Polisi Dar yathibitisha kumshikilia Dk Slaa
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limethibitisha kumshikilia Dk Willibroad Slaa.
Dar es Salaam. Saa chache baada ya kutolewa taarifa ya kukamatwa kwa mwanasiasa mkongwe, Dk Willibrod Slaa, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kumshikilia kwa mahojiano.
Taarifa ya kukamatwa kwa Dk Slaa imesambaa kupitia mitandao ya kijamii, ikisikika sauti ya mwanasiasa huyo akizungumza kuhusu kukamatwa na Jeshi la Polisi akieleza anapelekwa kituo cha Mbweni, Dar es Salaam.
“Nawajulisha tu kwamba kuna polisi wamenifuata, nitawajulisha kitakachotokea. Napelekwa Mbweni kituoni,” alisikika Dk Slaa katika sauti inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Taarifa zinaeleza Dk Slaa alikamatwa mapema asubuhi alipokuwa anafanya mazoezi eneo la karibu na nyumbani kwake, Mbweni.
Alipozungumza na Kituo cha Redio cha Wasafi FM leo Januari 10, 2025 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amethibitisha kukamatwa na kushikiliwa Dk Slaa kwa mahojiano.
“Ni sahihi daktari yupo, tuko naye na tumekuwa na mahojiano naye kwa baadhi ya mambo na mahojiano yetu yanakwenda vizuri kwa hiyo tunaangalia mifumo ya kisheria inatuelekeza nini cha kufanya naamini taarifa zaidi zitatolewa baadaye,” amesema.
Dk Slaa aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mbunge wa Karatu na pia Balozi wa Tanzania nchini Sweden.