Operesheni ya tozo ya huduma yaibua mapya Arusha

Muktasari:

  • Operesheni ya ukusanyaji madeni ya tozo ya huduma imeleta sintofahamu kwa wafanyabiashara Arusha, wakilalamikia makadirio ya kiwango cha malipo na mianya ya  rushwa. Mkurugenzi wa Jiji asisitiza umuhimu wa kulipa kodi, akisema wanadai zaidi ya Sh8.7 bilioni.

Arusha. Operesheni maalumu ya ukusanyaji madeni ya tozo ya huduma inayoendeshwa na Jiji la Arusha imeibua sintofahamu baada ya wafanyabiashara kudai hawatendiwi haki.

Wamesema jambo la wanalofanyiwa la kupigiwa hesabu za miaka hata mitano au sita nyuma ni kinyume kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Juni 9, 2022 akiwa mjini Bukoba mkoani Kagera.

“Suala la watu kupewa bili za nyuma za kodi walipe leo, miaka yote hiyo watoza kodi wapo, kama ni halmashauri zipo, mmeachia watu hawakulipa leo hii unampelekea mtu bili ya miaka mitano, sita alipe leo, wakati ule mlikuwa wapi?”

Hata hivyo, alisema wanaloweza kufanya ni kurudi tu mwaka mmoja nyuma kwa sababu inawezekana labda mwaka jana hawakumaliza kufanya mahesabu.


Malia madeni ya nyuma

Akizungumza na Mwananchi jana, mmoja wa wafanyabiashara hao, Peter Moshi wa maduka ya Stendi ndogo jijini hapa, alisema wamekuwa wakitembelewa na maofisa wa jiji la kufanya makadirio ya tozo huku wakiwalimbikizia na madeni ya nyuma na kuwapiga faini.

“Raisi akiwa Bukoba alisema tusamehewe ushuru na tozo za nyuma ili kuwasaidia wafanyabiashara twende sambambamba, lakini sasa hivi wanatuletea madeni yasiyolipika, kwani wanakuja kufukua makaburi ya madeni ya miaka sita hadi minane iliyopita, kiukweli huu ni uonevu” alisema.

Kadhia hiyo pia imeikumba kampuni moja ya raia wa China inayosambaza pembejeo za kilimo ambayo mmoja wa maofisa wake (hakutaka kutajwa jina), alidai ofisa mwenzao alikamatwa na kushikiliwa na maofisa wa halmashauri ya jiji kwa sababu hiyo.

“Mwaka jana, maofisa wa Halmashauri ya jiji walikuja na kudai tunadaiwa service levy zaidi ya Sh40 milioni. Tukawaambia kwanza tuhakiki, kwa kuwa hesabu hiyo si sahihi.

“Wiki mbili zilizopita wakaja kumkamata ofisa wetu wakaondokana naye, hadi mwanasheria wetu alipoingilia.

“Si kwamba hatukutaka kulipa, ilikuwa ni lazima tuhakiki na tulipohakiki tukakuta deni ni zaidi ya Sh30 milioni, sio Sh40milioni walizokuwa wakidai,” alisema.

Naye Neema Maro alisema kuwa amekuwa na utaratibu wa kulipa kidogo kidogo lakini siku za hivi karibuni biashara yake iliyumba na kushindwa kulipa kwa wakati, anashangaa kuletewa faini kubwa iliyotozwa isiyolingana na tozo yake.

 “Hatukatai kulipa, tatizo miezi hii biashara ilikuwa mbaya kidogo tukalimbikiza, shida ni kwamba wanaleta deni kubwa na wanatoa muda mfupi wa kulipa. Kwa mfano mimi nadaiwa Sh3.27 milioni napewa wiki mbili niwe nimelipa, nawezaje wakati nategemea biashara hii hii moja ya kuuza majokofu,” alisema.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Adolf Loken alidai kuwa makadirio hayo yamekuwa na harufu ya rushwa kutokana na kutokuwa na kiwango kimoja cha utozaji.

“Kwa sisi Arusha tunaomba Serikali ituwekee kiwango cha ulipaji kulingana na eneo la biashara zetu, kwa mfano iseme kwa sababu Chekereni, Moshono, Kijenge, Sinoni na Ngaramtoni biashara sio kubwa wahusika walipe labda Sh30, 000 na kuja Mjini kati, Mianzini, Sanawari na Mrombo walipe Sh50, 000 na wa mjini kati masokoni na Stendi walipe Sh100, 000 au vyovyote itakavyoweza hadi wafikie wa Sh300,000 lakini mtu ajue kiwango,” alisema.

“Hii ya kukadiria kila mtu alipe kiwango chake, imegubikwa na harufu ya rushwa na inainyima Serikali mapato halisi kwa sababu wako wanaokuja madukani kwetu wanatukadiria kulipa Sh300, 000, akitaka mazungumzo ya pembeni umpe kitu kidogo ili akupunguzie makadirio mnaanzia hapo uhalifu wa rushwa.”


Mkurugenzi wa Jiji aeleza

Akizungumzia jana na Mwananchi kuhusu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini alisema wako katika operesheni ya ukusanyaji madeni ya tozo ya huduma ambayo ni asilimia 0.3 ya jumla ya mauzo.

Amesema wameamua kuanza operesheni hiyo kwa ajili ya kufikia malengo yao ya makusanyo na pia kuwakumbusha wafanyabiashara wajibu wao wa kulipa kodi za Serikali kwa maendeleo ya Taifa.

“Wafanyabiashara hivi karibuni wamesahau wajibu wao wa kulipa tozo hizi ambazo kwa sasa tunawadai zaidi ya Sh8.7 bilioni, hivyo tumeamua kupita duka kwa duka na kibanda kwa kibanda, kwanza kuwakumbusha wajibu wao na kuwapa kiasi cha fedha wanachodaiwa,” alisema.

Awali, mmoja wa wajumbe wa Kamati maalum ya kukusanya maoni kwa ajili ya kutatua mgogoro baina ya Serikali na wafanyabiashara iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Hamis Livembe alisema kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe 14 ilipendekeza tozo hii iondolewe kabisa.

“Tulipeleka mapendekezo 25, na moja ni hii ya kuondolewa kwa tozo ya huduma ambayo inatozwa kiasi cha asilimia 0.3 ya mauzo lakini ikabainika ziko halmashauri za majiji zitaathirika kwani hiyo ndio chanzo kikuu cha mapato, hivyo tukakubaliana hadi June 2024 ipunguzwe hadi ifikie 0.1 ya mauzo” alisema Livembe ambae pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Taifa.

Alisema kuwa Serikali kila mwaka inakusanya zaidi ya Sh129 bilioni kutokana na tozo hii ya huduma, hivyo inakuwa vigumu kuifuta.

Alisema kwa jiji la Arusha zaidi ya Sh17 bilioni zinakusanywa kila mwaka kutokana na tozo hiyo.