Asimulia anavyoishi kama mkimbizi kwa tuhuma za uchawi

Limbu Rububu akiwa na mwanawe anayetembea naye kila mahari baada ya mke wake kufariki dunia.
Muktasari:
- Kutokana na kuendekeza tuhuma za uchawi, kumemfanya Limbu kuishi maisha ya ukimbizi.
Serengeti. Walioko magerezani si kwamba wote walitenda makosa,lakini pia wanauawa kwa sura za kishirikina si kwamba wote ni wachawi, bali watu hutenda unyama huo kwa kutimiza matakwa yao
Mauaji hayo yanaendeshwa na makundi ya watu kwa madai mbalimbali, ikiwamo wivu wa maendeleo,migogoro ya ardhi na ramli zinazopigwa na waganga wa kienyeji, mara nyingi huvikwa sura ya imani za kishirikina.
Lembu Rububu (56) mkazi wa kitongoji cha Nyigoti kijiji cha Nyichoka kata ya Kyambahi wilayani Serengeti,alikutwa na mkasa huo akidaiwa ni mchawi, tuhuma ambazo kama asingetafuta msaada angeweza kujikuta yeye ama familia yake wamekufa kama ilivyo kwa wengi waliokutwa na matukio hayo. Anasema Januari 14, familia yake ilijawa na furaha kubwa kutokana na mke wake kujifungua mtoto wa kike,akiwa ni mtoto wa saba
kwa mke wake Njile Mabula(34),hata hivyo furaha haikudumu kwa kuwa kesho yake mama huyo aliyejifungulia nyumbani alifariki dunia muda mfupi baada ya kumfikisha Hospitali Teule ya wilaya ya Nyerere,kutokana na kuvuja damu nyingi.
Januari 16,kwa heshima zote mazishi yakafanyika nyumbani kwake,eneo maarufu la uchimbaji madini ya dhahabu na chokaa,ambako imani za kishirikina zimeshamiri kwa maana kila mafanikio ya kupata mali lazima kuwe na mkono wa mtu.
Rububu akiwa na mdogo wake Nzungu Lububu(30) anasema baada ya mazishi ya mke wake walizushiwa tuhuma za ushirikina kuwa aliosha maiti ya mke wake,na mdogo wake akidaiwa kukata sehemu za siri na ulimi wa marehemukwa ajili ya imani za kishirikina.
Akizungumzia tuhuma hizo anadai hazina ukweli wowote kwa kuwa walioosha mwili wa marehemu ni yeye, watoto wake wakiongozwa na Kwimba Rembu (12) na wadogo zake.
Ukikutana na Lububu lazima utalazimika kusimama na kujiuliza maswali kutokana na jinsi ambavyo anazunguka na mtoto wake mdogo akiwa amebeba chupa ya kunyonyeshea, lakini kwenye mfuko anakuwa na chupa ndogo ya maziwa.
Kutokana na hali hiyo majirani zake Mbigo Igogo na Lubugwe Nyanda walitoa ng’ombe watatu ili kumwezesha kupata maziwa ili kunusuru maisha ya mtoto huyo, licha ya kulelewa na baba yake anazidi kuongezeka kwa kimo na uzito kutoka kilo mbili wakati anazaliwa sasa ni zaidi ya kilo nne.
Anavyoishi sasa
Kutokana na nguvu ya watendaji wa serikali kuanzia kitongoji chake, yeye na mdogo wake wako kwenye makazi yao, wakiwa ni watu waliojawa hofu licha ya kubainika kuwa tuhuma zao zilikosa uthibitisho, lakini wanaishi kama wakimbizi kwa kuwa hawana uhuru, wakijua lolote laweza kuwatokea.
“Dhamira yangu bado ni kwenda mahakamani kutafuta haki stahiki…maana hadi watoto wanajua sisi ni wachawi…watoto wangu wanaitwa wachawi…shuleni wenzao wanawanyanyapaa….kumbe mauaji yote yanayoendelea kwa kivuli cha uchawi ni ya kutungwa …nyuma yake kuna agenda,” anasema kwa masikitiko.
Mdogo wake ajitetea
Nzungu Rububu (30)anadai tuhuma hizo ni za kuzusha kwa kuwa hajawahi kufanya vitendo kama hivyo,nakuomba kama kuna mtu ana uthibitisho wa tuhuma wako tayari maiti ifukuliwe ili waone kama viungo hivyo vimekatwa.
“Wananituhumu bure tu....lakini msingi wa tuhuma zao kwangu ni kuwa nimeingia kijijini hapa bila kibali...mimi nilikuja kwa kaka yangu, baadaye nikajenga nyumba pembeni na kuishi na familia yangu akiwemo mama, hili la uchawi kuna visa wananitafuta,” anajitetea.
