Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usijidanganye, jela miaka saba inakuhusu ikithibitika unajihusisha na uchawi

Kamanda wa  Polisi Wilaya ya Ludewa, Deogratius Massawe akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kilima Hewa wilayani humo mkoani Njombe. Picha na Seif Jumanne

Muktasari:

  • Sheria ya Kudhibiti Uchawi inampa mamlaka mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa au Rais kumpeleka uhamishoni mtuhumiwa wa uchawi atakayethibitika.

Njombe. Wananchi wanaofanya vitendo vya uchawi na ushirikina wakidhani hawawezi kuchukuliwa hatua kwa kuamini kuwa Serikali haitambui uchawi wanajidanganya, imeelezwa Sheria ya Uchawi ipo na inafanya kazi.

Kauli hiyo imetolewa jana Januari 13, 2024 na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ludewa, Deogratius Massawe, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kilimahewa wilayani Ludewa, mkoani Njombe.

Amesema kuna mambo mengi yanajitokeza wilayani humo yanayoashiria kuwa kuna mambo ya uchawi au ushirikina unaendelea.

Massawe amesema si kwamba Serikali inaamini uchawi, bali inatambua kuna uchawi, ndiyo sababu kuna sheria imetungwa ya kukataza mambo hayo.

Amesema mtu yeyote anayetuhumiwa au kusadikika kuwa anafanya vitendo vya kishirikina vinavyoonekana, endapo atapelekwa mahakamani na ushahidi kutolewa anaweza kufungwa.

"Kwa hapa Ludewa watu wengi hatutambui, tunakutana na mambo kama haya tunatishiwa na tunawafahamu watu wanaotufuata tukanunue uchawi kwa ajili ya kuwadhuru watu wengine lakini hatusemi," amesema Massawe.

Amesema wananchi wa Kilimahewa na Ludewa kwa ujumla watoe taarifa polisi endapo watakutana na mambo yanayoashiria uchawi na ushirikina ili mhusika afunguliwe kesi na kufikishwa mahakamani.

Massawe amesema wanaotuhumiwa kuwa wachawi, sheria inampa mamlaka mkuu wa wilaya kumhamisha mtu kama huyo na kumpeleka kuishi sehemu nyingine.

Diwani wa Kata ya Ludewa, Monica Mchiro ameitaka jamii kuacha mambo ya kishirikina akisema hayana faida yoyote kwao na jamii kwa ujumla.

Amesema watu watakufa endapo Mungu ataamua iwe hivyo na siku ikifika, si kwa sababu mtu mwingine ameamua kukatisha maisha yao.

"Haiwezekani ushindane na jamii na usiombe jamii ikakutenga, utapata shida. Mtu mpaka anakutishia kunakuwa na chanzo," amesema Mchiro.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ludewa Mjini, Winfred Mwalongo amesema wananchi wa kitongoji cha Kilimahewa wanalalamika kuhusu mambo ya kishirikina, akidai kuna watu wanagongwa mihuri inayoashiria kuwa ni ushirikina wa kutaka kutoa roho za watu.

"Tumefuatilia ni kitu ambacho hakipo, ni maneno tu ya watu kijiji hiki kina amani ya kutosha," amesema Mwalongo.

Elius Kayombo, mkazi wa kitongoji cha Kilimahewa amesema wapo baadhi ya watu aliowaita wasamaria wema walimfuata na kumwambia amegongwa muhuri na alitakiwa kufa mwaka mpya.

"Mimi sikuona, ila wazee walioona walisema nimegongwa muhuri na muhuri wenyewe mimi siujui, nashukuru Mungu kwa maombi ya wachungaji muhuri huo umetoka na sasa najihisi nipo vizuri," amesema Kayombo.

Mmoja ya wazee ambao wanatuhumiwa kugonga wananchi mihuri inayodaiwa kuwa ya kichawi kwenye kitongoji hicho, Melkion Haule amesema suala hilo halipo bali tuhuma hizo zimelenga kumfedhehesha.

"Muhuri hakuna, wananinyooshea kidole tu wameona huo muhuri nimechukua kwa nani, na nani umemgonga," amehoji Haule.

Sheria ya uchawi

Sheria ya Uchawi Sura ya 18 ya Sheria za Tanzania zilizofanyiwa mapitio mwaka 2002 kifungu cha 3 kinatamka kuwa mtu yeyote ambaye kwa kauli au matendo yake akibainika kuwa na nguvu za kichawi, au anamiliki zana za kichawi au anasambaza zana hizo, au anashauri watu kutumia uchawi au kutishia kutumia uchawi dhidi ya mtu yeyote au vitu, atakuwa ametenda kosa la jinai.

Kifungu cha 5 (1) (a) cha sheria hiyo pia kinatamka kuwa mtu yeyote anayetenda kosa la uchawi kwa lengo la kusababisha kifo, ugonjwa, majeraha au madhila kwa jamii yeyote au mnyama anastahili kifungo kisichopungua miaka saba akitiwa hatiani.

Sheria ya Uchawi ilitungwa wakati wa utawala wa wakoloni baada ya kukuta jamii nyingi za Kiafrika zinaamini nguvu ya uchawi hata katika kupambana nao.

Sheria ya Kudhibiti Uchawi inampa mamlaka mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa au Rais kumpeleka uhamishoni mtuhumiwa wa uchawi atakayethibitika.

Kuna haja ya kuitazama upya sheria hii, iwapo haikidhi matakwa ya kudhiti matukio haya yenye imani za kishirikina, basi ifutwe na uwekwe utaratibu mwingine wa namna ya kuyashughulikia.

Kwa hali ilivyo, kuthibitisha uchawi kisheria ni vigumu, ndiyo maana Sheria ya Uchawi ni moja kati ya 40 ambazo Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali iliiainisha kuwa kandamizi na kupendekeza ifutwe.

Kwa msingi huu, ni wazi suala la uchawi linapaswa kushughulikiwa zaidi kwa wananchi kubadili mtazamo wa kifikra.