Sh1.3 trilioni zitakavyotumika

Sh1.4 trilioni zitakavyotumika

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania Samia afafanua Sh1.3 trilioni, zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwaajili ya Uviko-19 zitakavyotumika.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassana amesema Sh1.3 trilioni za Shirika la Fedha Duniani (IMF) zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii, kwenye sekta za afya elimu, maji na utalii.

Rais Sami ameeleza hayo leo Jumapili Oktoba 10,2021 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19.

Amesema mpango huo utagharimu fedha nyingi, ambapo upatikanaji wa fedha hizo ulikuwa na mbinumbinu nyingi lakini baada ya kutuma timu zao na kujadiliana waliwaelewa.

“Wenzetu waliopata fedha kama hizi, walizielekeza kwenye ununuzi wa vifaa vya kujikinga na chanjo, kwa upande wetu tukasema hapana ili tuweze kukabiliana na corona, lazima tuwe na maji, tupunguze wanafunzi kubanana, lazima tuwe na vituo vya afya vingi vitakavyoweza kutoa huduma ipasavyo kuanzia ngazi ya wilaya na tarafa,”alisema Rais Samia.

“Kule chini tuwe na vituo vinavyoweza kutoa huduma kule chini, ili corona ikipiga kule chini tupate pa kutolea huduma hivyohivyo na kwenye ngazi za juu, tunashukuru walituelewa fedha hizi tuzitumie vile tulivyoona zinafaa,”amesema.

Aidha Rais Samia ametoa wito kwa sekta binafsi, kutumia fursa hiyo kuzalisha bidhaa zitakazotumika kwenye miradi hiyo ikiwemo mabati, saruji na vifaa vingine vitakavyotumika kwenye ujenzi.

“Tunaenda kujenga madarasa 15,000 na vituo vya afya zaidi ya 200 vinaenda kujengwa na kufanyiwa ukarabati hivyo tutakwenda kuhitaji vifaa vingi kwaajili ya ujenzi,”amesema.

“Sekta binafsi niwaombe sana kuchangamka na kutuunga mkono, tusiwe na sababu ya kuchelewa kutumia fedha hizi, fedha hizi ni za miezi tisa tu lakini pia fedha hizi zinatakiwa kubaki na kuzunguka hapa nchini zisitoke nje.