Serikali: Akiba fedha za kigeni inakidhi mahitaji

Serikali: Akiba fedha za kigeni inakidhi mahitaji

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema akiba ya fedha za kigeni nchini Tanzania imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.


Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema akiba ya fedha za kigeni nchini Tanzania imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.

Amefafanua kuwa hadi Aprili 2021 akiba ya fedha za kigeni ilikuwa Dola 4.97 bilioni za Marekani  ambayo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takribani miezi mitano.

Dk Nchemba ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 10, 2021 bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2020 na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kiwango hicho ni zaidi ya lengo la nchi la kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa muda wa miezi minne  na ni zaidi ya lengo la miezi minne na nusu kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kuhusu mwenendo wa thamani ya Shilingi, amesema thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imeendelea kuwa tulivu ambapo dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh 2,298.5 Aprili 2021, ikilinganishwa na wastani wa Sh2,291.3 Aprili 2020.

“Utulivu wa shilingi umetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika usimamizi wa Sera za Fedha na Bajeti, kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje ya nchi pamoja na mwenendo chanya wa baadhi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii,” amesema.

Amebainisha kuwa hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kusimamia misingi ya uwazi katika ununuzi na uuzaji wa fedha za kigeni nchini zimechangia thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani kuwa tulivu.