi fulltime

Wakili Mallya: Kuna meseji ambazo zinasema kuna shughuli nyingine zaidi ya ulinzi?

Shahidi: Mazungumzo ya kazi nyingine yalikuwa ni kati yangu na Mbowe ana kwa ana.

Wakili Mallya: Kwenye meseji zipo au hazipo?

Shahidi: Kwenye Meseji hazipo

Wakili Mallya anampa kielelezo kingine simu yake shahidi anamuuliza namba aliyoisevu kwa jina la Free ni ya nani

Shahidi: Namba iliyoandikwa Free Ni ya Freeman Mbowe

Wakili Mallya anampa shahidi aiwashe simu hiyo naye anaiwasha anamtaka afungue sehemu ya mawasiliano baina yake shahidi na Mbowe kwenywe mtandao wa Telegram kisha anamtaka shahidi asogee karibu na Jaji amuoneshe kwenye simu kama kuna jina Free linaonekana akiwa amefungua meseji

Shahidi: Hii ni namba

Wakili Mallya: Ukiwa umefungua meseji linaonekana?

Shahidi: Hii ni namba ya Mbowe

Wakili Mallya: Jina Free linaonekana?

Shahidi: Hii ni akaunti ya Freeman Mbowe.

Wakili Mallya: Wakati anakuongoza wakili Chavula ulisoma meseji, ulitoa maelezo kwamba hapa jina halionekani kwa sababu hizi?

Shahidi: Mimi si mtaalam wa IT?

Wakili Mallya:Ulitoa maelezo kwamba hapa jina halionekanani? Mheshimiwa Jaji naomba ajibu swali langu

Jaji: Umeelewa swali lake? Kwamba ulitoa ufafanuzi?

Shahidi: Sikutoa

Wakili Mallya:Meseji uliyoifungua Telegram yako imeanzia mwaka hani?

Shahidi: imeanzia mwaka 2020

Wakili Mallya: Meseji nyingine zimeenda wapi?

Shahidi: Alikuwa ananipigia simu

Wakili Mallya:Ukipigiwa simu kwa telegram call zinabaki?

Shahidi: Naomba nirudie nilikuwa nawasiliana na Mbowe kwa telegram, WhatsApp na simu za kawaida kwa namba ambayo si yake

Wasikilizaji: wanasonya

Jaji: Samahani jamani ninyi ni wasikilizaji mmuache shahidi atoe majibu maana naona kama mnaonesha kutokuridhika.

Wakili Mallya: Shahidi kilichokusaidia usioneshe WhatsApp call Kati yako na Mbowe ni nini?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji mimi simu nilimkabidhi na nilitakiwa nisome meseji

Wakili Mallya: Swali langu liko palepale wewe wakati unaongozwa na wakili ulionesha WhatsApp call ni hizi?

Shahidi: Sikuonesha

Wakili Mallya: Namba za watu ambao Mbowe alikuwa anakupigia ulizionesha?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji namba ambazo alikuwa anatumia za watu wengine sikuzisevu wala sikuonesha.

Shahidi: Kwa nyongeza sikuonesha kwa sababu...

Wakili Mallya: Mimi sitaki sababu

Shahidi: Sikuonesha kwa sababu.

Jaji: Shahidi sikiliza swali?

Shahidi: Sikuonesha

Wakili Mallya: Mheshimiwa Jaji naomba simu ile ambayo haikuwaka. Shahidi jana ulishindwa kuwasha hii simu, ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi

Mbowe anampatia wakili Mallya kikaratasi cha njano chenye ujumbe wa maandishi.

Wakill Mallya: Shahidi jana ulishindwa kuwasha simu hii, ni sahihi?

Shahidi: Simu haikuwaka?

Wakili Mallya:  Ulitoa explanation kwa nini haikuwaka?

Shahidi: Nilisema wakati naitambua ilikuwa ina tatizo la kuwaka na jana nimesema aidha haina chaji.

Wakili Mallya: Wakati unaipeleka kwa Insp. Swima ulieleza kuwa ilikuwa na condition gani?

Shahidi: Nilieleza kuwa ina tatizo la kuwaka

Wakili Mallya: Kama Mshtakiwa akitaka kukizitumia taarifa zake anafanyaje?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, nilieleza nilikuwa na simu moja wakaniambia zinahitajika simu zangu zote nikampelekea, lakini nilimwambia kuwa ina tatizo la display, sasa aliyechunguza ndio anajua mimi si mtaalam?

Wakili Mallya: Sasa hiyo simu utetezi wa Mbowe anauhitaji?

Jaji: Hilo ameshajibu labda ubadilishe swali.

Wakili Mallya: Jana wakati unatoa ushahidi ukionesha call log za Mbowe?

Shahidi: Sikupewa maelekezo ya kuonesha

Wakili Mallya: Call log yako na Halfan Bwire ina taarifa ya muhimu sana kuwa sasa tunakwenda kufanya ugaidi ulionesha?

Shahidi: Sikupewa maelekezo ya kuonesha

Wakili Mallya: Meseji zako kwa Ling'wenya kuwaelekeza kuwa mkienda kukiwa na ugaidi wakueleze ulionesha?

Shahidi: Sikuonesha maana sikuziona

Wakili Mallya: Shahidi kwa ufahamu wako miji ya Dar, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya na Mwanza ina jumla ya masoko mangapi?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, mimi sifahamu anayefahamu ni Mbowe ndiye aliyekuwa amepanga kulipua

Wakili Mallya: Wewe unafahamu?

Shahidi: Mimi sihitaji kufahamu

Wakili Mallya: Miji ya Moshi, Dar, Arusha, Mwanza na Mbeya ina vituo vingapi vya mafuta?

