Mzee ahukumiwa miaka 20 jela kwa kukutwa na heroine

What you need to know:

  • Rayford anadaiwa kukamatwa Julai 5, 2018 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) akiwa na dawa hizo alizokuwa amezificha katika moja ya mabegi yake.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa maarufu kama Mahakama ya Ufisadi, imehukumu raia wa Marekani, Lione Lionel Rayford (70) kifungo cha miaka 20 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya, aina ya Heroine zenye uzito kilo 2.188.

Pamoja na hukumu hiyo, mahakama imetoa amri ya kuteketezwa dawa hizo na Hati ya kusafiria ya mshtakiwa huyo ikabidhiwe Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya taratibu nyingine.

Pia, imeamuru vitu vya mshtakiwa ambavyo ni nguo za kimasai pamoja na pesa ambazo upande wa mashtaka hawakupeleka ushahidi kuonyesha kama zilihusika kutenda uhalifu, arudishiwe mtuhumiwa.

Hukumu hiyo imetolewa  jana Mei 26 2023 na Jaji Godfrey Isaya, baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi 15 na vielelezo kadhaa vilivyotolewa na upande wa mashtaka huku upande wa utetezi ukiwasilisha mashahidi wawili akiwemo mshtakiwa mwenyewe.

Jaji Issaya alisema mshtakiwa ambaye ni mkazi wa Jimbo la Michigan nchini humo, ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa na hivyo anatakiwa kutumika kifungo cha miaka 20 gerezani.

“Mahakama imezingatia maoni ya upande wa mashtaka kuhusu athari za dawa za kilevya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimataifa. Imezingatia pia kiasi kikubwa cha dawa ambacho mshtakiwa amekutwa nacho na kwamba madhara yake ni makubwa kwa sehemu kubwa kwa jamii. Mahakama imezingatia pia mtuhumiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na umri mkubwa,” amesema jaji Isaya na kuongeza.

“Katika kuzingatia maoni ya pande zote mbili Mahakama hii inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine,” amesem jaji Isaya.

Awali, jopo la Mawakili watatu wa Serikali, Clara Charwe, Erick Shija na Moses Mafuru waliwasirisha hoja nane mahakamani hapo wakiomba itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa.

Katika hoja hizo, Wakili Mafuru alidai kiasi cha dawa alichokutwa nacho mshtakiwa kilikuwa ni kikubwa hivyo kilikuwa kinakwenda kuharibu na kuathiri sehemu kubwa ya jamii.

“Madhara ya dawa za kulevya kama yalivyo elezwa katika taarifa ya Mkemia yanasababisha ulevi usio ponyeka, yana sababisha kuharibikiwa na akili na ni dawa ambazo zipo kwenye kundi la sumu, hivyo athari zake ni mbaya na zenye madhara makubwa kwenye afya ya binadamu,” amedai wakili Mafuru.

Hoja ya tatu, Mafuru alidai matumizi ya dawa hizo yanaongeza uhalifu kwa maana ya kuongeza vibaka, wezi na hata wauaji.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa dawa za kulevya zinaharibu akili ya vijana ambao ni nguvu kazi katika ukuaji wa uchumi, hivyo kwa maana nyingine zinaharibu uchumi na ukuaji wa uchumi katika jamii.

Hoja ya tano, walidai kuwa dawa hizo huharibu akili ya vijana ambao ndo sehemu kubwa ya jamii, zinahafifisha na kudidimiza maendeleo ya jamii kwa sababu vijana wanakuwa hawana akili timamu za kufanya kazi na wanakuwa tegemezi, hivyo maendeleo kuhafifishwa na kudidimizwa.

Wakili Mafuru aliendelea kudai kuwa dawa hizo huharibu akili ya vijana na zinaathiri uwezo wa kufanya maamuzi kuanzia ngazi ya familia, katika ngazi ya uaandaaji wa sera na mipango ya maendeleo wa jamii na katika inchi.

Hoja ya saba, Wakili Mafuru alidai kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizotia saini mikataba ya kimataifa ya kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya hivyo mtuhumiwa kusafirisha dawa hizo ndani ya nchi ya Tanzania inaharibu taswira ya inchi katika masuala ya ushirikiano wa nchi kimataifa na diplomasia.

“Dawa za kulevya hazikubaliki na kifungu cha 60 (2) cha sheria ya uhujumu uchumi kimetoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 lakini pia kimeeleza kama sheria nyingine itatoa adhabu zaidi ya hiyo basi adhabu hiyo ndio itolewe, katika kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia dawa za kulevya imeelekeza adhabu ya kifungo cha maisha, hivyo ni rai yetu mtuhumiwa apewe adhabu kubwa kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya,’’ amedai Wakili Mafuru wakati akihitimisha hoja upande wa mashtaka.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa mshtakiwa huyo kujitetea kwanini asipewe adhabu kali.

Rayford kupitia wakili wake, Omari Kilwanda, alidai upande wa mashtaka hauna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mteja wake na kwamba Rayford ni mkosaji wa mara ya kwanza na sheria inaelekeza apewe adhabu ndogo.

Wakili Kilwanda alidai kuwa Rayford ana mke na watoto wanaomtegemea hivyo ni busara kupewa adhabu ndogo ili awe na nafasi ya kuendelea kuhudumia familia inayomtegemea.

“Mtuhumiwa ana umri wa miaka 70, hivyo kwa umri wake anastahili kupewa adhabu ndogo hasa ukizingatia umri wake unanyemelewa na maradhi mbalimbali,’ alidai wakili Kilwanda.

Hata hivyo Jaji Isaya alitupilia mbali maombi ya mshtakiwa na kukubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kisha kumhukumu mshtakiwa huyo kwenda Jela miaka 20.

Katika kesi ya msingi, Rayford anadaiwa alikuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 17/2021 ambapo anadaiwa kukamatwa Julai 5, 2018 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) akiwa na kilo 2.188 za dawa za kulevya aina ya Heroine, alizokuwa amezificha katika moja ya mabegi aliyokuwa nayo.