Mbunge akerwa magari ya Serikali kutokatiwa bima
Muktasari:
- Mbunge wa Vwawa (CCM) Japhet Hasunga amekerwa na hatua ya magari na majengo ya kibiashara kutokuwa na bima ya lazima na hivyo kusababisha watu kutolipwa fidia inapotokea majanga.
Dodoma. Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga ameshauri Serikali kuweka bima ya lazima katika majengo ya kibiashara na magari yake ili watu wanapopata majanga waweze kulipwa.
Hasunga ameyasema hayo leo Jumatano Juni 7, 2023 wakati wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango ya mwaka 2023/24.
Amesema yapo magari na majengo ya kibiashara ya Serikali hayana bima, na kuongeza kuwa: “Ajali nyingine nyingi zinasababishwa na magari ya Serikali, matokeo yake yanawagonga watu na mali za watu na hivyo kusababisha hasara kubwa, yule anayegongwa anatakiwa afidiwe na bima,” amesema.
Amesema kikawaida duniani kote, utaratibu unaonyesha anayegongwa ama kuharibiwa mali anatakiwa afidiwe na bima, lakini kwa utaratibu ulivyo hivi sasa; magari ya Serikali hayana bima na hivyo inakuwa vigumu kutoa fidia hizo.
Amesema maana yake ni watu wanapata hasara lakini hawana mahali pa kujitetea ili kuomba fidia hiyo kwamba jambo hilo sio zuri.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wameliona jambo hilo na kubadilisha sheria ambapo magari yote yana bima ya lazima ili watu wote wakisababishiwa hasara waweze kufidiwa.
“Sisi huku bado, nafikiri hili watu wanaumia, wanapata majanga na hakuna fidia. Juzi tumeshuhudia kwenye lifti watu wakidondoka hadi chini (jengo la PSSSF), watu wameumia katika lift lakini hawana mahali pa kuomba fidia,” amesema na kuongeza;
“Serikali ilitazame na kuona kuna haja ya kuja na mfumo wa magari yote ya kiserikali, majengo ya kibiashara yanayomilikiwa na Serikali yaweze kuwa na bima ya lazima.”