Tanzania kupata Sh1.3 trilioni za kupambana na Uviko-19

Tanzania kupata Sh1.3 trilioni za kupambana na Uviko-19

Muktasari:

  • Bodi ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imekubali kuipa Tanzania dola za Marekani milioni 567.25 (Sh1.3 trilioni) ambazo ni msaada wa dharura kwa ajili ya kushughulikia janga la Uviko-19.


Dar es Salaam. Bodi ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imekubali kuipa Tanzania dola za Marekani milioni 567.25 (Sh1.3 trilioni) ambazo ni msaada wa dharura kwa ajili ya kushughulikia janga la Uviko-19.

Mlipuko wa ugonjwa huo nchini umesababisha kuanguka kwa sekta ya utalii na kuongeza hitaji la ufadhili mkubwa ili kukabiliana na athari za kiafya na kiuchumi za janga hilo.

IMF iliidhinisha msaada huo wa dharura wa kifedha chini ya kituo cha mikopo ya haraka kwa lengo la kuunga mkono juhudi za mamlaka katika kukabiliana na janga hilo kwa kushughulikia gharama za haraka za kiafya, kibinadamu na za kiuchumi.

Mtazamo wa uchumi wa Tanzania umedorora kutokana na athari za janga la Uviko-19 pamoja na kuanguka kwa utalii baada ya vizuizi vya kusafiri, uchumi unaripotiwa kupungua kwa ukuaji wa asilimia 4.8 mwaka 2020, na ukuaji unatarajiwa kubaki chini kwa mwaka 2021.

Tanzania inahitaji fedha za haraka karibu asilimia 1.5 ya Pato la Taifa kama mamlaka kutekeleza mpango mpana wa kupunguza athari za janga hilo na kuhifadhi utulivu wa uchumi mkuu mbele ya wimbi la Uviko-19.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Serikali imeonyesha nia kwa kufuata sera za uchumi zinazofaa kushughulikia athari za janga hilo na kujitolea kuimarisha uratibu na uwazi ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinatumika katika kupambana na janga hilo.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji, Bo Li, ametoa taarifa ifuatayo:

"Janga la Covid-19 limeathiri mtazamo wa uchumi mkuu wa Tanzania katika afya na ustawi wa idadi ya watu.

“Ukuaji wa uchumi umepungua kuanzia mwaka 2020 na unatarajiwa kubaki chini kwa mwaka 2021, kuongezeka kwa umasikini na kuathiri ajira. Hatari ya Tanzania kuendelea kuwa na deni kubwa nje ya nchi imeongezeka hadi wastani, haswa kutokana na athari ya janga hilo kwa fedha zilizopatikana kupitia  utalii.

"Mamlaka inatekeleza mpango kamili wa kukabiliana na janga hilo kijamii na kiuchumi, Tanzania inahitaji msaada wa haraka wa kifedha kutekeleza mpango huu na kuiepusha mdororo wa kiuchumi,” amesema Bo Li.