Profesa Mkenda amtimua meneja kitengo cha mbolea TFRA

Profesa Mkenda amtimua meneja kitengo cha mbolea TFRA

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ameagiza kuondolewa kwa Kaimu Meneja wa Kitengo cha Ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kilichopo Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA), Nganga Nkonya.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ameagiza kuondolewa kwa Kaimu Meneja wa Kitengo cha Ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kilichopo Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA), Nganga Nkonya.

Waziri Mkenda ameagiza kaimu meneja huyo aondolewe na arudishwe wizarani kutokana na kushindwa kuwahudumia vizuri wafanyabiashara wanaohitaji kuingiza mbolea nchini.

Ametoa agizo hilo leo Agosti 9, 2021 katika kikao chake na wafanyabiashara wa mbolea nchini, cha kujadili namna ya kupunguza bei ya mbolea ili kuweza kuwa na kilimo chenye tija.

"Yuko kijana, pale nimesema aondoke mara moja TFRA arudishwe wizarani yule niliona ushahidi watu wanaomba conrol number anawazunguusha ili walipie waingie kwenye uingizaji wa mbolea.

Profesa Mkenda amtimua meneja kitengo cha mbolea TFRA

"Badala ya kuhudumia watu yeye anazunguuka zunguuka tu. Nimesema aondoke arudi huku wizarani watu wanataka control number unamzunguusha zunguusha na ana bahati mtu kama huyu ni wa kufukuza kabisa," amesema.  

Ameongeza kuwa, pamoja na kushindwa kuhudumia wafanyabiashara hao vizuri, kwenye tangazo la kupata watu wanaohitaji kuingiza mbolea iliwekwa namba tofauti na ya wizara.

"Tangazo la Serikali lakini namba imewekwa ya bwana mmoja yuko huko Geita hajui hata nini kinaendelea.

Huyu bwana nimemuondoa na ashukuru Mungu kwasababu sisi suala la mbolea ni la kufa na kupona sio suala la mzaha na inaonekana kwamba kuna mtu alikuwa anacheza ili orodha ya waingizaji isiwe na watu wengi," amesema.

Hata hivyo, amesema Serikali imekuwa ikifatilia bei ya mbolea kwa makini, pamoja na kuangalia akiba iliyopo ili kuhakikisha bei ya mbolea inapungua.