Sababu 20 upungufu nguvu za kiume, matibabu yake

Muktasari:

  •  Dk Ali Mzige, Mtaalamu wa afya ya jamii na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya kabla hajastaafu mwaka 2005, ameyataja mambo 20 yanayochangia kuvuruga mfumo wa mwili na ubongo na kusababisha upungufu wa nguvu za kiume, na matibabu sahihi anayopaswa kutibiwa mwathirika.

 “Upungufu wa nguvu za kiume au za kike sio ugonjwa, bali ni dalili kuwa kuna kasoro katika mfumo wako wa mwili pamoja na ubongo,” ndivyo anavyoanza kusema mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige.

Anasema changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume huwakumba wanaume wengi, hali inayowafanya wasake matibabu kila kona, wakiamini matumizi ya dawa za viwandani, mitishamba na ulaji wa baadhi ya vyakula kama supu ya pweza, vumbi la Congo, alkasusu ni suluhisho.

Kwa mujibu wa Dk Mzige aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya na kustaafu mwaka 2005, anasema hakuna dawa ya nguvu za kiume.

Bali anasema unywaji wa maji mengi, ulaji wa vyakula jamii ya mikunde na mizizi ikiwemo choroko, mbaazi na mboga za majani kuwa tiba halisi.

Dk Mzige anasema watu wengi hutumia baadhi ya vitu kwa malengo ya kuongeza nguvu za kiume.

“Utakuta mtu anatumia karanga mbichi, mihogo mibichi, vipande vya nazi, supu ya pweza, alkasusu, hivi ni vitu visivyoenda moja kwa moja kuongeza nguvu hizo kama w

New Content Item (1)
New Content Item (1)

anavyodhania, bali ni vichocheo na kuongeza homoni ya kiume iitwayo ‘testosterone’,” amesema.


Sababu 20 hizi hapa

Daktari huyo anazitaja sababu 20 zinazochangia tatizo la ukosefu wa hamu ya tendo la ndoa na upungufu wa nguvu za kiume, kuwa ni pamoja na upungufu wa damu.

“Upungufu wa wekundu wa damu ‘anemia’, mara nyingi mwenye kadhia hii lazima atakuwa na upungufu wa nguvu za kiume au za kike. Kwa mwanaume kiwango au kiasi cha damu inayohitajika ili uume ufanye kazi na damu hiyo ifikie mililita 127,” amesema Dk Mzige.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ametaja sababu nyingine kuwa ni tabia ya kujichua ambayo amesema ni tatizo sugu na huchangia upungufu wa nguvu za kiume na za kike, lakini pia umri ukipitiliza zaidi ya miaka 65.

Ametaja ugonjwa wa kisukari ambao nao bado haujadhibitiwa, shinikizo la damu, “Wengi wana changamoto ya shinikizo la damu yaani ‘presha’ lakini hawajui hali zao. Hii inaanza kwa kukuonyesha dalili mbalimbali ikiwemo kushindwa kufanya tendo au nguvu kupungua, unapaswa kutafuta wataalamu wa afya na si kurukia viagra au vumbi la Congo,” amesema Dk Mzige.

Michepuko yatajwa

Daktari huyo amesema chanzo kingine ni ‘michepuko’, lishe duni, kutokufanya mazoezi ya mwili na viungo kubweteka.

Amesema hata wenye matatizo katika valves za moyo, uvutaji wa sigara, shisha, mirungi pia ni chanzo cha kupunguza hamu ya tendo kwa baadhi ya watu, huku akiitaja mirungi kuwa na tabia ya kukausha sehemu za ndani za uke wa mwanamke yaani kuondoa ‘ute’.

Pamoja na hayo ametaja sababu nyingine ni unywaji wa kupindukia wa kahawa, maumivu ya mgongo eneo la chini katika kifundo cha mwisho cha uti wa mgongo na utumiaji wa dawa za kulevya ikiwemo pombe kupita kiasi.

