Mwanafunzi ajeruhiwa na walimu akigomea udanganyifu kwenye mtihani

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wazazi wa wanafunzi 140 waliofutiwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022 katika Sekondari ya Thaqaafa iliyoko jijini Mwanza kuhusu mstakbari wa watoto wao. Mkenda alisema hakuna uwezekano kwa matokeo hayo kutangazwa badala yake Serikali itaangalia uwezekano wa kuwafanya warudie mitihani hiyo. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lililifuta matokeo ya mitihani ya waliomaliza mwaka 2022 kidato cha nne 337 sawa na asilimia 0.06 ya watahiniwa wote 560,335 waliofanya mitihani yao ya kumaliza elimu hiyo huku matokeo ya wanafunzi 20 yakizuiliwa ili kupisha uchunguzi.

Mwanza. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mmoja wa wanafunzi waliogoma kufanya udanganyifu katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022 katika Sekondari ya Thaqaafa iliyoko jijini Mwanza alijeruhuwa vibaya kutokana na adhabu aliyopewa na uongozi wa shule hiyo.

Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo leo Februari 19,2023 alipokuwa akizungumza na wazazi na walezi wa wanafunzi 140 waliofutiwa matokeo yao katika Sekondari ya Thaqaafa huku akisema uchunguzi wa awali umeonyesha udanganyifu huo umekuwa ukifanyika kila mwaka katika shule hizo.

Bila kutaja jina la mwanafunzi huyo, Profesa Mkenda ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kufanya ufuatiliaji wa tukio hilo na kuwachukulia hatua wahusika wote wa ukatili huo huku akiwataka wazazi kuzungumza na watoto wao wawaeleze jinsi wizi huo ulivyokuwa unafanyika.

"Katika Sekondari ya Thaqaafa kulifanyika utaratibu wa watu kuanza kupeana majibu kwenye mtihani, mwalimu anaitwa Rajul Zakaria anatuhumiwa kuwafundisha majibu ya mtihani halafu wenye shule wanasema aah..sisi tumeshamuondoa lakini kuna ushahidi unaonyesha kabisa hajaondolewa," amesema Mkenda na kuongeza,

"Wakafanya mpango kabisa kwamba sasa wanafunzi watakuwa wanatoka chumba cha mtihani wanaenda nje kuchukua majibu kama wanaenda kujisaidia wanasaidiana, wameelekezwa shuleni saidianeni kwenye kujibu mtihani,"

"Mwanafunzi mmoja akagoma, akapigwa vibaya sana na mwalimu, kwa kukataa huyu nadhani alichokuwa anasali huko kama ni msikitini au kanisani alielewa yale maadili na malezi, alikataa akapigwa sana na ushahidi upo kwamba kwa nini wakati shule yetu ni kufundisha watu wizi wa mitihani," ameongeza

Amewasisitizia wazazi kwamba matokeo ya wanafunzi hao hayatatoka kwani Serikali inaendelea kukusanya ushahidi kuhusu udanganyifu huo huku akisema anauhakika wahusika ambao wamekamatwa na wanaoendelea kusakwa watachukuliwa hatua ikiwemo kufungwa kwa wizi wa mitihani hiyo.

"Wazazi wenzangu naomba mnielewe kwamba wizi ulifanyika kwa sababu uchunguzi unaonyesha kwamba ushahidi ni zaidi ya mfanano. Ninachoweza kuwaahidi ni kwamba wizara tutajadiliana kuangalia uwezekano wa kuwafanya warudie hiyo mitihani," amesema Profesa Mkenda.

Huku akichelea kutaja tarehe ya kurudia mitihani hiyo, Profesa Mkenda amesema suala hilo ni la kisera hivyo amewataka wazazi hao kuwa wavumilivu wakati huu ambao Serikali inaendelea kusaka mwarobaini wa suala hilo.

Awali, akizungumza kwa niaba ya wazazi na walezi wa wanafunzi 140 waliofutiwa matokeo hayo katika Sekondari ya Thaqaafa jijini Mwanza, Patrick Masagati ameiomba serikali kuwasaidia waweze kurudia mitihani hiyo huku akiomba shule zilizofanya udanganyifu huo zifungiwe.

"Wazazi, wajane na walezi wa watoto hawa, tunakuomba (Waziri) na Serikali uweze kuachilia matokeo ya watoto wetu au kuwapa nafasi ya kurudia masomo yaliyosemekana walifanya udanganyifu kwa maana ya Uraia, Kiswahili na Baiolojia," amesema Masagati

Naye, Upendo Alfred amemshukuru Profesa Mkenda kwa kufika jijini Mwanza kusikiliza kilio chao huku akiahidi kwamba wako tayari kuwaandaa watoto wao kwa ajili ya kurudia mitihani hiyo.