RC Lindi aagiza watendaji Amcos kukamatwa

- Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainabu Telack akizungumza jambo na wadau wa korosho. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack amemwagiza Kaimu Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa waLindi, Cesilia Sositenes kuwakamata watendaji wa Amcos ya Mbwemkuru iliyopo Wilaya ya Liwale mkoani hapa.
Lindi. Mkuu wa Mkoa waLindi Zainabu Telack, amemwagiza Kaimu Mrajisi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi, Cesilia Sositenes kuwakamata watendaji wa Chama cha msingi cha ushirika (Amcos) cha Mbwemkuru kilichopo wilayani Liwale Mkoani Lindi, kutokana na ubadhirifu wa Sh27 million za wakulima.
Akizungumza kwenye kikao cha tathimini ya mazao ya ufuta na mbaazi kwa mwaka 2023 na mandalizi ya msimu wa ununuzi wa korosho 2023/2024 leo Jumatano Oktoba 4, 2023, Telack amesema Amcos hiyo kuanzia leo wasijishughulishe na upokeaji wa mizigo kwa msimu wa korosho na watendaji wote waliohusika wakamatwe na kupelekwa Mahakamani.
"Mrajisi kwanza kafunge hicho chama na kwenyekorosho wasiingie kununua korosho hadi watakapo fanya uchaguzilakini hiyo fedha walioiba katengenezeni mashtaka mpeleke mahakamani.
"Mali zao zitaifishiwe walipwe wakulima na nataka kusikia kesi imeanza kusikilizwa,” amesema Telack.
Awali akiwasilisha taarifa kwa mkuu wa mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Gudluck Mlinga amesema tangu mwaka 2017 wakulima wanadai fedha za korosho na Amcos ya Mbwemkuru ilisababisha hasara.
"Baada ya kuwakamata wale watendaji wa Amcos, nikawatoa ili waje kulipa fedha za wakulima lakini cha kushangaza mwenyekiti wa Amcos ile akanywa sumu, mimi nikamtibu.
“Akipona baada ya kupona atafunguliwa kesi mara mbili; upotevu wa fedha za wakulima fedha zao na kesi nyingine kutaka kujiua," amesema Mlinga bila kumtaja kiongozi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ruangwa, Nachingwea na Lindi (Runali), Audas Mpunga amesema kuwa taarifa ya Amcos ya Mbwemkuru wameipata na wanapitia taarifa ipo kwa Mrajisi na ofisa ushirika wa wilaya.
"Nilifanya ziara pamoja na wakuguzi wangu wandani tatizo hilo tumelikuta na kuna vyama sugu wilayani Liwale na watu waliosababisha hiyo hasara wafuatiliwe na wakulima walipwe," amesema Audas.
Katika hatua nyingine, RC Telack amewataka wakulima wa korosho kuhakikisha wanazingatia ubora, ilikuweza kupata bei nzuri pindi minada inapoanza na pia amesema kuwa korosho kwa msimu wa 2023/2024 zitasafirishwa kwa njia ya bandari.
"Mwaka huu korosho zote za Lindi zitasafirishwa kwa njia ya bandari ya Mtwara na mnada mwaka huu unaanza Oktoba 21, niwaombe wakulima na viongozi mhakikishe mnasimamia korosho ipasvyo, korosho isiletwe Ghalani zikiwa hazina ubora," amesema.