Serikali lawamani matumizi ya 'energy drinks'

Muktasari:

  • Yalaumiwa kukithiri matumizi ya vinywaji vinavyotajwa kuwa madhara pombe kali, energy drinks.

Dar es Salaam. Kushindwa kuweka sera madhubuti na kudhibiti utumiaji holela ya vinywaji vikali na vile vya kuongeza nguvu maarufu kama energy drinks, kumetajwa ni chanzo cha kukithiri na hatimaye madhara kwenye afya za wananchi.

Kutokana na hilo, wanasheria, wananchi na wadau wa masuala ya afya wameitaka Serikali kuja na sera zitakazodhibiti uingizaji, uzalishaji na matumizi ya vinywaji hivyo, badala ya kuangalia tu mapato na makusanyo ya kodi, ili kupambana na unywaji holela unaoambatana na athari za kiafya.

Maoni hayo yametolewa siku moja baada ya Mwananchi Digital kuchapisha habari iliyowanukuu wataalumu wa afya wakisema pombe kali na energy drink ni miongoni mwa visababishi vya magonjwa moyo, ini na figo ambayo yameanza kuwaathiri hata kwa vijana.

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya Dodoma juzi ilitangaza kuwa inapokea wagonjwa wapya wa figo wanne mpaka tisa kila wiki, wenye umri kati ya miaka 24 mpaka 40, ambao hufika hospitalini hapo figo zao zikiwa kwenye hatua ya nne ya ugonjwa, ambayo ni sugu na matibabu yake ni kupandikizwa nyingine.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wanasheria na wadau wa afya wameshauri Serikali ichukue hatua kwa kuhuisha sheria zilizowekwa na kufuata Katiba ya nchi katika kulinda afya ya jamii.

Mwanasheria na wakili maarufu, Jebra Kambole amesema wananchi wana haki ya kupata usalama, ikiwa ni pamoja na kula na kutumia vinywaji bora na vyenye viwango.

"Kama walaji wana haki ya kupata taarifa na kupata fidia kutokana na madhara kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1)(b) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayosema kwamba ‘lengo kuu la kwanza la Serikali ni ustawi wa watu wake’," amesema.

Kambole amesema madhara hayo yanatokana na Serikali kutokujali ustawi wa watu wake, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania (TMDA) wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

“Kampuni zinazouza energy na vitu vingine vyenye madhara zina wajibu wa kuhakikisha bidhaa zao hazina madhara, kama yapo basi wanayapunguza. Kwa mfano, chupa zao zinaathiri sana uoto wa asili na uchafuzi baharini.

“Lakini hawafanyi lolote kutatua tatizo hilo, wana wajibu pia wa kuwalinda hawa walaji ikiwa ni pamoja na kuiunga mkono Serikali kununua dawa na mashine za kutibu madhara ya energy drink na pombe kali,” amesema.

Kwa mujibu wa Kambole, Serikali inapaswa kulisimamia hilo kwa kuweka sheria na sera nzuri za wajibu wa kampuni za ndani na za nje kwa wananchi wake.

“Siyo kama sasa, kampuni zinajiamulia ni lini na wapi watoe msaada gani? Na hili ni lazima liangaliwe kwa undani,” amesisitiza.

Mtazamo wa Kambole ni sawa na wa aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshala aliyesema wataalamu wa afya wameshaonyesha njia ya kuainisha madhara, hivyo Serikali haina budi kuchukua hatua.

“Tangu mwaka 2023, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ilitoa chapisho na leo Benjamin Mkapa wameainisha ukubwa wa tatizo, Serikali ichukue hatua.

“Uamuzi ufanyike, maana kuna watu wanalinda masilahi yao. Kuna madhara makubwa kwa vijana tunazungumzia miaka 20 baadaye, kutakuwa na matatizo makubwa ya figo na saratani na atakayeyagharamikia ni walipa kodi haohao, njia ya kuepusha hivyo vitu ni kupiga marufuku na kuviondoa,” amesema Dk Nshala, mwasisi wa Chama cha wanasheria watetezi wa mazingira (LAET).

Wakati wanasheria wakisema hayo, mtaalamu wa saikolojia, John Ambrose amesema licha ya faida zilizopo, ikiwemo kuchangamsha mwili, vinywaji hivyo huleta au kusababisha uraibu, hivyo huathiri utendaji wa kawaida wa akili na matendo ya mwili kupata changamoto.

“Pia kuna kuathirika kimwili, ogani kama ini huathirika zaidi na utumiaji hatari wa pombe. Hizi husababisha ini kupata makovu ambayo si rahisi kutibika. Kwa vijana chini ya miaka 22 kwa matumizi ya pombe na energy drinks ni hatari zaidi kwa sababu huathiri ukuaji na uwezo wa ubongo kufanya kazi,” amesema.