Nzungu mdogo wake anayetuhumiwa kufanya ngono na wake za watu kishirikina anasema, hana amani kwa kuwa watu wamefikia hatua ya kudai kuwa akiangalia mazao yao hawavuni, hivyo anaamini kwa jinsi ilivyo iko siku wanaweza kuwafanyia mambo mabaya.
Mwenyekiti wa kitongoji ashangaa
Kiroyo Edward ni Mwenyekiti wa kitongoji hicho anasema, alikuwapo wakati wa mazishi hapakuwa na tuhuma wala madai yoyote juu ya watuhumiwa,hivyo uamuzi wa Mwenyekiti wa Ritongo kutoa hukumu kama hiyo kwa madai kama hayo si sahihi.
Aitwa na wazee wa mila(Ritongo)
Januari 30 yeye na mdogo wake waliitwa na wazee wa mila maarufu kama Ritongo ili kuthibitisha tuhuma hizo, lakini hakufika kwa kuwa alimpeleka mtoto kliniki,hata hivyo wazee hao walifikia uamuzi wa kuwatenga wasifike kwa mtu,wala kutembelewa na hata dukani wasipewe huduma, hatua iliyosababisha watoto wake kushindwa kwenda shule.
Akiwa hana taarifa za maamuzi hayo,usiku akiwa na familia yake alisikia yowe inapigwa nje ya nyumba yake ikiambatana na maneno,
“toka leo Rembu na mdogo wako tumewafungia kwa sababu ni wachawi
....hakuna kwenda kwa mtu wala kutembelewa mpaka walipe faini,”anasema kwa masikitiko.
Alilazimika kwenda kwa Mwenyekiti wa kitongoji na baadaye polisi ambao walimwambia suala hilo ni la mila hawahusiki, aliamua kutafuta msaada wa kisheria kumnusuru na adhabu iliyotishia uhai wajumla ya watu 29 ikiwa ni familia yake na ya mdogo wake.
Mzee wa Kisukuma aliyejitambulisha kwa jina moja la Masanja mkazi wa Magu, anasema kwa mila za kabila hilo maiti ya mwanamme huoshwa na wanaume,wakiwa ndugu ama watoto na kwa wanawake hivyo hivyo,mume haruhusiwi kuosha maiti hiyo na inapotokea,hupigwa faini mbuzi mmoja ama wawili na huchinjwa lakini si kutengwa.
Paulo Bhoche mkazi wa kijiji cha Burunga wilayani Serengeti anasema kwa mila na desturi za makabila hayo,mwanaume haruhusiwi kuosha maiti ya mke wake,vivyo hivyo hivyo mwanamke,na akitokea adhabu hutolewa kwa mhusika na wanawake wanadai kuwa kazi hiyo wangeifanya wao si yeye kuosha maiti ya mke wake.
Tuhuma zingine dhidi Nzungu Rububu, ni kwamba tangu ameingia kijijini hapo kumekuwapo na mchezo wa kuwatoa wanaume kitandani na kuwalaza chini, kisha kufanya ngono na wake zao kwa njia za kishirikina,tuhuma ambazo hazikuthibitishwa.
Kwa mujibu wa taarifa pia walimuhusisha Nzugu na matukio ya wizi wa mahindi na upoteaji wa kukuyamekithiri na kuwa utafiti wao ulibaini kuwa ndiye anahusika namatukio hayo.
Watetezi wa Haki za Binadamu
Mwenyekiti wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria na Haki za Binadamu
(WASHEABISE)wilayani Serengeti, Samwel Mewama kwa masikitiko anasema, hayo ni matokeo ya viongozi wa serikali kutumia vyombo visivyo vyakisheria kuhukumu watu.
“Ibara ya (3),Haki za raia,wajibu na Maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamriwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu washeria,”anabainisha Mewama.
Mwantumu Mussa ni Mwanasheria wa kujitegemea anasema Sheria ya Uchawi Na.9 ya mwaka 1928 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inabainishakuwa uchawi ni kosa la jinai,na anayethibitika kutenda kosa la uchawi anatakiwa kufikishwa mahakamani.
Kutokana na matukio ya kutuhumu watu kwa uchawi kwa ulemavu, macho mekundu,vikongwe,kifungu cha 3 cha sheria ya uchawi ya mwaka 1928,imebainisha makosa ya uchawi ikiwa ni pamoja na mtu kutamka mwenyewe ama vitendo vya nguvu ya kichawi,kumiliki vifaa vya uchawi,kutishia kuua kwa matumizi ya uchawi,au kumiliki vifaa vyauchawi.
“Sheria hii inategemea sheria yaa Ushahidi No.6 ya Tanzania ya mwaka 1967...hii inamtaka mpeleka shauri kutoa vielelezo kwa kile kinacholalamikiwa na kuthibitisha kosa bila kuacha shaka...lakini
kujichukulia sheria mkononi kwa kuwahukumu watu nje ya sheria nikutenda kosa la jinai,”anafafanua.