Amesema asilimia 20 ya wagonjwa wa akili wodini, kisababishi kikubwa ni unywaji wa pombe uliokithiri na wakifikia hatua hiyo hukosa kabisa hamu ya tendo.

“Upungufu wa homoni ya kiume ‘testosterone’ haswa kwa watumiaji wa bangi, kwani kilevi hiki hutengeneza homoni za kike oestrogen kwa kuwa kokwa zina sinyaa na mvutaji wa bangi kabla hajapevuka anakuwa na tabia za kikekike,” amesema.

Dk mzige ametaja walio hatarini kupata changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume ni pamoja na vijana wanaovaa chupi na suruali za jinzi za kubana, “wanapata tatizo hilo na mwisho wanaweza kupata saratani ya korodani.”

Amesema sehemu za kiume zinapaswa kupata hewa ya kutosha ikizizunguka korodani zote mbili.

“Hakikisha mtoto wako wa kiume akiwa na umri wa miaka miwili, korodani zote mbili ziko kwenye mfuko wake, kokwa zote mbili ziwepo. Kama bado hazionekani, muhimu kumuona daktari wa upasuaji wa watoto ziteremshwe chini,” amesema.

Dk Mzige ametaja pia msongo wa mawazo na sonona kuwa ni chanzo pamoja na umasikini.

Amesema mara nyingi mwanaume akiwa hana fedha na ana mambo mengi yanayohitaji fedha, hujikuta akishindwa kupata nguvu.

Ametaja pia unene uliokithiri kwa mwanamke au mwanamume, kijana au mzee kisababishi cha kupata kadhia ya upungufu wa nguvu za kiume.

“Mama mwenye unene uliokithiri anaweza kuchelewa kupata mimba hata kama hatumii dawa za uzazi wa mpango, huku akitaja uchafu sehemu za siri pia huchangia tatizo hilo.”

“Wanaume wanaougua tezi dume au tezi dume lililovimba wanaweza kuwa na upungufu wa nguvu za kiume, mwanamke anayetia ugoro kule kwenye uke wake kuondoa hamu ya kujamiiana, anaweza kupata saratani ya shingo ya kizazi, hivyo nguvu hupungua.”

Dk Mzige ametaja tabia ya kukaa kwenye kiti zaidi ya saa nne kuwa sawasawa na kuvuta sigara 14.

“Angalizo lingine hiyo mihadarati wanayotumia vijana, shisha, kuberi, ugoro, mirungi, bangi, sigara na kadhalika sio suala la upotevu wa nguvu za kiume pekee. Pia wanajiweka katika hatari ya kuugua kifua kikuu cha mapafu.

“Hapo mbeleni uwezekano upo wakapata saratani mbalimbali za kifua, koo, shavu, mdomo na aina nyingine.”


Matibabu sahihi

Kwa mujibu wa Dk Mzige, matumizi ya dawa za viagra, vumbi la Congo, supu ya pweza, alkasusu na dawa nyinginezo hazitibu tatizo, bali huongeza msukumo wa damu na kusababisha changamoto zingine kiafya.

“Msitafute udongo kutoka Zaire hausaidii kitu, supu ya pweza ni hadithi tu. Upungufu huu si ugonjwa, kama unakunywa pombe na ndiyo inakuathiri huna budi kuiacha, kile unachougua kiache kama hupati usingizi tafuta nini kinasababisha usipate usingizi.”

 “Watu wasidanganye wanatibu nguvu za kiume, siyo kweli wanaojichua hata zile sehemu zinaathirika, kilichopo ni kuacha kile kinachokuletea matatizo,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mzige kwa mwanaume uchangiaji wa damu, husaidia kuimarisha mfumo wa kinga na huusaidia mwili kutengeneza damu nyingine.

“Utakuwa ni sawa na gari lililokwenda matengenezoni likabadilishwa vipuri vilivyoharibika na mafuta machafu, unakuwa na damu nyingine nzuri na yenye kinga za kutosha, licha ya kwamba utakua unajua afya yako,” amesema.

Amesema mara nyingi wanaume wanaposumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu hupungukiwa nguvu za kiume na kwamba linaweza kusababishwa  kimwili, kisaikolojia na kitabia.