Vilevile, amesema kuna kipindi aliwahi kufanya utafiti mdogo na kubaini unywaji wa energy drink katika vyuo vikuu, hasa wakati wa mitihani, ni mkubwa.

“Nilifanya utafiti mdogo kwenye vyuo vitatu jijini Dar es Salaam (anajitaja), kati ya wanafunzi 30 niliowahoji, wasichana wakiwa 20 na wavulana 10, wote kwenye kipindi cha mitihani hutumia energy drinks,” amesema.

Amesema kati yao, asilimia 60  wamesema (energy drink) ingekuwa na madhara isingeuzwa sokoni, asilimia moja wamesema muulize Profesa Janabi, asilimia 30 wamesema wanatumia kiasi kidogo haina shida na asilimia 9 wamesema hawajui.


Kauli ya Serikali
wakati Serikali ikitupiwa lawama kwa kutochukua au kuchelewa kuchukua hatua, yenyewe imesema iko mbioni kukamilisha utafiti.

Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu suala hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema,  ili Serikali ifanye uamuzi wa misimamo ya kisera au sheria kwenye mambo yanayohusu afya ya watu, lazima iongozwe na utafiti.

Amesema vinywaji vya energy drink vilifanyiwa tafiti za awali na kuonyesha athari, hivyo Serikali imeshachukua uamuzi wa kufanya utafiti na maandalizi ya mwisho yanakamilika, ikiwemo kukusanya fedha za kufanyia utafiti huo.

"Serikali imekabidhi jukumu hili kwa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), ambayo kwa sasa inakamilisha taratibu zake na maandalizi, utafiti utatupatia mwanga wa nini kinapaswa kufanyika," amesema Matinyi.


Kwa nini vipi?

Baadhi ya wananchi wamehoji sababu ya uwepo wa vinywaji hivyo na kuuzwa kiholela kwa watu wote, wakiwemo watoto wadogo.

Mkazi wa Mbweni jijini Dar es Salaam, Japhet Mwandu amesema kuna haja ya Serikali kuchukua hatua za haraka, ili kuepusha kizazi ambacho kinafanya maamuzi ya kutumia vinywaji, hivyo bila kujua madhara, hasa watoto wadogo.

“Nashauri licha ya kuweka masharti makali kwa wazalishaji na wasambazaji, bei zipandishwe, hii ndiyo namna pekee ya kuwafanya watu wasitumie kiholela kama ilivyo hivi sasa,” amesema Mwandu.

Timoth Mhagama ambaye ni mkazi wa Morogoro amesema, “Serikali ichukue hatua madhubuti kuokoa watu wake, pia hizo energy drink zinachangia uchafuzi wa mazingira na bahari kwa kiasi kikubwa.”


Wataalamu wa afya

Pamoja na kueleza madhara ya kiafya, wataalamu wa afya wameshauri njia mbili za kufanya ikiwemo kutoa elimu na kutungwa kwa sera pamoja na kuhuisha miongozo iliyopo, kwa wazalishaji, waingizaji na wasambazaji wa bidhaa hizo.


Sababu ni nyingi

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilanha amesema chanzo cha figo kufeli ni mambo mengi, lakini lazima nchi ichukue hatua.

“Tunahitaji kutafiti kisayansi na tuje na majibu kuhusu hili tatizo. Ipo wazi hawa vijana wanatumia mara nyingi kutokana na aina ya kazi wanazofanya na wanajikuta wanaongeza presha kwa kuwa hawalali, na presha ikikaa kwa muda mrefu bila kutibiwa itaanza kuleta shida kwenye figo,” amesema Dk Ndilanha.

Moja ya njia za kuondokana na hilo, Inapendekezwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti kutoka Taasisi ya Moyo ya jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Palangyo aliyesema elimu ni muhimu kwa kuwa wengi hawajui madhara ya energy drinks, wanakunywa kupata ladha na wengine kukata kiu.

“Sigara ilielezwa sana madhara yake na ndiyo maana leo wavutaji ni wachache na madhara wanapata wachache. Unywaji wa energy drink haijawahi kusemewa, mwaka jana sisi tulitoa chapisho lakini tulipingwa vibaya bungeni.

“Ikionekana tunataka kuua biashara ya watu na kwamba hivi vinywaji vinaingiza kodi kubwa. Angalau wizara baadaye ilitoa matangazo machache kukataza, kisha ikakaa kimya,” amesema.

Dk Pedro amesema kuna umuhimu vitu vyenye athari kwenye afya vipigwe kodi kubwa, sababu zipo aina nyingi na vinywaji, hivyo zitaleta athari lakini zipo zenye athari zaidi.

