Serikali yakabidhi pikipiki 221 Shinyanga

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yahaya Nawanda akikabidhi pikipiki 221 kwa wakuu wa Wilaya ya Kahama, Shinyanga na Kishapu
Muktasari:
- Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yahaya Nawanda amekabidhi pikipiki 221 kwa wakuu wa Wilaya ya Kahama, Shinyanga na Kishapu, akiwawataka maofisa ugani kuzitumia kwa kazi za kilimo pekee.
Shinyanga. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yahaya Nawanda amekabidhi pikipiki 221 kwa wakuu wa Wilaya ya Kahama, Shinyanga na Kishapu kwa ajili ya maofisa ugani kutoa huduma kwa wakulika ili wawe na kilimo chenye tija.
Amewaagiza maofisa ugani wote katika kata zao wasizigeuze pikipiki hizo kama bodaboda, bali wawafikie wakulima kwa wakati na kuwaelimisha kulima kilimo chenye tija.
Maagizo hayo ameyatoa leo Februari 10 wakati akikabidhi pikipiki hizo katika ofisi ya mkoa, ambapo amekabidhi pikipiki 39 kwa Wilaya ya Kishapu, pikipiki 82 kwa Wilaya ya Shinyanga na 100 kwa Wilaya ya Kahama.
"Ni marufuku kumpa pikipiki mtu yeyote yule ambaye hahusiki, hizi pikipiki zimenunuliwa kwa fedha ya umma hivyo mnatakiwa mzitunze na kuzihifadhi sehemu nzuri.
“Msizigeuze kama bodaboda ama msizitumie kwa mambo ya anasa tumieni kwa masilahi ya wananchi na Taifa," amesema Nawanda.
Amewataka maofisa hao kuhakikisha kuwa kilimo kinachangia asilimia 10 katika pato la Taifa ufikapo mwaka 2023.
“Ili maofisa ugani waweze kuwafikia wakulima, niwaagize wakurugenzi mhakikishe mnawawezesha mafuta maofisa ugani waweze kufanya kazi zao vizuri tunataka tukaione hiyo tija kwa vitendo,” amesema Nawanda.
Pia amewataka maofisa ugani wote kuwa na mashamba ya mfano ili wananchi wanapoona mashamba hayo waweze kuchukua mfano huo
"Hapa nilipo mimi nina heka tano Simiyu zinaendelea vizuri, hata maofisa ugani wangu niliwaagiza kulima kila mmoja heka moja na wamefanya," amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi wamesema maagizo waliyopewa watayabeba na kuyafanyia kazi.