Profesa Mkenda: Kupanda bei ya mbolea hakuhusishi tozo za Serikali

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa kuongezeka kwa bei ya mbolea nchini hakuhusishi tozo za Serikali kwa kuwa mbolea haitozwi kodi.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa kuongezeka kwa bei ya mbolea nchini hakuhusishi tozo za Serikali kwa kuwa mbolea haitozwi kodi.


Ameyasema hayo leo Julai 20, 2021 alipofanya ziara bandarini kuangalia kasi ya ushushwaji wa mbolea, ambapo amesema Serikali inafuatilia kwa ukaribu bei yake ambayo imepanda duniani kwa sababu ya uzalishaji wa baadhi ya mazao kupungua wakati wa mlipuko wa kwanza wa virusi vya Corona.


Amesema Serikali inapambana bei ya mbolea isipande sana, ambapo mwezi mmoja uliopita alikutana na wauzaji wa mbolea nchini ambao pia wametaja moja ya sababu ilikuwa ni shehena ya mbolea ikiingia inachelewa kushushwa.


“Lakini niwahakikishie wakulima bei mnayoiona haikutokana na tozo ya Serikali kwa sababu mbolea haitozwi kodi mahali popote, sehemu moja wapo ya gharama kuwa kubwa ni ucheleweshwaji wa kushusha mbolea lakini nyingine ni upandaji wa mbolea dunia nzima.


“Hata hivyo Serikali tunaendelea na jitihada kuhakikisha bei ya mbolea inashuka. Niliagiza meli yenye mbolea ikija itapokelewa kama iliyobeba silaha ikifika moja kwa moja kushusha, zamani walikuwa wanakaa mpaka siku 10 matokeo yake gharama inakuwa kubwa kwa sababu mwenye meli nae anachaji hela, kwahiyo sasa hivi utaratibu umebadilika,”alisema.


Kaimu Meneja wa sehemu ya Kichele TPA, Tatu Moyo alisema meli ya mbolea inayoshusha iliingia Julai 15 ikiwa na tani 33,000, nyingine itaingia Julai 25 ikiwa na tani 11,000, Julai 29  itaingiwa ikiwa na tani 4753 ya mbolea, pamoja Julai 31, mwaka huu ikiwa na  tani 9,400 ya mbolea.


“Katika kuendeleza kilimo hapa bandarini tuna meli ya lita 20,000 za viuatilifu vya maji kwaajili ya kilimo imeingia saa hizi asubuhi na nyingine itaingia mchana ikiwa na kilo 366,000 ya sulpher ya unga kwaajili ya mikorosho,” alisema Tatu.


Mmoja wa waingizaji mbolea nchini kutoka kampuni ya Export Trading (ETG), Hasina Abdul alisema changamoto wanayoipata ni katika kusafirisha mbolea, hivyo wanaomba magari yasipite kwenye mizani yawe yanaenda moja kwa moja sehemu husika.