Shahidi: Mimi sijui lakini Freeman Mbowe ndio anajua akiyekua amepanga kulipua?

Jaji: Swali liko wazi, wewe unafahamu?

Shahidi: Mimi sifahamu

Wakili Mallya: Jana ulieleza kuwa ulipokwenda DCI ulionesha namba za watu wa ajabu ambazo Mbowe alikuwa anakupigia?

Shahidi: Sikueleza

Wakili Mallya: Unafahamu DCI ana vifaa vya kisasa kabisa vya kurekodi sauti?

Shahidi: Sifahamu wala DCI hakunieleza

Wakili Mallya: Unafahanu DCI ana simu za kuweza kurekodi?

Shahidi: Sifahamu maana sikwenda kufanya upelelezi?

Wakill Mallya: Wakati unawasiliana na Bwire alikueleza kuwa wanakwenda kutumia vifaa gani?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, Wakati nawasiliana na Bwire alinieleza Bro samahani tumekengeuka...

Jaji: Swali anauliza alikwambia ni vifaa gani?

Shahidi: Hakuniambia

Wakill Mallya: Kwa hiyo wewe ulifuzu mafunzo vizuri ndio maana ukapewa zawadi ya bunduki?

Shahidi: Bunduki, Mheshimiwa Jaji kwanza naona wakili anataka kuniwekea maneno mdomoni, mimi sijawahi kusikia mahali popote mtu anapewa zawadi ya bunduki, inaonesha wakili anaongea kitu asichokijua.

Wakili Mallya: Ulipokwenda Dafur ulikuwa private, Ni sahihi?

Shahidi: Si sahihi

Wakili Mallya: Ulikuwa Koplo?

Shahidi: Sahihi

Wakili Mallya: Ulikuwa officer?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, wakili anataka nielezee masuala ya mpangilio wa kijeshi jambo ambalo naona si sahihi

Jaji: Anauliza wewe ulikuwa ofisa?

Shahidi: Hapana

Wakili Mallya: Hukuwa ofisa ndio maana ulikuwa na Adamoo (Adamu Kasekwa Mshtakiwa wa pili) Sasa leo umepanda cheo unamkana.

Shahidi: Sikumbuki kama nilikuwa na Adamoo?

Wakili Mallya: Wewe una Digrii?

Shahidi: Hapana

Wakili Mallya: Lakini ni Luteni?

Shahidi: Ndio

Wakili anampa nyaraka maelezo ya Ling'wenya (Mshtakiwa wa tatu) anamuonesha mahali pa kusoma ambapo pameandikwa " Luteni Urio akitupa nauli Sh87,000 ya kwenda Moshi

Shahidi: Ilikuwa nauli ya kwenda Dar si Moshi

Wakili Mallya: Wakati unaongozwa kutoa ushahidi ulieleza namba ambayo uliokuwa unawasiliana na Bwire?

Shahidi: Sikueleza

Wakili Mallya: Mara ya kwanza kwenda kwa Afande Swila ukamkabidhi simu yako ilikuwa lini?

Shahidi: Tarehe 11/8/2020

Wakili Mallya: Ndio siku ambayo uliandika maelezo yako?

Shahidi: Ndio siku niliandika maelezo yangu.

Wakili Mallya: Ulipokwenda kwa DCI baadaye akaja Kingai, Jana ulieleza kuwa kuna mtu mwingine alikuja kuwajoin?

Shahidi: Hakuna mtu mwingine aliyekuja

Wakili Mallya: Shahidi, kwenye Meseji ya mwisho ambayo Mbowe alikutumia ukasema hukuelewa maana yake kwa nini hukumtumia sms nyingine kumuuliza hukuelewa?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, wakati Mbowe ananitumia meseji njlipata taarifa kutoka kwa Bwire, nikamuuliza bosi wenu anajua akasema anajua, na ilikuwa baada ya mwezi sina mawasiliano nayo.

Wakili Mallya: Mheshimiwa Jaji sina swali zaidi.

Wakili Dickson Matata: Shahidi nitakuuliza maswali machache na naomba ushirikiano wako, mara ya kwanza uliponana na Mbowe ilikuwa tarehe ngapi?

Shahidi: Freeman Aikael Mbowe nilionana naye mwezi wa saba tarehe za katikati, mwaka 2020

Wakili Matata: Siku hiyo ndipo alikwambia kuwa anahitaji vijana wa kuambatana naye kuwashambulia viongozi ambao hawautaki upinzani?

Shahidi: Hiyo ilikuwa ni pointi mojawapo tu

Wakili Matata: Si ndivyo alikwambia?

Shahidi: Ndio

Wakili Matata: Wakati unatoa ushahidi wako ulisema ulifanya tactical appreciation sasa na mimi nataka tufanye tactical appreciation, hayo ndiyo aliyokwambia Mbowe?

Shahidi: Ndio

Wakili Matata: Na mlikuwa wawili tu.

Shahidi: Ndio

Wakili Matata: Ukiacha siku hiyo mliyokuwa wawili kuna siku nyingine aliwahi kukueleza hayo hayo?

Shahidi: Kuna siku alikuwa ananipigia simu mara kwa mara kunisisitiza

Wakili Matata: Hakuna ushahidi wowote uliouleta hapa mahakamani wa sauti au maandishi kuthibitisha kuwa haya ndio aliyoniambia

Shahidi: Hakuna sauti

Wakili Matata: Baada ya kukwambia ukaona utoe taarifa kwa DCI, kwanza ulimpigia simu akakupa appointment

Shahidi: Sahihi

Wakili Matata: Kwamba ukipokwenda akamuita Kingi?

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Matata: Kingai ambaye alikuwa mpelelezi mkuu wa mkoa ana uzoefu na ujuzi wa kiupelelezi?