“Inahitaji mkono wa Serikali kuweka sera zitakazobana uingizaji na matumizi pia bei zipandishwe hii ni namna ya kuwafanya watu wasitumie kiholela kama ilivyo hivi sasa,” amesema.


Tafiti….

Kwa mujibu wa ripoti inayoitwa 'Tanzania Energy Drinks Market 2023', utafiti wa hivi karibuni unaonesha biashara ya vinywaji hivi nchini, inatazamiwa kukua kwa kiwango cha dola milioni 13.3 kati ya mwaka 2023 na 2028.

Ingawa watumiaji hao ni wa rika mbalimbali na kwa sababu mbalimbali, watumiaji wakubwa ni wale walio na umri wa kati ya miaka 24 na 40 na ndio waliotajwa na Mwananchi kuwa vijana wanne kati ya tisa hufika Hospitali ya Benjamin Mkapa kila wiki figo zikishindwa kufanya kazi.

Vinywaji hivi vinaweza kuwa na athari kwa afya ya figo, hasa vinapotumiwa kupita kiasi.

Ndani yake kuna maji, sukari, kafeini, mitishamba, taurine (aina ya kemikali iitwayo amino sulfonic acid), protini, vitamini, madini na virutubisho vingine.

Tukianza na caffein, hicho ni kiambato cha kawaida katika vinywaji vya 'energy drinks' ambacho kinaweza kusababisha kuongezeka kwa shinikizo la damu na kiwango cha mapigo ya moyo.

Kiambato hicho kinapotumiwa kwa pamoja na viambato vingine kama vile taurine, athari zake kiafya huwa kubwa zaidi.

Kwa sababu hii, watu walio katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo wanapaswa kuwa waangalifu katika matumizi ya vinywaji hivyo.

Kwa upande mwingine, taurini, ambayo ni asidi ya amino inayotokana na vyanzo vya protini kama vile maziwa, nyama na samaki, inapatikana katika vinywaji vingi vya aina hiyo.

Wataalamu wamesema viwango vikubwa vya taurini katika damu kinaweza kuwa na madhara, hususan kwa watu walio na ugonjwa sugu wa figo (CKD au chronic kidney disease).

Kiambato kingine kinachotajwa ni sukari ambayo katika vinywaji hivyo iko kwa kiasi kikubwa.

Ulaji wa sukari kupita kiasi unaweza kuathiri afya kwa ujumla, pamoja na utendaji kazi wa figo.

Taarifa ya Taasisi ya Taifa ya Kisukari na Magonjwa ya Usagaji chakula na Figo (NIDDK) ambayo ni sehemu ya Taasisi za Taifa za Afya za Marekani, inasema kuwa matumizi ya mara kwa mara ya vinywaji hivyo yanaweza kuongeza hatari ya mawe kwenye figo.

Hii ni kutokana na kiasi kikubwa cha sodiamu inayopatikana katika vinywaji vingi vya kuongeza nguvu. Njia bora ya kuzuia kujengeka kwa mawe kwenye figo ni kunywa maji mengi kila siku.

Vinywaji hivyo vinaweza kuchangia upungufu wa maji mwilini kutokana na aina ya dawa inayojulikana kama 'diuretiki' ambayo hufanya figo kutoa mkojo mwingi.

Ikiwa figo zinatengeneza mkojo mwingi, basi mtu atakojoa mara nyingi na matokeo yake maji mwilini hupungua.

Upungufu wa maji mwilini huathiri mtiririko wa damu kwenda kwenye figo, jambo ambalo linaweza kusababisha figo kushindwa kufanya kazi.

Hata hivyo, matumizi ya wastani ya 'energy drink' hayawezi kuwa na madhara kwa figo, lakini matumizi ya kupita kiasi na mara kwa mara yanaweza kuwa na madhara kwa afya kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na utendaji kazi wa figo, na hata kushindwa kufanya kazi yake.

Ingawa vinywaji vya kuongeza nguvu vyenyewe havidhuru figo, kuvitumia kwa uangalifu ni muhimu ili kuzuia hatari za kiafya.

Unywaji wa maji na kuzingatia tahadhari katika matumizi kafeini na sukari ni muhimu kwa kudumisha afya ya figo.

April 13, 2021, gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, liliripoti kuwa kulikuwa na zaidi ya wagonjwa 600 waliokuwa wanapatiwa matibabu ya dialysis kutokana na ugonjwa wa figo katika vituo 17 vya kusafisha damu kote nchini.

Licha ya hatari hizi zinazojulikana, matumizi ya vinywaji vya hivyo yanaendelea kuongezeka, hususan miongoni mwa vijana, na pia unywaji mwingi wa mara kwa mara wa vinywaji hivi ni kubwa miongoni mwa watoto kuliko vijana.


Nyongeza na William Shao