Shahidi: Sabaya aligoma kuandika maelezo polisi

Muktasari:

  • Katika Kesi hiyo Sabaya na wenzake wawili wanashtakiwa kwa makosa matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha uliotokea Feb 9,  2021  katika duka la Mohamed Saad eneo la bondeni jijini Arusha.

Arusha. Shahidi wa saba ASP Gwakisa Venance Minga (45) ambaye ni mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Wilaya ya Arusha ameieleza mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Arusha  kuwa aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya alikataa kuandika maelezo ya kuthibitisha tuhuma za washtakiwa aliowapeleka kituo cha polisi.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali mwandamizi, Minga ameieleza  mahakama hiyo kuwa Februari 9, 2021 alipigiwa simu na aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha,   Kenani Kihongosi akimjulisha kuwa Sabaya ana watuhumiwa anawapeleka kituoni hapo na  kumpa angalizo kama wàna shauri la jinai aendelee na upelelezi na kama hawana shauri la jinai ampe mrejesho.

Aliieleza mahakama kuwa katika uchunguzi wa awali alibaini kuwa Sabaya  aliwakamata Numan Jasin na Hajirin Saad kinyume na utaratibu na kwamba  Sabaya na mtuhumiwa wa pili waliwapeleka kituoni hapo vijana hao huku wakiwa na mikwaruzo usoni iliyoashiria wamepigwa.

Amedai mahakamani hapo kuwa hawakumkamata Sabaya kwa sababu alikuwa mkuu wa Wilaya ya Hai na mteule wa rais,  na jeshi la polisi linajua taratibu za kushughilika na wateule wote wa rais ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi na kupeleka mamlaka zao za uteuzi.

Sehemu ya mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:

Wakili: Shahidi hebu ieleze mahakama 9/2/2021 majira ya saa nne usiku ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa nipo kituo cha polisi Arusha nikiendelea na majukumu yangu ya kawaida

Shahidi: Sabaya aligoma kuandika maelezo polisi

Wakili: Shahidi ieleze mahakama wakati ukiwa kituoni unaweza kukumbuka ni jambo gani lilitokea?

Shahidi: Nilipokea simu ya aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi.

Wakili: Alikupigia akikujuza juu ya mambo yapi?

Shahidi: Alinijuza aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Sabaya ana watuhumiwa hivyo akanipa angalizo kama wàna shauri la jinai niendelee na upelelezi na kama hawana shauri la jinai nimpe mrejesho.

Wakili: Shahidi hebu ieleze mahakama hiyo aliyekuwa Dc Arusha alikueleza watuhumiwa hao ni wa makosa yapi na wamekamatwa wapi?

Shahidi: Hakunieleza

Wakili: Shahidi ieleze mahakama baada ya kukupa taarifa hiyo nini kilitokea?

Shahidi: Moja baada ya taarifa hizo nilimjulisha mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha SSP Mchunguzi, nilimjulisha mkuu wa upelelezi Mkoa wa Arusha ACP Mwafulambo ambaye alinipa maelekezo nisubiri mpaka watuhumiwa watakapofikishwa nifanye mahojiano nao naye nimpe mrejesho.

Wakili:Baada ya kuwapa mrejesho viongozi wako wawili nini kilitokea?

Shahidi: Baada ya muda mfupi Sabaya akiwa na Sylvester (mshtakiwa wa pili) walifika kituo cha polisi wakiwa na vijana wawili.

Wakili: Shahidi hebu iambie mahakama hao vijana wawili walioletwa ulikuwa umewahi kuonana nao?

Shahidi:Hapana ile siku ndiyo niliwaona

Wakili: Shahidi na vipi kuhusiana na mshtakiwa wa kwanza uliwahi kuonana naye wapi?

Shahidi: Namjua tumewahi kuonana kwenye shughuli za kiserikali

Wakili: Shahidi umemtaja Sylvester naye uliwahi kuonana naye wapi?

Shahidi: Siku ya tukio ndio nilimuona kwa ukaribu kabla ya tukio hatujawahi kuwa karibu.

Wakili: Sasa hebu iambie mahakama ulitambua vipi jina lake ni Sylvester

Shahidi: Walivyofika kituoni nilifanya nao mahojiano ndipo akaniambia anaitwa Sylvester Nyegu.