Shahidi: Ana uzoefu

Wakili Matata: Na wewe ukiwa kamanda kila jambo unalipima

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Matata: Sasa katika kikao hicho wewe au wao umuhimu wa kwamba licha ya kwamba Mbowe  amekuambia kwa mdomo bali kutengeneza ushahidi kwa voice note au kwa meseji?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji mimi nilikwenda kutoa taarifa

Wakili Matata: Hamkuona umuhimu?

Shahidi: Mamlaka ndio inajua

Wakili Matata: Sasa kwako wewe hukuona kuna umuhimu?

Shahidi: Niliona ndio maana nikawapigia kina Bwire?

Wakili Matata: Ukiachana na kina Bwire hukuona umuhimu wa kuandaa voice notes, au meseji?

Shahidi: Wakati natoa taarifa hayo Mbowe alikuwa ameshaniambia kwa hiyo alikuwa ananisisitiza tu.

Wakili Matata: Hukuona umuhimu siku ile kuwa na voice notes?

Shahidi: Sikuwa na device?

Wakili Matata: Una ushahidi gani zaidi kwamba Mbowe alikuambia hayo maneno?

Wakili Matata: Hiyo meseji Ina mahali kwamba Mbowe anataka kulipua masoko?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji Mbowe hakutaka kuzungumzia hayo kwenye simu?

Wakili Matata: Mheshimiwa Jaji swali langu hiyo meseji kuna sehemu inasema kulipua masoko?

Shahidi: Hakuna mahali inasema hivyo?

Wakili Matata: Kuna mahali inasema kuwadhuru viongozi wasiopenda upinzani?

Shahidi: Hakuna mahali inasema hivyo

Wakili Matata: Kuna mahali ilikuwa inasema kulipua vituo vya mafuta?

Shahidi: Hakuna mahali inasema hivyo?

Wakili Matata: Uliieleza mahakama wewe ulikuwa unafahamiana na DCI?

Shahidi: Nilisema wakili wa Serikali aliniuliza nikasema nilikuwa nimeshakwenda

Wakili Matata: Siyo ofisi, DCI Boaz?

Shahidi: Sikusema

Wakili Matata: Ulieleza namba ya DCI uliipata wapi?

Shahidi: Sikusema

Wakili Matata: Hiyo namba yake yenyewe uliitaja?

Shahidi: Sikuitaja?

Wakili Matata: Sasa nikisema hukumpigia simu una ushahidi wowote?

Shahidi: Ushahidi ninao na namba yake ninayo

Wakili Matata: Uliitaja?

Shahidi: Sikuitaja

Wakili Matata: Ulipokwenda kwa DCI ulifuata utaratibu wa kuingia ofisi za umma?

Shahidi: Sahihi

Wakili Matata: Na hukuieleza mahakama kwamba wewe ulikuwa na upekee wa kuingia moja kwa moja?

Shahidi: Nilisema kuwa nilifika nimejitambulisha kwa secretly kuwa mimi ni Askari wa JWTZ nina appointment na DCI

Wakili Matata: Wakati unaoongozwa ulieleza kwa nini hukufuata utaratbu?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji nimeshaeleza kuwa nilifika nimajitambulisha kama kuna utaratibu aliyepaswa kunielekeza ni yeye?

Wakili Matata: Ulisema kuwa ninyi Askari hampaswi kufuata utaratibu hukusema?

Shahidi: Sikusema

Wakili Matata: Umeleta dispatch book kuonesha siku hiyo ulikwenda kwa DCI?

Shahidi: Sikuleta

Wakili Matata: Shahidi wewe ni Askari unafuata taratibu za kijeshi unapotoka nje lazima uwe na movement order?

Shahidi: Inategemea na muda kama ni siku tatu haihitajiki?

Wakili Matata: Hayo uliyasema hapa?

Shahidi: Sikusema

Wakili Matata: Lakini pia unapokwenda kwenye ofisi za umma lazima uwe na pass?

Shahidi: Siyo kweli, pasi lazima uandike?

Wakili Matata: Umeleta pasi hapa kwamba ulikwenda ofisi ya DCI?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji sijaleta.

Wakili Matata: Na kwamba tarehe 11 na 12/8 ulikwenda kwa Swila kupeleka simu?

Shahidi: Sijaleta maana sikupewa maelekezo?

Wakili Matata: Umeleta au unaleta?

Wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hilla: Mheshimiwa Jaji shahidi amejibu kuwa hajaleta kwa sababu hakupewa maelekezo

Wakili Matata: Mheshimiwa Jaji anasema hajapewa maelekezo hizo ni sababu  mimi sizitaki sababu kwa hiyo naomba anijibu swali langu?

Shahidi: Sijaleta

Wakili Matata: Mheshimiwa Jaji naomba kielelezo namba 20 Kuna miamala yako hapa unasema Mbowe alikutumia Sh500,000 na ukatoa laki 499.

Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Kwa mantiki nyingine hukuitoa yote kwa sababu kuna makato?

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Matata: Ukichukua laki 5 ukatoa 499,000 Kuna makato shilingi ngapi?

Shahidi: Elfu moja

Wakili Matata: Shahidi naomba nikuoneshe muamala huo wa tarehe 20 mwezi wa Saba 2020, hebu nioneshe kwenye huo muamala ulitoa 499,000

Shahidi: Mheshimiwa Jaji nilitumiwa shiling lai 5 nikatoa keshi

Jaji: Anakuuliza hapo

Shahidi: Hapa haioneshi

Wakili: Kuna jedwali nina kwenda kwenye previous balance, unakubaliana na mimi kwenye akaunti yako kulikuwa na balance ya 49,646 na baada ya kuwekewa laki 5 ikawa 549,646

Shahidi: Sahihi

Wakili Matata: Siku hiyohiyoukatoa laki 3 na balance yako ikawa 243646

Shahidi: Sahihi.

