Rufaa dhidi ya Mbunge Gekul, hukumu leo

Muktasari:

  • Hashim Ally  anayewakilishwa mahakamani na Wakili Peter Madeleka, alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara akisema hajaridhishwa na amri ya kuifuta kesi hiyo.

Moshi/Arusha. Mbivu na mbichi kujulikana leo Jumatatu, Aprili 15, 2024 kwa kile kitakachojitokeza wakati wa kusomwa kwa hukumu ya rufaa ya jinai iliyofunguliwa na Hashim Ally dhidi ya Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul.

Awali, Hashim alimfungulia Gekul ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, kesi ya jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Babati akimtuhumu kumfanyia shambulio la kudhuru mwili analodai kufanyiwa Novemba 11, 2023.

Desemba 27, 2023, Hakimu Victor Kimario aliifuta kufuatia uamuzi wa DPP kumfutia mbunge huyo kesi hiyo kwa kutumia kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20 kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Hata hivyo, Hashim anayewakilishwa mahakamani na Wakili Peter Madeleka, alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara akisema hajaridhishwa na amri ya kuifuta kesi hiyo iliyotolewa na Hakimu wa Wilaya ya Babati, Victor Kimario, akijenga hoja sita.

Katika Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, mbele ya Jaji Devotha Kamuzora, baada ya kukamilika usikilizwaji wa hoja za pande mbili, amepanga kutoa hukumu yake leo saa 8:00 mchana, kwa mujibu wa wito wa Mahakama.

Wito huo wa kuitwa shaurini wa Aprili 3, 2024, umesainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara na Wakili Madeleka alilithibitishia Mwananchi Digital kupokea wito huo wa mahakama na yeye na mteja wake wako tayari kupokea uamuzi.

Katika rufaa hiyo, hoja ya kwanza ni kwamba hakimu alikosea katika sheria na ukweli kwa kushindwa kuzingatia matakwa ya sheria chini ya Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania ambayo inatoa haki ya msingi ya kusikilizwa na kupata haki.

Ibara hiyo inasema: “Wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kingine kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu.”

“Na pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo kingine kinachohusika,” Inasema ibara hiyo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake.

Katika rufaa hiyo waomba rufaa walikuwa na hoja sita ambazo zote waliziwasilisha mahakamani hapo na siku hiyo Machi 21, mwaka huu, Jaji huyo alisikiliza kwa mara ya kwanza rufaa hiyo sambamba na pingamizi la awali  lililoibuliwa na mrufaniwa (Pauline), siku moja kabla, Machi 20, akipinga rufaa hiyo kusikilizwa, huku akiwasilisha  hoja tatu.

Katika hoja ya kwanza, Gekul alidai Mahakama haikuwa na uwezo wa kusikiliza rufaa hiyo kwa kuwa sababu ya kwanza na ya pili ya rufaa ilikuwa imehusisha hoja zinazohusu katiba na kwa maana hiyo Mahakama hiyo haikuwa ya kikatiba.

Sababu ya pili, alieleza rufaa hiyo imewasilishwa mapema kabla ya wakati na hivyo haistahili kusikilizwa na sababu ya tatu alieleza kuwa kesi haipaswi kuzingatiwa kwa ujumla.

Mrufani kupitia mawakili wake watatu wakiongozwa na Wakili Madeleka walisema mapingamizi hayo hayakuwa mashiko na kusisitiza Mahakama hiyo ina mamlaka ya kisheria kupokea rufaa zote zinazotokana na maamuzi ya Mahakama za chini.

“Kusema kwamba haina mamlaka ni kukosa upungufu wa usahihi na hoja nyingine ni kwamba DPP hakuwa sehemu ya kesi, hivyo hakuwa na mamlaka na haki ya kuingilia kesi ile kwa namna ambavyo aliingilia”, alisema wakili Madeleka na kuongeza:-

“Kwa sababu hati ya kutokuwa na nia kuendelea na mashtaka haikuingizwa mahakamani kwa njia zinazoelekezwa na sheria.”

Baada ya kusikiliza pingamizi hilo, Jaji alisema uamuzi juu ya pingamizi hilo atautoa pamoja na hukumu ya rufaa hiyo.


Tuhuma zilivyokuwa

Kwa mujibu wa hati ya malalamiko ya kesi hiyo, mbunge huyo alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la shambulio na kusababisha madhara kwa mwili chini ya kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marekebisho ya mwaka 2022.

Gekul anadaiwa kuwa yeye na watu wengine ambao hawawepo mahakamani kuwa Novemba 11, 2023 , mjini Babati, walimuita Hashim na kumuweka kizuizini,huku wakimtishia kwa silaha ya moto.

Kisha walimvua nguo na kumshambulia kwa kumlazimisha kukalia chupa ya soda, ili iingie katika njia yake ya haja kubwa.

DPP aliwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha CPA, kinachompa mamlaka ya kufuta kesi yoyote ya jinai katika hatua yoyote kabla ya hukumu ya Mahakama na bila kulazimika kutoa sababu za uamuzi huo.