Wakili:Shahidi ieleze mahakama wale vijana unaosema waliletwa walikuwa na asili gani?

Shahidi: Walikuwa na asili kama waarabu

Wakili: Shahidi  hebu eleza mahakama alipofika na vijana hao alikwambia nini

Shahidi: Mshtakiwa namba moja aliniambia amewakamata vijana wawili wakiwa na shauri la uhujumu uchumi, nilifanya mahojiano naye anipe uthibitisho  kama kuna kesi imefunguliwa dhidi yao Sabaya alishindwa kutoa uthibitisho huo.

Nilimtaka Sabaya aandike maelezo kuthibitisha tuhuma hizo ambapo aligoma kuandika lakini baada ya kumsikiliza maelezo yake nikaona utaratibu wa kitendo chake alichokifanya ni kinyume kabisa na sheria za nchi kwa sababu mwenendo wa makosa ya jinai haukufuatwa.

Wakili: Ulibaini hao watu aliokuja nao alikuwa amewakamata wapi?

Shahidi: Walikamatwa ndani ya duka maeneo ya Bondeni hicho kilikuwa kiashiria cha kwanza kwamba sheria imevunjwa.

Wakili: Sabaya alikueleza aliwakamata katika mazingira yapi?

Shahidi: Alinieleza kuwa aliwakamata ndani ya duka. Jambo la pili nikiangalia tukio zima siyo jeshi la polisi wala vyombo vya ulinzia na usalama  ulizingatia alikuwa DC Hai, ni operesheni ambayo jeshi la polisi Arusha halikuwa linaifahamu.Operesheni zote zinazohusisha taasisi nyingine kokote zitakakokuwa lazima OC CID ajue, zoezi lake halikuhusisha jeshi la polisi.  Na hata katika mahojiano tulibaini hakukuwa na chombo chochote cha usalama katika operesheni ile.

Wakili: Shahidi hebu tuambie wale vijana walioletwa walipokuwa mbele yenu walikiwa katika hali gani?

Shahidi: Wale vijana Hajirin Saad na Numan Jasin walivyoletwa,   Numan usoni alikuwa na alama usoni akionyesha amepigwa na Hajirin pia alikuwa na mikwaruzo inayoonyesha wamepigwa

Wakili: Unaposema mikwaruzo hasa unamaanisha nini

Shahidi: Walipigwa na kitu ambacho ni butu mfano mkono au fimbo hivyo iliacha alama katika miili yao siyo majeraha

Wakili:Shahidi hebu tuambie umeongea na Sabaya amekueleza baada ya hapo nini kilitokea?

Shahidi:Baada ya kukamilisha mahojiano naye na kuona hamna kesi taratibu zimevunjwa na kilichofanyika siyo sahihi, Sabaya na Sylvester  waliondoka na tukapata nafasi ya kufanya mahojiano na wahanga wawili ambao walitusimulia tukio zima na wao kuandikwa maelezo.

Wakili: Unatupa wakati mgumu sana umesema Sabaya alikiuka taratibu ukatizama huku unaona watu wameonekana wamepigwa halafu unaiambia mahakama mlimuacha akaondoka kwanini hamkumkata.

Shahidi: Hatukumkamata Sabaya kwa sababu alikuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, mteule wa rais na jeshi la polisi linajua taratibu za kushughilika na wateule wote wa Rais ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi na kupeleka mamlaka zao za uteuzi.

Wakili: Hebu ieleze mahakama mliwahoji wale vijana wawili mlibaini vijana hao walifanyiwa vitendo gani?

Shahidi: Kwenye mahojiano tulibaini vijana walivamiwa eneo la duka bila utaratibu na walidai kuna baadhi ya fedha zimechukuliwa, vijana wale walisema wamepigwa sana na watuhumiwa waliokuwa eneo la tukio na baada ya kuandika maelezo vijana walipewa PF 3 na tulibaini hakuna kosa la jinai.

Wakili: Utaratibu uliopo unatoa mamlaka gani ya kukamata mtu kwa kiongozi kutoka wilaya nyingine?

Shahidi:Mamlaka yake yalikuwa Hai angetakiwa taarifa zifike kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

Katika Kesi hiyo Sabaya na wenzake wawili wanashtakiwa kwa makosa matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha uliotokea Feb 9,  2021  katika duka la Mohamed Saad eneo la bondeni jijini Arusha.