Wakili: Hebu chukua salio ulilokuwa nalo utoe 243,646

Wakili wa Serikali Kidando: Wakili yuko kwenye cross examination na anauliza swali kwenye kielelezo namba 20 lakini swali hilo halijajengewa msingi kama kulikuwa na tozo kwa hiyo wakili afuate utaratibu.

Wakili Matata: Shahidi tusipoteze muda wa mahakama, Utakubaliana na mimi kwamba hapo kuna tofauti ya Sh6,000, je hayo ni makato?

Shahidi: Sijui maana unanisomea document ambayo siifahamu inawezekana ni makato au si makato.

Wakill Matata: Shahidi wakati unatoa ushahidi ulitaja hivyo vituo vya mafuta ambavyo Mbowe alitaka kulipua?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji Freeman Mbowe alitaja mikoa hakutaja vituo

Wakili Matata: Kwa hiyo ukiulizwa alitaka kulipua vituo gani Morogoro utakuwa na majibu?

Shahidi: Sitakuwa na majibu, anayo Freeman Aikael Mbowe, sina majibu

Wakili Matata: Ukiulizwa vituo alivyotaka kulipua Mwanza utakuwa na majibu hutakuwa nayo?

Shahidi: Majibu hayo mimi sina anayo Freeman Mbowe

Wakili: Shahidi nakuuliza wewe?

Shahidi: Majibu hayo Mimi sina anayo Freeman Mbowe.

Wakili Matata: Shahidi ukiulizwa ni sehemu ipi specifically aliyopanga kukata miti barabarani utakuwa na majibu?

Shahidi: Kwenye barabara ya Iringa Morogoro Hakuniambia?

Wakili Matata: Uliwataja viongozi wa Serikali aliopanga kuwashambulia?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji hakunitajia viongozi alisema tu viongozi wa Serikali ambao ni vikwazo.

Wakili Matata: Shahidi, ukiachana na kumtafutia hao vijana kuna vitu vingine alikwambia kumtafutia kama vilipuzi?

Shahidi: Hakunieleza

Wakili: Kumtafutia silaha labda kushambuliwa hao viongozi

Shahidi: Hakunieleza

Sasa ni Wakili Peter Kibatala

Wakili Kibatala:  Shahidi nikikuita Baba Careen ni sawa?

Shahidi: Sawa

Wakili Kibatala:  Baba Jackson?

Shahidi: Ni sawa

Wakili Kibatala:  Shahidi wewe ni mkristo?

Shahidi: Mimi ni Mkristo

Wakili Kibatala:  Unasali wapi, kanisa gani?

Shahidi: RC

Wakili Kibatala:  Parokia gani?

Shahidi: Parokia ni Ngerengere

Wakili Kibatala:  Paroko wako Unamfahamu?

Shahidi: Namfahamu

Wakili Kibatala:  Kateksta wako?

Shahidi: Simfahamu

Wakili Kibatala:  Nakuuliza tena kanisani mara ya mwisho ulikwenda lini?

Shahidi: Kwa pale Ngerengere Sikumbuki

Wakili Kibatala: Wewe una gari Rav4 ya Silver kutoka tarehe 16/82020 ilikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa naitumia haikuwa parked….

Wakili Kibatala: Ulipokuja kutoa ushahidi hapa gari hii umepaki wapi?

Shahidi: Mwanzoni nilikuwa nimeipaki.

Wakili Kibatala: Sikuulizi habari ya mwanzoni, nimekwambia tuna case theory, maana umekuja kutoa ushahidi hapa kutoka Morogoro na si kambini ambako ulikuwa umewekwa baada ya kutekwa...

Shahidi: Mheshimiwa samahani kunaswali hapa....

Wakili Kibatala: Shahidi relax sijakuuliza swali.

Wakili Kidando: Mheshimiwa ulishatoa maelekezo kwamba wakili anapoulizwa maswali yasiingie maneno mengine ambayo hayafahamiki, kwa hiyo yeye ajielekeze kwenye maswali

Jaji: Kibatala.

Wakili Kibatala: Wala sitajibu

Jaji: Yuko sahihi?

Wakili Kibatala: Siyo sahihi.

Wakili Kibatala: Nakuuliza tena gari yako umepaki wapi?

Shahidi: Kwenye parking ya kikosini kwangu

Wakili Kibatala: Uli register?

Shahidi: Hiyo ni parking ya Jeshi huhitaji kusajiri, unapaki kisha unaondoka na ufunguo?

Wakili Kibatala: Kwa hiyo hiyo at owner's risky?

Shahidi: Ni owners risky

Wakili Kibatala: Unafahamu kwamba bila wewe kwenda kutoa taarifa ulizozitoa kwa DCI kusingekuwa na hii kesi?

Shahidi: Nafahamu

Wakili Kibatala: Umeapa kwa Biblia, nakuomba usome Yohana 8:31-39

Shahidi anasoma

Wakili Kibatala: Unafahamu maana ya hilo neno?

Shahidi:Nafahamu

Wakili Kibatala: Lengo lake ni Nini?

Shahidi:Usiogope useme ukweli

Wakili Kibatala: Unafahamu maisha ya Bwire, Kasekwa na Ling'wenya yako mikononi mwako?

Shahidi: Nafahamu

Wakili Kibatala: Soma tena Waef 4:25-32.

Shahidi anasoma

Wakili Kibatala: Unafahamu maana ya andiko Hilo Ni nin?

Shahidi: Nafahamu, kusamehena na pia tusiseme uwongo.

Wakili Kibatala: Narudia tena Unafahamu maisha ya Bwire,Kasekwa na Ling’wenya yako mikononi mwako?

