Kikwete apigia chapuo teknolojia kufikia mapinduzi ya viwanda
Muktasari:
- Amesema pamoja na juhudi zinazofamyika katika sekta ya elimu, jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha Tanzania haiachwi nyuma.
Dar es Salaam. Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema licha ya Serikali za awamu zote kuchukua hatua mbalimbali za kuleta mabadiliko kwenye sekta ya elimu, bado kazi kubwa inahitajika kufanyika kuhakikika Tanzania inakwenda sambamba na kasi ya mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanatagemea zaidi teknolojia.
Kikwete amesema hayo leo, Novemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la ubora wa elimu ikiwa ni muda mfupi baada ya kukabidhiwa tuzo na Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) iliyotambua mchango wake kwenye sekta ya elimu.
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Global Partners for Education (GPE), amesema hakuna awamu ya uongozi ambayo imemaliza kazi yote inayotakiwa kufanyika kwenye sekta ya elimu, licha ya sifa nyingi kuelekezwa kwenye uongozi wake.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Kikwete amesema pamoja na hatua zinazoendelea kupigwa, bado jitihada zaidi zinahitajika kufanyika kuhakikisha Tanzania haiachwi nyuma wakati dunia inaendelea kusonga mbele.
“Mmenipa sifa nyingi kwa jitihada nilizofanya wakati wa uongozi wangu na kunipatia hii tuzo, naipokea na kuipeleka kwa wote ambao walifanya kazi kubwa kuhakikisha sekta ya elimu inapiga hatua ila ukweli ni kwamba sikuyamaliza yote.
“Mimi nilipewa jukumu la kujenga shule za kata, ili wanafunzi waendelee na elimu ya sekondari hilo lilifanyika na tuna shule za kata, lakini miezi sita baada ya kutoka kwenye uongozi nilikutaja na kijana wa miaka 15 kule katikati ya Tabora na Nzege hajawahi kwenda shule, ingawa anatamani kusoma, sasa ukijuliza kuna watoto wangapi wa namna hii hawajapelekwa shuleni?” amehoji.
Kikwete amebainisha kuwa Rais aliyemfuata, John Magufuli chama kilimuelekeza kuhakikisha elimu inatolewa bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita na akatekeleza agizo hilo, lakini bado changamoto zimeendelea kuwepo.
“Samia naye ameingia amefanya mengi, ila bado kuna kazi kubwa inahitajika kuendelea kufanyika kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora kwa kuwa sasa tumejikita kwenye ubora, tofauti wakati ule naingia madarakani kipaumbele kilikuwa upatikanaji wa elimu kwanza.
“Baada ya shule za kata kujengwa kazi niliyoiacha ilikuwa kuhakikisha ubora wa elimu inayotolewa unazingatiwa na hilo limefanyika kwa kiasi kikubwa tunaona zipo shule za kata zinafanya vizuri hata pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanafunzi wengi tunaowapokea ni kutoka shule za kata,” amesema Kikwete.
Akitolea mfano mowajapo ya sekondari ya kata wilayani Kilindi iliyokuwa na wanafunzi 56 kati ya hao 54 walipata daraja la kwanza na wawili daraja la pili, matokeo yaliyomfanya afunge safari kwenda kumuona mkuu wa shule hiyo.
Amesema katika kipindi hiki ambacho mapinduzi ya nne ya viwanda yameshika hatamu, Tanzania inapaswa kuendana na maendeleo hayo kwa kuwa dunia haitatusubiri.
Akifungua kongamano hilo, Naibu Katibu Mkuu Tamisemi Dk Charles Msonde amesema mkutano huo umefanyika wakati mwafaka ikizingatiwa Tanzania inafanya jitihada kuboresha elimu.
“Jitahada nyingi zimefanyika kuhakikisha tunakuwa na elimu bora ikiwemo kuongezea miundombinu, kuboresha ufundishaji, mapitio ya sera na mitaala haya yote yanalenga kuwa na elimu inayoendana na uhitaji wa dunia.
“Kufanikisha yote haya ni lazima uwepo ushirikiano wa kutosha kati ya Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na mashirika yanayojihusisha na elimu kwa pamoja tuunganishe nguvu kuhakikisha tunakuwa na elimu bora,” amesema Dk Msonde.
Mratibu wa Tenmet, Ochola Wayoga amesema kufanyika kwa kongamano kunatoa fursa kwa wadau wa elimu ikiwepo Serikali, watunga sera, vyuo vikuu, wanafunzi, walimu, watafiti, taasisi za elimu, mashirika ya umma na binafsi na wadau wa elimu wa ndani na nje ya nchi kujadili hali ya ubora wa elimu.
Amesema hatua hiyo inalenga kubadilishana mawazo na kushirikishana uzoefu kwa lengo la kuboresha utoaji wake na kuunda mustakabali bora wa utoaji elimu hapa nchini.
Wayoga amebainisha matarajio ya kongamano hilo ni kutoa fursa na njia kwa watunga sera, watafiti, wasomi, wadau, wanafunzi na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Afrika, kujadiliana na kushirikishana uzoefu wao na maarifa juu ya nafasi ya elimu ya katika kukabili mabadiliko yanayokabili ulimwengu sasa.
Kongamano hilo limehusisha washiriki kutoka katika zaidi ya nchi 10 za Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda , Ethiopia, Lesotho, Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Sudani Kusini na Sudan.