Muuguzi matatani, baada ya mama kujifungua pasipo usaidizi
Muktasari:
- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa atoa maelekezo.
Kigoma. Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imemsimamisha kazi muuguzi katika Zahanati ya Basanza, Alex Lyimo kupisha uchunguzi baada ya kuhusishwa na malalamiko ya kumuacha Prisca Makenzi kujifungua bila msaada wake akiwa zamu Juni 9, 2024.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Prisca (17) anayedaiwa kujifungua bila msaada wa mtoa huduma katika zahanati hiyo iliyopo Kijiji cha Basanza.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 15, 2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Jesca Leba amesema tayari Serikali ya mkoa imeanza uchunguzi wa tukio hilo.
Leba amesema Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetoa taarifa rasmi ya kumsimamisha kazi kwa muda mtumishi huyo baada ya kuhusishwa na malalamiko hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotelewa Juni 14, 2024 na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Fred Milanzi ufuatiliaji uliofanyika umebaini Prisca alifika Zahanati ya Basanza Juni 9, 2024 akitokea maabara binafsi iliyopo katika kijiji hicho kwa ajili ya kupata huduma zaidi.
Taarifa inaeleza kabla ya kupatiwa huduma ghafla alishikwa uchungu akatembea moja kwa moja kuelekea kwenye chumba cha kujifungulia.
Inaelezwa baada ya kupata taarifa muuguzi wa zamu (Alex) ambaye anaishi karibu na kituo (takribani mita tano), alifika wodini na kukuta mama huyo ameshajifungua mtoto wa kiume akiwa salama mwenye uzito wa kilo 2.6.
Inaelezwa katika taarifa mzazi huyo alipatiwa huduma zote muhimu za uzazi na kupumzishwa hadi Jumatatu Juni 10, 2024 mchana aliporuhusiwa kwenda nyumbani akiwa salama yeye pamoja na mtoto.
“Halmashauri imepokea kwa uzito wa kipekee na imeshachukua hatua ya kumpumzisha kutekeleza majukumu ili kupisha uchunguzi zaidi mtumishi wa zamu aliyehusishwa na malalamiko haya kuanzia Juni 15, 2024,” inaeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, endapo atabainika kuwa na kosa atachukuliwa hatua za kinidhamu kulingana na sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
“Nimesikitika na kitendo kilichofanywa na mwananchi ambaye alithubutu kuingia wodi ya wazazi bila ridhaa na kuchukua video ya tukio hilo na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii na kuleta taharuki kubwa kwa wananchi,” amesema mkurugenzi kwenye taarifa.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amewaelekeza watumishi wa afya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miiko ya taaluma zao.
Katika taarifa kwa umma iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Tamisemi, Nteghenjwa Hosseah, leo Juni 15, 2024, Mchengerwa amesema hatasita kumchukulia hatua mtumishi yeyote atakayeenda kinyume cha miiko na maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu aliyokabidhiwa.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kupitia ukurasa wake wa Instagram amelaani kitendo kilichofanywa na muuguzi huyo na kueleza kuwa ni kitendo kibaya ambacho hakipaswi kuvumiliwa.
Pia amepongeza hatua iliyochukuliwa na Tamisemi na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya kuanzia ngazi ya msingi yaani Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri, ngazi ya Kati (Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda) hadi ngazi ya Taifa.