Shahidi: Nafahamu kabisa

Wakili Kibatala: Umesema Mbowe alikueleza siri ya mambo aliyokuwa anapanga kuyafanya, bila shaka alikuawa anakuamini, Unakumbuka tarehe ambayo Mbowe alikuambia hayo?

Shahidi: Sikumbuki

Wakili Kibatala: Kwa hiyo hukumbuki tarehe ambayo  Mbowe alikueleza mambo hayo mazito

Shahidi: Ilikuwa ni tarehe za katikati

Wakili Kibatala: Tarehe za katikati ni kuanzia lini?

Shahidi: Kuanzia tarehe moja mpaka 15.

Wakili Kibatala: Na wewe ni Luteni wa Jeshi tunaloliheshimu sana?

Shahidi: Kabisa

Wakili Kibatala: Jeshini una rafiki?

Shahidi: Ndio, lakini sina rafiki wa kudumu

Wakili Kibatala: Ulipopata taarifa hizi za Mbowe ulipeleka kwa nani?

Shahidi: Kwa DCI

Wakili Kibatala: Hukuona umuhimu hata wa kumueza Askofu wako labda akuombee kwa mambo haya mazito?

Shahidi: Hilo si la halihusiki.

Wakili Kibatala: Raia akipita anaona watu wanapigana hana citizenship power ya arrest?

Shahidi: Anayo

Wakili Kibatala: Mwanajeshi akikuta watu wanapigana hawezi kuwakamata mpaka akimbilie Polisi?

Shahidi: Anaweza

Wakili Kibatala: Freeman Mbowe alipokuambia taarifa hizi uliona ni kosa au si kosa?

Shahidi: Niliona ni kosa ndio maana nikatoa taarifa?

Wakili Kibatala: Hakuna Kikosi kinachohusika kuzuia ugaidi?

Shahidi: Hakuna

Wakili Kibatala: Uzuri kuna mtandao hapa unaonesha taarifa hizo , bado unakataa mbali na taarifa hizi?

Shahidi: Sifahamu Kikosi hicho sijawahi kukisikia

Wakili Kibatala: Jeshini kuna kikosi cha uchunguzi na utambuzi?

Shahidi: Ndio

Wakili: Bado Hukuona umuhimu wa taarifa hizi kumweleza mtu yeyote jeshini?

Shahidi: Hizi ni taarifa za Polisi ndio wanaohusika na uchunguzi.

Wakili Kibatala: Kwani jeshi halina mamlaka ya kupokea taarifa hizo?

Shahidi: Jeshi linashughulika na taarifa zinazohusika na masuala ya Jeshi kwa uhalifu wa uraiani ni polisi ndio wanahusika.

Wakili Kibatala: Kwani kama Mbowe alipanga kulipua kituo cha mafuta Mwenge , kinaweza kuiathiri kambi ya Jeshi iliyoko pale?

Shahidi: Ingeweza kuathiri

Wakili Kibatala: Jeshi hawana mamlaka ya moja kwa moja kushughulika na masuala yanayowaathiri?

Shahidi: Linaweza

Wakili Kibatala: Ulisema ulipata taarifa za Mbowe wito ukiwa wapi?

Shahidi: Temeke, Mgulani?

Wakili Kibatala: Kwani kambi ya Mgulani na kwa DCI wapi ilikuwa karibu?

Shahidi: Inategemeana na geographical position

Wakili Kibatala: Unafahamu kuwa DCI ni kama Waziri Mkuu kwa naana anachunguza mambo madudu mengi?

Shahidi: Nafahamu

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji kwamba Ulipokwenda kwa DCI kuna mtu akijiridhisha na wewe kwanza kabla ya kuingia ofisini kwa DCI?

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Unafamu kwa DCI Kuna utaratibu wa kuacha simu mlangoni?

Shahidi: Sijawahi kuacha simu?

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji kuwa wakati unamsubiri DCI mtu muhimu yule, waziri mkuu wa Jeshi la Polisi ulikuwa na mtu pale,

Shahidi: Nilikuwa na msaidizi wake

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji?

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Uliweza kum-describe DCI kuelezea haiba yake umri wake umbile gani ili tuweze kuamini kuwa kweli ulikwenda kwa DCI?

Shahidi: DCI anafahamika

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji ulitokaje hapo mwenye hilo jengo?

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Ulisema ulibadilishana namba na ACP Kingai, ulimtajia Jaji namba muhimu kama hiyo?

Shahidi: Sikumtajia

Wakili Kibatala: Jana ulioneshwa simu zako, wakati umepewa moja baada ya nyingine ulimuomba jaji ruhusa kwamba naomba nichungulie phone book ningalie namba ya Kingai ambayo mlibadilishana?  

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Na namba ya DCI pia ulimuomba Jaji kuangalia ili umtajie?

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Mheshimiwa Jaji Sasa hivi naona ni saa 7 na utaratibu wetu ni kwamba tunapaswa kub-reak na Nina propose dakika 45 kama wenzetu hawatakuwa na pingamizi.

Wakili Kidando: Mheshimiwa Jaji hatuna pingamizi.

Jaji: Ninaahirisha shauri hili kwa dakika 45.

Mahakama imerejea baada ya mapumziko kwa ajili ya Wakili wa utetezi Peter Kibatala kuendelea kumuhoji shahidi wa 12 Luteni Denis Urio.

Jaji ameingia na mawakili wa pande zote wako tayari kuendelea.

