Kikongwe wa miaka 90 amaliza mbio za kilometa 10

Fatuma Issa akikimbia umbali wa kilomita 10 katika mbio za Korosho msimu wa pili zilizofanyika leo mkoani Mtwara ambazo zimeandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Mbio za korosho msimu wa pili zilizohudhuriwa na wakimbiaji zaidi ya 1,200 ambapo miongoni mwao wakiwemo vikongwe wengi ambao wajigamba kuwashinda vijana kukimbia na kusema kuwa hawana nguvu.
Mtwara. Msimu wa pili wa mbio za korosho umefanyika leo mkoani Mtwara na kuhudhuriwa na zaidi ya wakimbiaji 1,200 huku mbio hizo zikihudhuriwa na vikongwe wengi huku vijana wakilalamikia kushindwa kukimbia.
Akizungumza mara baada ya kumaliza mbio za kilomita (10) mzee Mashaka Maluya (90) mkazi wa Dodoma majengo amesema kuwa ameanza kukimbia akiwa kijana lakini anasikitishwa na vijana wa siku hizi kuwa wavivu.
“Yaani nimeanza kukimbia tangu nikiwa kijana tatizo la vijana wa siku hizi wamezidi uvivu hawafanyi mazoezi unajua kwa umri huu nimewazidi zaidi ya 40 wako nyuma yangu lakini enzi nzagu ningeweza kushinda kabisa nimekimbia kilomita 10,” amesema.
“Wakati tunaanza nilianza kukimbia kidogo kidogo mwishoni nikaweza siyo kama wazee wengine wanajidekeza yaani hata washiriki niliokuwa nao wamechoka hata kukimbia hawawezi,” amesema Maluya.
Nae Fatuma Issa (80) amesema siri kubwa ya mafanikio yake ni mazoezi ambayo huwa anafanya mara kwa mara ili kuweka vizuri mwili na kuepusha magonjwa na matatizo mengine yasiyoyalazima kiafya.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred amesema kuwa mbio hizo zimehudhuriwa na wakimbiaji 1,200.
“Lengo ni kuwakutanisha pamoja watu mbalimbali wakimbie lakini wale korosho na kuweza kufahamu bidhaa zitokanazo na korosho ambapo tumeshuhudia ongezeko la wakimbiaji zaidi ya 1,200 hii kwetu ni hatua kubwa,” amesema.
“Mbio hizi zinalenga kuhamasisha ulaji wa bidhaa zotokanazo na korosho ambazo ni fursa kwa wadau kujitokeza zaidi ili kuongeza ubanguajia, matumizi ya korosho na kuboresha uchumi wetu kwa kutumia zao la korosho,” amesema Alfred.