PSSF yatumia Sh80 bilioni kulipa wastaafu Kusini

Meneja wa uhusiano na Elimu kwa Umma, kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), James Mloe. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
- Baadhi ya halmamshauri katika mikoa ya Kusini zadaiwa kuwa na changamoto katika kuwasilisha michango wa watumishi wake katika mfuko wa madeni ya watumishi wao kwenye Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSF) Kanda ya Kusini.
Lindi. Halmashauri zilizopo katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, zimetajwa kukabiliwa na changamoto ya kutowasilisha michango ya watumishi wao kwa wakati na hivyo kuchelewesha malipo ya wastaafu.
Hayo yamesemwa jana Jumatatu Novemba 13, 2023; na Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSF) Kanda ya Kusini, Sayi Lulyalya, kwenye mkutano wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaoendelea mkoani Lindi.
Amesema kuwa juhudi ambazo wamefanya ni kuhakikisha halmashauri zote zinalipa madeni kwa watumishi wao, na kwamba katika harakati hizo, halmashauri zimelipa zaidi ya Sh80 bilioni na kwamba wamebaki wanachama wachache ambao bado hawajalipwa.
"Tunashukuru kwa hatua tuliyofikia sisi kama mfuko wa PSSF kwa kujitahidi kupunguza madeni kwa wastaafu wetu, na kubakia wastaafu wachache na pia halmashauri zetu kulipa madeni ya watumishi wake," amesema Lulyalya
Kwa upande wake, Meneja wa uhusiano na Elimu kwa Umma PSSF, James Mloe ameonya kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwalipa wastaafu na kwamba ni vema wakaepuka watu wanaowapigia simu kuwadai hela kwa lengo la kutaka kuwasaidia kupata mafao yao.
"Kumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaotumia teknolojia ya mawasiliano ya habari (IT), wamekuwa wakijitambulisha kama viongozi wa Serikali wanaotoka hazina au Tamisemi na kutega mitego ya mawasiliano na kupata taarifa za wateja na mwisho wa siku wanawatapeli wastaafu, kwa kujifanya ni watumishi wa umma au watumishi wa mfuko," amesema Mloe na kuongeza;
"Niwatahadharishe, wastaafu wote kupitia mfuko wa PSSF, kuwa Serikali haitoi malipo yoyote kwa wastaafu, unapopigiwa simu na kutakiwa kutuma hela ili usaidiwe, usikubali hao ni matapeli, utaratibu wa Serikali yetu unajulikana fedha zote zinatumwa kwa mfumo maalumu uliowekwa na Serikali."
Naye Afisa Uhusiano wa mfuko huo, Fatma Elhady amewaomba watumishi ambao bado hawajajiunga na mfuko wa PSSF wajiunge na kwamba watapata mafao ya kuugua pamoja na kupata kwa wakati mafao ya kustaafu na kiinua mgongo.
"Mfuko huu wa PSSF ni kwaajili ya watumishi, hivyo niwaombe kujiunga na mfuko wa wetu," amesema Fatma