Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanamke afukuzwa kijijini kwa tuhuma za ushirikina

Sehemu ya wananchi waliokusanyika kwenye nyumba ya mtuhumiwa wa ushirikina

Muktasari:

  • Uamuzi huo wa wananchi umekuja baada ya kumkuta mwanamke huyo kwenye nyumba ya jirani yake akiwa hajavaa nguo, jambo lililoibua hisia kwamba alikuwa akiwanga.

Songwe. Mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60, mkazi wa kitongoji cha Ipapa kilichopo kijiji Cha Isongole, wilaya ya Ileje mkoani Songwe amefukuzwa kijijini hapo na wananchi akituhumiwa kujihusisha na imani za kishirikina.

Wananchi hao wamefikia hatua hiyo baada ya kumkuta mwanamke huyo kwenye nyumba ya jirani yake akiwa hajavaa nguo, jambo lililoibua hisia kwamba alikuwa akifanya imani za kishirikina.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 12, 2024 kuhusu tukio hilo lililotokea saa nane usiku, baadhi ya wananchi wamesema mwanamke huyo amekuwa akituhumiwa kwa imani za kishirikina kwa kuwaroga majirani na kuharibu vitu vyao kishirikina kama vile mazao na mifugo.

Mkazi wa kitongoji hicho ambaye ameshuhudia tukio hilo, Mainesi Mwambene amesema wamemkuta mwanamke huyo bila nguo akiwa mlangoni kwenye nyumba ya jirani yake (jina limehifadhiwa), jambo lililozua taharuki kwa majirani waliokusanyika kumshuhudia mwanamke huyo.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukimhisi huyu mwanamke kama mchawi, lakini leo Mungu katuonyesha na tumefikia makubaliano ya kutomtaka kwenye kitongoji chetu, aende anakokujua yeye, sisi hatutaki matukio ya ushirikina,” amesema Mwambene.

Kwa upande wake, Wilson Mtafya amesema hawamtaki mama huyo, kwani amekuwa akifanya matukio mengi ya ushirikina wakamvumilia hadi wakachoka lakini leo yamemkuta, kila mtu kashuhudia akiwa bila nguo.

“Licha ya kwamba Serikali haiamini ushirikina, lakini wananchi wake tunaamini kama ambavyo mnashuhudia wananchi wameamua kutoa vyombo nje kwa ishara kwamba hatumtaki, kama Serikali haiamini iende kuishi naye,” amesema Mtafya.

Akizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutoandikwa jina lake, mmiliki wa nyumba hiyo amekiri kumkuta mama huyo akiwa bila nguo kwenye mlango wake na kwamba aliyekwenda kumtoa ni chifu aliyefika saa 11 alfajiri kushuhudia tukio na kumtaka mama huyo aondoke kwenye kitongoji hicho.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Nelbati Kasekwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amewapongeza wananchi kwa kutojichukulia sheria mkononi, hivyo mtuhumiwa yuko salama chini ya ulinzi wa balozi wa eneo husika.

Baada ya Jeshi la Polisi, kituo cha Itumba kupata taarifa hizo, limefika eneo la tukio na kumchukua mtuhumiwa kwenda naye kituo cha polisi kwa usalama zaidi.