Samia: Tunajenga bandari ya kwanza ya kisasa tangu uhuru

Rais samia katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa.

What you need to know:

  • Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Kilwa kuchangamkia fursa za ajira na kufanya uvuvi wa kisasa baada ya Serikali kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi huku akiisifia kuwa ni ya kisasa na ya kwanza kujengwa tangu uhuru.

Kilwa. Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Kilwa kuchangamkia fursa za ajira na kufanya uvuvi wa kisasa baada ya Serikali kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi huku akiisifia kuwa ni ya kisasa na ya kwanza kujengwa tangu uhuru.

Rais Samia ameyasema hayo leo jumanne Septemba 19, 2023, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari hiyo, ambayo bado kukamilika itagharimu zaidi ya Sh.260 bilioni, pamoja na kugawa boti za uvuvi 34 kati ya 62 kwa wavuvi wadogo pamoja na wanawake wanaolima mwani.

“Huu mradi wa ujenzi wa bandari ya kisasa...ni wa kwanza kwa Tanzania, na fedha hizo za ujenzi wa bandari zimetolewa ili Wanakilwa waweze kuchangamkia fursa za ajira na kufanya uvuvi wa kisasa kwa ajili ya kuongeza kipato na kuboresha maisha yao,” amesema na kuongeza;

"Serikali imetoa boti kwa mkopo wa bei nafuu, niwaombe wavuvi na wakulima wa mwani kuzitunza boti hizi na muweke ahadi yenu ya kulipa mkopo huu kwa wakati kwani ni nafuu...ninataka kuona Kilwa ya sasa inabadilika baada ya miaka miwili au mitatu.”

Rais amewataka wakazi wa Kilwa kutoa ushirikiano kwa Serikali katika mradi wa bandari hiyo, na hivyo kufanikisha mradi huo kukamilika kwa wakati.

“Bandari ikikamilika soko la samaki lipo la kutosha na tunafikiria kujenga bandari ya Bagamoyo, pia bandari hii itakapoanza kujengwa, ajira 3000 zitazalishwa, kipaumbele kitawekwa kwa vijana wa kilwa," amesema Rais Samia.

Aidha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema kuwa, bandari hiyo itakapo malizika, kutakuwa na karakana kubwa ambayo meli zitakuwa zinatengenezwa, huku akisema itakuwa pia na sehemu ya kupaki meli 10 kwa wakati mmoja .

“Hii bandari ya uvuvi, itakuwa na karakana ya meli ambazo zitatengenezwa hapa hapa nchini katika eneo la kilwa, zitakuwa meli zenye urefu wa mita 30, pamoja na karakana ya kutengeneza nyavu, pia bandari hii itachukua mashua na mitumbwi 200, pamoja na boti.

Hassani Masudi, mmoja wa wanufaika wa boti hizo, ni mkazi wa Kilwa Masoko, amesema kuwa, boti hizo zitawasaidia katika kuongeza kipato na kulipa mkopo kwa wakati, “kwani ni boti za kisasa na zimefungwa GPS ambayo itasaidia kuona maneo ambayo yana samaki.”

Kwa upande wake Mwanahawa Jumbe, amemshukuru Rais Samia kwa kuwakabidhi boti hizo, “ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa, na kwa uhakika, kufanya shughuli ya kilimo cha mwani. Mwanzoni tulitumia boti za kukodi, ila sasa tumepata za kwetu, zitarahisisha kazi.”