Wakili Kibatala: Unafahamu utambulisho wa simu ni IMEI

Shahidi: Nafahamu

Wakili Kibatala: Unakumbuka uliongozwa kutoa nyaraka kwa ajili ya utambuzi

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Ilikuwa ya utambuzi wa nini nyaraka ya makabidhiano ya simu

Shahidi:Utambuzi wa simu

Wakili Kibatala: Mwambie muheshimiwa Jaji kama wakati unaaongozwa kutambua simu moja moja kwa IMEI zake

Shahidi:Nilitambua simu moja ya Tecno Camon

Wakili Kibatala: Ulisema unaishi Ngerengere

Shahidi:Ni sahihi

Wakili Kibatala: Kuna sehemu ulisema unaishi kihonda

Shahidi : Hapana

Wakili Kibatala: Tafuta sehemu ilipoandikwa Tecno Camon kwenye hii nyaraka

Shahidi: Hakuna

Wakili Kibatala: Imeandikwa nini

Shahidi:Tecno

Wakili Kibatala: Angali hii hati ya makabidhiano kwenye kielelezo hili imeandikwa unaishi wapi

Shahidi: Kihonda

Wakili Kibatala: Kuna sehemu ulimwambia muheshimiwa Jaji katika ushahidi wako unaishi Kihonda

Shahidi: Sikusema

Wakili Kibatala: Aliyemkabidhi Inspekta Swilla simu aandike IMEI nani

Shahidi: Mimi akaandika yeye

Wakili Kibatala: kwa hiyo aliandika bila wewe kuwepo

Shahidi:Nilimkabidhi akaandika nikiwepo

Wakili Kibatala: Ulimwambia Mheshimiwa Jaji kama ulishuhudia Inspekta Swilla alisaini

Shahidi:Sikusema

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba nyaraka hii tunaweza kujua nini kama wewe haupo

Shahidi: Mimi sina utaalamu anajua mpelelezi

Wakili Kibatala: Ulisema unafahamu ofisini ya DCI

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: Ni sahihi unafahamu meza na viti vilivyoko ofisi ya DCI

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: Mwambie Mheshimiwa Jaji iwapo ulimwambia meza ya DCI ina rangi gani

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Mwambie muheshimiwa Jaji kama ulimwambia nyuma ya kiti cha DCI kuna bendera

Shahidi: Sikumwambia

Wakili: Mwambie muheshimiwa Jaji kama ulisema ukutani kuna picha mbalimbali

Shahidi:Sikumwambia

Wakili Kibatala: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama ulimwambia iwapo kwenye ile gorofa ya saba kuna ofisi nyingine

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Pale mapokezi ulimwambia kulikuwa na askari wangapi wa zamu

Shahidi:  Sikumwambia

Wakili Kibatala: Ulimwambia kama pale nje ya ofisi huwa kuna egeshwa magari

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Umepokea taarifa Kutoka kwa Freeman Mbowe na Afisa wa Jeshi hawezi kuona uhalifu unatokea ulimwambia Jaji kwa nini hukumuweka chini ya ulinzi?

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Unakumbuka kwa DCI ulienda baada ya tarehe 18/7,2020 au kabla

Shahidi: Sikumbuki

Wakili Kibatala: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama una kitu kingine kitakachoonyesha ulienda kwa DCI kabla ya tarehe 18 /7,2020  

Shahidi:Hakuna

Wakili Kibatala: Mtu wa kwanza kuwasiliana nae ni nani

Shahidi: Mose Lijenje

Wakili Kibatala: Tuambie mtu wa kwanza kuwasiliana nae akiwa Tunduma ni tarehe ngapi

Shahidi: Sikumbuki

Wakili Kibatala: Kutoka tarehe 18 hadi 24/7,2020 ni siku ngapi

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Na walikuwa hawafahamiani na Mbowe

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: Ni nini kilichofanya Swilla afungue kesi tarehe 18 /7,2020 siku mbili kabla ya kuwatafuta

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Wewe ulikula njama na Mbowe

Shahidi: Sijala njama

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji kutoka kwa DCI kwenda Morogoro ulitumia gari gani

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Baada ya kutoka kwa DCI ulifika nyumbani usiku

Shahidi: Ilikuwa saa kumi

Wakili Kibatala: Mwambie Jaji nani ulimkuta nani

Shahidi: Alikuwa mke wangu

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji kama mwanao Careen alikuwepo

Shahidi: Wanangu wote walikuwepo

Wakili Kibatala: Unafahamu kila gari inavyoingia hoteli huwa inasajiliwa

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji kama dereva alisajili gari pale

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji kama hoteli ya casam ni nyumba ya kawaida au gorofa

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Unajua Freeman Mbowe akiwa pale casam hotel huwa anahudumiwa na mtu mmoja

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji mhudumu alivyokuwa amevaa

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji Mbowe alivyokuwa amevaa

Wakili Kibatala: Afisa wa jeshi unafunga safari kufuata mtu usiemjua?

Shahidi: Nilikuwa namfahamu kwa kuwa tulikuwa tunawasiliana

Wakili Kibatala: Unafahamu casam hotel ina camera na ulienda na Rav 4 yako ya Silva

Shahidi: Sikwenda na gari

Wakili Kibatala: Pale casam hoteli ulilipia chochote

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Nani alikulipia

Shahidi: Freeman Mbowe

Wakili Kibatala: Na aliyekulipia usafiri

Shahidi: Freeman Mbowe

Wakili Kibatala: Ukapokea fadhila za mtu aliyekwambia mambo ya kufanya ugaidi

Shahidi: Sio fadhila

Wakili Kibatala: Baada ya kutoka kwa DCI hukwenda kumwambia mtu yoyote

Shahidi: Nlimwambia CO wangu

Wakili Kibatala: Lini

Shahidi: Tarehe 5/8/2020

Wakili Kibatala: Ulimtajia Jaji jana kuwa uliripoti kwa CO wangu wakati ukiongozwa na wakili Chavula

Shahidi: Sikumbuki

Wakili Kibatala: Pamoja na Mbowe kukwambia anapanga mambo ya kihalifu uliendelea kuwasiliana nae?

