Lowassa ‘Mzee wa maamuzi magumu’

Muktasari:

  • Edward Lowassa alisifika kama mchapakazi hodari na msimamizi wa moja kwa moja wa shughuli za Serikali.

Dodoma. ‘Ni Mzee wa maamuzi magumu.’ Ndivyo alivyofahamika kwa jina la utani, Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa tisa kushika madaraka hayo.

Lowassa alishika rasmi wadhifa wa Waziri Mkuu kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008. Ni takriban miaka miwili.

Katika kipindi hicho cha uwaziri mkuu, Lowassa alisimamia bajeti mbili kwenye utawala wake, bajeti ya Julai 2006 hadi Juni 2007 na bajeti ya Julai 2007 hadi Juni 2008.

Pia, ni Waziri Mkuu wa kwanza tangu Uhuru wa Tanganyika kuhama chama tawala cha CCM na kwenda kujiunga na chama cha upinzani Chadema, akifuatiwa na Waziri Mkuu mwingine, Frederick Sumaye.

Lowassa pia ni kati ya mawaziri wakuu watatu waliowahi kuwania urais mara mbili na kushindwa. Wengine ni John Malecela (1995 na 2005), Frederick Sumaye (2005 na 2015).

Mawaziri wakuu wengine waliopita ni Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye, Mizengo Pinda na sasa Kassim Majaliwa.

Wakati akiwa Waziri Mkuu, Lowassa alisifika kama mchapakazi hodari na msimamiaji wa moja kwa moja wa shughuli za Serikali na hadi kupachikwa jina la utani la ‘Mzee wa maamuzi magumu.’

Lowassa aliwahi kukataa kuelezwa historia ya Kigoma wakati akisomewa taarifa ya mkoa akisema historia ya mkoa huo anaijua tangu akiwa shuleni na anachotaka kujua walivyojipanga kuchochea uchumi wa mkoa huo.

Pia, akiwa kwenye tukio la kupata taarifa ya mkoa, alielezwa changamoto wanayopata wakulima ni pembejeo kwa kuwa bei ilikuwa haijatangazwa.

Kwa kuwa kwenye msafara wake alikuwapo Waziri wa Kilimo kwa wakati huo, Joseph Mungai alimuamuru atangaze bei hapo. Mungai alijitetea wangetangaza wenzake Dar es Salaam kwa kuita vyombo vya habari.

Majibu hayo hayakumridhisha Lowassa, alimtaka atangaze papo hapo kwa kuwa kwenye msafara wake kulikuwa na waandishi wa habari aliotoka nao Dar es Salaam.

Ulikuwa wakati mgumu kwa Mungai kwa kuwa hakuwa na taarifa kamili na alilazimika kuomba ruhusa ya dakika chache apige simu Dar es Salaam kupata taarifa kamili, na alitangaza bei hapo.

Wakati Rais Jakaya Kikwete akiingia madarakani mwaka 2005, ujambazi nchini ulikuwa umefikia kiwango cha kutisha. Hata hivyo, kuna wakati Waziri Mkuu wake Lowassa aliutangazia umma namna Serikali ilivyomaliza ujambazi.

Lowassa alitumia neno kwamba Serikali imefanikiwa kuuvunja uti wa mgongo wa ujambazi na sasa hali ni shwari.


Maamuzi magumu

Maamuzi magumu ilikuwa kaulimbiu ya kiutendaji ya Lowassa alipokuwa Waziri Mkuu chini ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Lowassa alifanya maamuzi magumu halisi yenye kupimika na muonekano dhahiri au kwa vitendo uwezavyo kuvishuhudia katika ubora wake.


Ujenzi shule za kata

Lowassa ni mashuhuri kwa kusimamia mpango wa Serikali uliofanikiwa wa ujenzi wa shule za kata ambazo ziliiletea Tanzania sifa kubwa kwa kutoa fursa ya watoto wengi kupata nafasi shuleni.

Mwanzoni mwa 2006, Lowassa alitoa maelekezo mawili muhimu kuhusu elimu ya shule za sekondari.

Lowassa alitaka kila kata lazima iwe na shule ya sekondari na pia isipungue asilimia 75 ya wanafunzi waliofaulu mitihani wawe wamejiunga sekondari ifikapo Aprili 1, 2006.

Kabla ya hapo shule hizo zilizoanza kujengwa wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa hazikuitwa shule za kata. Na zilikuwa chache.

Ujenzi wa shule za kata ulifanyika baada ya Lowassa kuchukua uamuzi wa kuwaita wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa mikoa na aliwaagiza kujenga haraka shule za kata kwa ukombozi wa Watanzania.

Baada ya hapo shule zote zilizojengwa kabla pamoja na mpya za Lowassa ndiyo zikaitwa shule za kata.

Machi, 2006, wanafunzi walianza kujiunga na shule hizo, baada Lowassa kutoa agizo kwa wakurugenzi kuhakikisha wanakamilisha shule hizo ikiwa ni pamoja na kuchangisha wazazi wa kila kata.

Baada ya ujenzi wa shule hizo ilianza operesheni ya walimu waliokuwa wanaitwa ‘vodafasta’ vijana wengi walichukuliwa katika utaratibu huu ili kuziba pengo la uhaba wa walimu kwenye shule hizo.


Ujenzi wa Udom

Japokuwa mipango ya ujenzi wa chuo kikuu mkoani Dodoma ulikuwapo tangu utawala uliopita, lakini utekelezaji na namna zilivyopatikana fedha ulitokana na uamuzi mgumu wa Lowassa.

Alifanya jitihada na kufanikiwa kupata fedha za kujenga Chuo Kikuu Dodoma (Udom).

Chuo hiki kikuu cha umma kilichopo katikati ya Tanzania kilianzishwa mwaka 2007.

Lowassa alifanya uamuzi wa kuwaita wakurugenzi wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kuwataka kuidhinisha fedha ndani ya saa 24 ili kufanikisha ujenzi wa Udom. Haikuwa kazi rahisi, lakini iliwezekana.


Kupambana na wazembe

Lowassa hakuwa kiongozi wa mchezo serikalini na alifananishwa na Sokoine aliyepambana kupiga vita uhujumu uchumi

Aliweza kuwasimamisha kazi watendaji wabovu, kwa mfano, kumsimamisha mkandarasi wa ghorofa lililoporomoka eneo la Kisutu jijini Dar es Salaam na watendaji wengine wa Serikali.