Patachimbika leo Kamati Kuu ikiwahoji kina Mdee

Patachimbika leo Kamati Kuu ikiwahoji kina Mdee

Muktasari:

Leo patachimbika wakati wabunge 19 wa Chadema walioapishwa Novemba 24 itajulikana leo baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kukaa na kuwahoji kuhusu madai ya kukiuka msimamo wa chama.


Dar es Salaam. Leo patachimbika wakati wabunge 19 wa Chadema walioapishwa Novemba 24 itajulikana leo baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kukaa na kuwahoji kuhusu madai ya kukiuka msimamo wa chama.

Juzi, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alitangaza kuwa kamati kuu ya chama hicho itakutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwahoji wabunge hao wa viti maalumu, pia, aliwataka wabunge hao kuhudhuria kikao hicho.

Mnyika alisisitiza kwamba Kamati Kuu ya Chadema ambayo ndiyo ina mamlaka kikatiba ya kupendekeza wabunge wa viti maalumu, haijakutana kufanya hivyo wala kutuma majina kwa Tume kwa Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa uteuzi.

Kufuatia wito wa wabunge hao, Gazeti hili jana liliwatafuta baadhi yao ili kujua kama wataitikia wito huo wa Mnyika, ambao baadhi yao walikuwa na kigugumizi kuzungumzia suala hilo na mkanganyiko uliojitokeza katika uteuzi wao.

Tangu kuapishwa kwao kumekuwa na sintofahamu kuhusu suala hilo, hasa baada ya viongozi wa Chadema kuweka msimamo wa kutoteua viti maalumu kutokana na kutoyatambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28.

Baada ya uchaguzi, Chadema pekee ndicho chama cha upinzani kilichokidhi vigezo vya kupata wabunge wa viti maalumu baada ya kufikia asilimia tano ya jumla ya kura za wabunge.

Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kushangazwa na hatua ya kuapishwa kwa makada wake kuwa wabunge wa viti maalumu bila baraka zake.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema baada ya kuwaapisha wabunge hao, kwamba Novemba 20 alipokea orodha ya majina hayo kutoka NEC ma kuwahakikishia ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake baada ya kuapishwa, Halima Mdee, mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), alikishukuru chama chake chini ya mwenyekiti Freeman Mbowe kwa kuwapa fursa hiyo.


Nitakwenda kuhojiwa

Wakati wabunge wengi walioapishwa wakipata kigugumizi kuzungumzia wito wa kamati kuu, Naghenjwa Kaboyoka pekee alisema ataitikia wito kwa sababu ameitwa na chama chake.

Alikiri kwamba tayari amepokea barua ya kiongozi huyo na leo atakwenda kuwasikiliza.

Kuhusu sintofahamu katika uteuzi wao, Kaboyoka alisema “mambo yote yatawekwa wazi siku hiyo, tutajua nani ni mkweli.”

Mbunge huyo ambaye katika bunge la 11 alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema alikwenda kula kiapo baada ya kupigiwa simu na maofisa wa Bunge wakimtaarifu kwamba aliteuliwa kuwa mbunge wa viti maalumu.

“Sikuona ajabu kuitwa kwenda kuapa kwa sababu niliitwa hivyo pia mwaka 2015,” alisema Kaboyoka ambaye katika Bunge lililopita alikuwa mbunge wa Jimbo la Same Mashariki.

Alipoulizwa Mdee ili kupata msimamo wake, alijibu kwa ufupi “nikuhakikishie tu sijasaliti na siwezi saliti chama… Wakati mwafaka nitasema, niko imara mno.”

Naye Hawa Mwaifunga, makamu mwenyekiti wa Bawacha Bara, alidai hadi jana hakuwa amepata barua ya kuitwa na kamati kuu kwa ajili ya mahojiano yaliyopangwa kufanyika leo.

Kwa upande wake Nusrat Hanje, katibu wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) alisema “kaka sorry, sio right time (samahani kama, sio muda sahihi), tuzungumze wakati mwingine.”

Wakati Hanje akisema hayo, Grace Tendega, katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), alisema bado anatafakari kama ataitikia wito wa Katibu Mkuu.

Kwa upande wao, Tunza Malapo na Jesca Kishoa ambao walikuwa wabunge wa viti maalumu katika Bunge lililopita, hawakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kwa sasa.

“Msemaji ni mmoja tu kwenye hili,” alisema Kishoa bila kumtaja msemaji huyo kisha akakata simu.


Ni usaliti

Wakati hayo yakiendelea, mabaraza ya chama hicho kutoka sehemu mbalimbali yametoa matamko kupinga kitendo kilichofanywa na wabunge hao wakikiita ni usaliti kwa chama chao.

Baraza la vijana Chadema (Bavicha) wamejitosa kwenye sakata hilo na kuunga mkono msimamo wa chama hicho juu ya wananchama hao waliokwenda kuapa kinyume na muongozo wa chama hicho.

Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu akitoa msimamo wa baraza hilo, alisema anaunga mkono uamuzi wa watu hao kuitwa ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.

“Tunaunga mkono kwa sababu kamati kuu ya chama ambayo mwakilishi wa vijana yumo hatukuwahi kujadili na kupitisha orodha ya viti maalumu,” alisema Pambalu.

Mbali na hilo, Pambalu alisema kamati ya utendaji ya baraza hilo lililoketi juzi limeishauri kamati kuu kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya wanachama hao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema mkoa wa Arusha, Nuru Ndossi, baraza hilo linapinga kuapishwa kwa wanachama wao 19 ambao baadhi yao ni viongozi wa Bawacha Taifa.

Pia, Bawacha mkoa wa Kilimanjaro kupitia taarifa ya mwenyekiti wake, Grace Kiwelu, imelaani kitendo cha kuapishwa kwa wabunge hao kinyume cha kanuni, taratibu na miongozo ya chama chao na sheria za nchi.

Akizungumza katika ofisi ya Kanda ya Kati ya Chadema jijini Dodoma, mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Ruvuma, Khadija Maula alisema wanakilaani kitendo kilichofanywa na Mdee akiwa na wenzake waliokwenda kula kiapo Bungeni.

Taarifa nyingine zilitoka kwa Bawacha katika mikoa ya Mbeya, Manyara, Tabora, Temeke, Mara, Katavi, na Mwanza, zote zikilaani kile walichoita usaliti wa wabunge wa viti maalumu kutoka katika chama hicho.

Taarifa hizo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na mambo mengine zimelaani kile wanachoita kughushi fomu za uteuzi wa wabunge wa viti maalumu ili kuhalalisha kwamba uteuzi huo ni halali.