Profesa Mkenda aapa kutotoa vibali vya kuagiza sukari

Monday August 30 2021
sukari pc
By Noor Shija

Dodoma. Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema yuko tayari kuachia ngazi nafasi ya uwaziri kuliko kutoa kibali kwa wafanyabiashara cha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi.


Profesa Mkenda amesema hayo leo Agosti 30 jijini Dodoma wakati akizindua ripoti ya sensa ya kilimo, mifugo na uvuvi ya mwaka wa kilimo 2019/2020.


Amesema kumekuwa na shinikizo toka kwa wafanyabiashara wanaokwenda kuisumbua Bodi ya Sukari kutaka kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi.

Soma hapa: Profesa Mkenda amtimua meneja kitengo cha mbolea TFRA

“Unajua sukari ni kama dawa za kulevya, ina hela nyingi na kila mtu anataka kufanya biashara hiyo. Kuna mwaziri wa kilimo wameondoka kwa sababu ya kutoa vibali vya sukari. Mimi sitoi ng’o,” amesema Profesa Mkenda.


Amesema pamoja na fitina zinazofanywa kutaka kutolewa vibali vya sukari kwake hatotekeleza hilo.
Profesa Mkenda amesema viwanda vya sukari kwa muda mrefu vimeshindwa kupanuka viwanda vyao kuongeza uzalishaji wa sukari kwa sababu ya sukari inayoagizwa kutoka nje.

Advertisement


Amesema Tanzania inaagiza sukari toka Malawi, Uganda na Zambia wakati miwa mingi inazalishwa Tanzania.


Profesa Mkenda amesema kila mwaka katika bonde la Kilombero inatupwa miwa tani 350,000 huku wakulima wa Mtibwa wakiacha kulima miwa kabisa kwa sababu viwanda vya sukari uwezo wake wa uzalishaji ni mdogo na miwa ni mingi.


Amesema Serikali iliamua kupitisha sheria kwamba uagizaji wa sukari utafanywa na wenye viwanda vya sukari nchini wanazalisha kuanzia tani 10,000 na kuendelea.

Soma hapa: Profesa Mkenda aongeza muda zabuni
Profesa Mkenda amesema uagizaji holela wa sukari umesababisha ukosefu wa ajira, ukosefu wa kodi ya Serikali na wakulima kukosa soko la miwa.

Advertisement