“Matibabu sahihi ni kujaribu kupima vipimo sahihi kilichosababisha tatizo hilo kurekebisha, kwa dawa za kisukari kwa wenye kisukari na dawa za kudhibiti shinikizo la damu na kujiepusha na visababishi vya unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara na kutoa huduma za kisaikolojia tiba kwa wale wenye msongo wa mawazo na sonona,” amesema.

Dk Mzige amesema kuwa zipo  dawa ambazo wahusika hawapaswi kuzinunua kiholela bila cheti cha daktari, ambazo zinaweza  kuimarisha kiwango cha damu kiweze kufika kwenye via vya uzazi.

Amesema pia lishe duni inapaswa kuimarishwa na upungufu wa damu anemia ni muhimu kurekebishwa hususan kwa wajawazito.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

 “Dawa za mitishamba zinatangazwa sana kibiashara, ni vema wenye tatizo hilo waende vituo vya afya, watapimwa na kutoa historia ya magonjwa. Tiba siyo ya siku moja inatakiwa ufuatiliaji,”amesema.

Amesema kuna tiba sahihi kama zinazotolewa na Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Jijini Dodoma ya kuweka vipandikizi katika uume, ambazo gharama yake ni Sh8 milioni au zaidi, hata hivyo siyo wote wana uwezo wa kuzifukia.

“Homoni za kiume zikipungua au kama hazitengenezwi na mwili wako, itabidi upimwe damu na homoni hiyo itolewe kwa njia ya sindano. Dawa za kienyeji za asili kama zipo nazo zina maelekezo yake,” amesema.


Vyakula sahihi

Pia Dk Mzige ametaja aina za vyakula vinavyoweza kuchochea afya bora ya afya ya uzazi kuwa ni vyenye madini ya zink kwa wingi. “Kuna vyakula vya mikunde mbaazi, choroko, mboga za majani maharage, matunda na vyakula jamii ya mizizi na karanga na vingine vya protini.”

“Wengi hawajui, chakula ndicho kitakufanya ukanenepa kupita kiasi, au ukawana nguvu imara za kiume. Hunywi maji ya kutosha unaharibu figo lakini mwili wa binadamu kama gari lazima upate maji ya kutosha, usingizi wa kutosha, vyakula asilia, mazoezi, punguza kitambi hata magonjwa mengine yatatoweka oksijeni ikiwa nyingi mwilini,” amesisitiza.


Asili ya nguvu za kiume

Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (MUHAS), Fredrick Mashili ametaja saikolojia na kwamba ubongo unahusika katika tendo hilo, lakini kikubwa ni vichocheo ‘homoni ya kiume’.

Amesema kiwango cha homoni hii huongezeka zaidi nyakati za asubuhi.

“Kwenye uume kuna mishipa mikubwa ya damu, halafu wenyewe upo kama sponji hivyo mwanaume anavyojengeka kisaikolojia kuwa tayari kwa lile tendo, damu hutoka katika maeneo mengine ya mwili na kushuka chini. Damu ikienda katika uume hushibisha ile mishipa inatanuka, uume hurefuka na kunenepa na ndipo nguvu za kiume hutokea,” amesema.

Dk Mashili ametaja sababu kubwa inayoleta shida kwa wengi kuwa ni mishipa ya damu, “hapa ndiyo unakutana na dawa za kuongeza nguvu ambazo kazi yake hushusha damu kwenye uume, mwili hauwezi kufanya kazi wenyewe mpaka nguvu ya dawa na ndiyo maana huwa zinaua sana.”

Amesema kabla mtu hajatumia dawa hizo anashauriwa na daktari na kwamba hushauriwa watu za zaidi ya miaka 60, kwa sababu zina madhara na ukishaanza kutumia kuna uwezekano hutaweza kuwa na nguvu mpaka uzitumie.

Amesema wataalamu waliweka umri huo kwa kuwa kawaida mwanaume akifikia umri huo kiwango cha homoni hiyo hupungua mwilini.