Shahidi: Niliendelea kuwasiliana nae

Wakili Kibatala: Bila kujali kama ulitumiwa au hukutumwa ulishiriki kwenye mipango ya kigaidi

Shahidi: Sikushiriki

Wakili Kibatala: Ulishiriki

Shahidi: Sikushiriki

Wakili Kibatala: Kuna sheria inayomruhusu mwanajeshi kushiriki kufanya uhalifu ili kumpata mhalifu mkuu  

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Ungeeleweka kama ingefahamika kama unawasiliana kwa simu na Kiongozi wa waasi

Shahidi: Ni singeeleweka

Wakili Kibatala: Kwa kuwa alikuwa mhalifu wa amani

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: lakini huku ukawa unawasiliana na Freeman Mbowe

Shahidi: Nilikuja kufahamu baadae

Wakili Kibatala: Wakati unawasiliana na Mbowe ulitoa taarifa kwa mtu yoyote jeshini

Shahidi: Nilikuja kutoa taarifa baadae

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji ulikuwa Unamfahamu Adamoo ni jina lake la utani jeshini

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji Lijenje jina lake maarufu ni Kakobe

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala:. Ni ushahidi wako Lijenje wakati anatoka hadi mnakutana anaenda kufanya kazi ya ulinzi

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: Huyu Lijenje yuko wapi

Shahidi: Sifahamu yuko kwa Freeman Mbowe

Wakili Kibatala: Nikisema amekufa

Shahidi: Mimi sijui nilimpakia  akaenda kwa Freeman Mbowe

Wakili Kibatala: Tunakubaliana hadi anatoa Morogoro alikuwa hajui mambo ya ugaidi

Shahidi: Alikuwa anaenda kufanya kazi ya ulinzi

Wakili Kibatala: Ulikutana lini na Lijenje Morogoro

Shahidi: Tarehe 21/7,2020

Wakili Kibatala: Baada ya hapo lini uliwasiliana nae tena

Shahidi:  Sijawasiliana nae tena

Wakili Kibatala: Kuna nini unaweza kudhibitisha kuwa Mbowe alimwambia Lijenje wakafanye vitendo vya kigaidi

Shahidi: Hakuna

Wakili Kibatala: Kuna sehemu yoyote Mbowe aliwahi kutoa hela akampa Lijenje

Shahidi: Alituma fedha nikampa

Wakili Kibatala: Unajua maana ya utakatishaji fedha

Shahidi: Nafahamu

Wakili Kibatala: Kuna fedha Mbowe alituma ulimuhamishia moja kwa moja au ulimpa ya kwako

Shahidi: Niltoa 300, 000 nikaongezea na za kwangu nikampa

Wakili Kibatala: Ulitumiwa 500,000 na Mbowe na mfukoni ulikuwa na hela

Shahidi: Nilienda kwa wakala nikatoa 300,000 nilikuwa na hela mfukoni Sh200, 000

Wakili Kibatala: Kwahiyo ulimkata Mbowe Sh10000

Shahidi: Nilijikata mimi

Wakili Kibatala: 499, 000 uliyotoa ilitokea wapi?

Shahidi: Kama nisingekuwa na hela kwenye akaunti yangu ningepata pungufu

Wakili Kibatala: Kwa hiyo aliyekata 1000 ni nani

Shahidi: Wakala

Wakili Kibatala: 200, 000 iliyobaki kwenye simu uliitoa lini ?

Shahidi: Kimya

Wakili Kibatala: Naomba kielelezo namba 20, naomba nitafutie sehemu ukiona tuambie ulikitoa lini

Wakili Chavula: Kielelezo hiki sio cha shahidi na wakili hajajenga msingi angemuelekeza kuepusha mahakama kupotoshwa

Wakili Kibatala: Namuonyesha kwa ruhusa ya mahakama.

Shahidi. Niliitoa kabla ya tarehe 30/7,2020

Wakili Kibatala: Nitafutie hapo niambie hiyo 200, 000

Shahidi: 200, 000 hamna

Wakili Kibatala: Ulisema baadae Mbowe alikutumia Sh199, 000

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: Ilikuwa tarehe ngapi

Shahidi: 27 /7,2020

Wakili Kibatala: Alikutumia nani

Shahidi: Wakla

Wakili Kibatala: Ukaitoa lini

Shahidi. Tarehe 24,/7,2020

Wakili Kibatala: Ukaitoa yote

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Nitafutie hapo kwenye kielelezo

Shahidi: Haionekani.

Wakili Kibatala: Tarehe 22/7,2020 kuna muamala wa 190, 000 unakumbuka ulimtumia nani fedha

Shahidi: Sikumbuki

Wakili Kibatala: Ulisema 200, 000 haiwezi kuonekana kuna maelezo yoyote Ulitoa kwa Jaji

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Ulipompa Lijenje fedha ulimsainisha

Shahidi: Sikumsainisha yoyote

Wakili Kibatala: Kuna ujumbe wowote kwenye simu unaonysha Lijenje kupokea fedha

Shahidi: Hakuna lakini walipokea

Wakili Kibatala: Niambie ni kazi gani Lijenje alipewa majukumu gani ya kigaidi

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Unafahamu wapi Lijenje alikuwa akiishi Moshi

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Una ushahidi wa kimaandishi Ukionyesha ulimsainisha Bwire

Shahidi: Hakuna

Wakili Kibatala: Una ushahidi wa maandishi kuwa Bwire akifika kwa Freeman Mbowe

Shahidi: Hakuna

Wakili Kibatala: Bwire alipewa jukumu gani la Kigaidi?

Shahidi: Kwenda kumdhuru Sabaya

Wakili Kibatala: Alikwambia anaenda kumdhuru lini

Shahidi: Kabla ya tarehe 7/8/2020 na kabla ya tarehe 12 watakuwa Dar es Salaam

Wakili Kibatala: Bwire aliwahi kukwambia kuhusu Bastora A5340

Shahidi: Hajawahi kuniambia

Wakili Kibatala: Aliwahi kukwambia kuhusu kukaa kikao kwa ajili ya kwenda kumdhuru Sabaya

Shahidi: Hakuwahi

Wakili Kibatala: Baada ya kuwa unawasiliana na Bwire akakupa taarifa uliwahi kwenda kwa DCI

Shahidi: Nlikuwa nawasiliana na Kingai

Wakili Kibatala: Taarifa muhimu na nzito kwa nini hukumwambia Kingai

Shahidi: Nlimwambia

Wakili Kibatala: Ni sahihi uliwaambi waende wakishafanya uhalifu waje wakwambie

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: DCI alikwambia kama Bwire Amekamatwa

Shahidi: Hakuniambia

Wakili Kibatala: Kingai alikwambia kama Bwire amekamatwa

Shahidi: Hakuniambia

Wakili Kibatala: Ni nani alikwambia Bwire kakamatwa

Shahidi: Niliona kwenye vyombo vya habari

Wakili Kibatala: Unakumbuka uliieleza kuwasilisha simu kwa Inspekta Swilla

Shahidi: Nakumbuka

Wakili Kibatala: Unakumbuka ni karatasi ngapi ulikabidhi hapa mahakamani

Shahidi: Karatasi moja

Wakili Kibatala: Ulimwambia Mheshimiwa Jaji ni kwa nini hukutoa karatasi nyingine

Shahidi: Sikupewa ningepewa ningetoa

Wakili Kibatala: Unakumbuka ulikuwa unawasiliana na Kingai mara kwa mara

Shahidi: Sio mara kwa mara.

Wakili Kibatala: Wewe ni Luteni wa jeshi

Shahidi. Ni sahihi

Wakili Kibatala: Unafahamu base intelligence

Shahidi: Nafahamu

Wakili Kibatala: Wakati unaulizwa ulisema ufahamu namna ya kurekodi ulifafanua siku moja yoyote uliwahi kupiga simu ukaweka loudspeaker ili mtu mwingine angalau asikie

Shahidi: Mbowe hakunipigia simu

Wakili Kibatala: Hukumkabidhi Inspekta Swilla simu na chaji

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: Na ni ushahidi wako simu hizo ulizikabidhi zaidi ya mwaka mmoja na nusu

Shahid: Sahihi

Wakili Kibatala: Ulimfafanulia Mheshimiwa Jaji kuwa simu yako inauwezo wakutunza chaji kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu

Shahidi: Sikusema

Wakili Kibatala: Na hukuieleza kama simu zako nyingine kama zina uwezo wa kuitunza chaji kwa zaidi ya Mwaka mmoja na nusu

Shahidi: Ni sahihi

Wakili Kibatala: Wakati ulikabidhi Inspekta Swilla simu ilikuwa na chaji kiasi gani

Shahidi: Chini ya nusu

Wakili Kibatala: Kwa mujibu wa kanuni za jeshi mnaruhusiwa kuwa na miamala ya kifedha kama mlivyokuwa mnafanya

Shahidi: Ukiwa kazini huruhusiwi lakini mkiwa kambini mnaruhusiwa

Wakili Kibatala: Kama ofisa ulikuwa na jukumu la kutoa taarifa ya ufanyaji wa miamala ya fedha?

Shahidi: Lilikuwepo

Wakili Kibatala: Ulimwambia Jaji katika kipindi chote uliwahi kutumiwa fedha kabla ya tarehe 20/7,2020

Shahidi: Haikuwa muhimu

Wakili Kibatala: Kuna hii namba yako nyingine uliambiwa kama inaonekana kwenye ripoti ya uchunguzi

Shahidi: Sikumwambia

Wakili Kibatala: Unafahamu Bwire alishakuwa bodgurd wa kijeshi

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Mbowe umeanza kufahamiana nae 2003 au 2008

Shahidi: Mwaka 2008

Wakili Kibatala: Ukitoa Sabaya hao viongozi wengine ambao walitaka kudhuriwa huwajui

Shahidi: Hata Sabaya nlikuwa simjui

Wakili Kibatala: CDF ni Kiongozi wa Kimataifa au sio Kiongozi wa kitaifa

Shahidi: Ni kiongozi wa Kitaifa

Wakili Kibatala: Suala lake linaweza kushughulikiwa na jeshi au haliwezi

Shahidi: Linaweza

Wakili Kibatala: Na waziri wa Ulinzi je?

Shahidi: Ni Kiongozi wa Kitaifa

Wakili Kibatala: Suala lake haliwezi kushughulikiwa na jeshi

Shahidi: Linaweza.

Wakili Kibatala: Mheshimiwa Jaji naomba kutoa hoja. Imefika saa 11 na bado nina maswali kwa shahidi naomba kuahirisha shauri hili hadi Jumatatu tarehe 31/1/2022 kwa ajili ya kuendelea kumuhoji

Wakili Kidando: Hatuna pingamizi Mheshimiwa Jaji.

Jaji: Kufuatia muda na maombi yaliyoletwa na upande wa utetezi na kuridhiwa na upande wa mashtaka na ahirisha kesi hii hadi Jumatatu Januari 31, 2022 Shahidi unakumbushwa kuja kuendelea na ushahidi wako ambapo upande wa utetezi wataendelea kukuhoji.