Sikumbuki kushtakiwa kwa kujifanya Usalama wa Taifa -Sabaya

Sikumbuki kushtakiwa kwa kujifanya Usalama wa Taifa -Sabaya

Muktasari:

  •  Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, amedai hakumbuki kushtakiwa kwa kujifanya ofisa Usalama wa Taifa wala kuhojiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

  

Arusha. Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, amedai hakumbuki kushtakiwa kwa kujifanya ofisa Usalama wa Taifa wala kuhojiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana, Sabaya alitoa madai hayo alipokuwa akihojiwa na mawakili wa Serikali, Tumaini Kweka, Felix Kwetukia na Baraka Mgaya kwa nyakati tofauti, kuhusu utetezi aliotoa mahakamani hapo.

Akihojiwa na Mgaya, Sabaya aliieleza mahakama kumtambua mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Sylvester Nyegu na kudai kuwa hakuwa msaidizi wake, bali alipangiwa kazi na mkurugenzi wa halmashauri ya Hai.

Sehemu ya mahojiano ilikuwa hivi:

Wakili: Shahid nilikusikia wakati unatoa ushahidi wako kuwa mamlaka ya utezi iliunda tume sijui akaja Dk Bashiru na kesi iliyokuwa inakukabili mahakamani iliondolewa na DPP?

Shahidi: Ndiyo

Wakili: Ni sahihi ulifikishwa mahakamani kwa kosa la kujitambulisha wewe ni ofisa usalama wa Taifa ‘undercover’.

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Shahidi ni sahihi kesi hiyo ya jinai ndiyo ilipeleka ukatenguliwa nafasi yako ya uenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha?

Shahidi: Siyo kweli

Wakili: Shahidi wa sita wa jamhuri (Bakari Msangi) aliieleza mahakama alikuwa mjumbe, wewe ukiwa mwenyekiti na moja ya sababu za kuondolewa ilikuwa ni kesi hiyo na tume iliundwa makao makuu?

Shahidi: Sikumbuki Bakari alisema nini kuhusu kutenguliwa, lakini hakueleza hayo.

Wakili: Kuanzia Julai 2018 hadi Mei 2021 ukiwa katika Wilaya ya Hai, ulikuwa ukifahamika kama mkuu wa wilaya?

Shahidi: Kila mtu alikuwa na namna yake ya kunitambua

Wakili: Hapa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 16, 2021 ulisomewa mashtaka matatu yanayokukabili?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Uliulizwa majukumu yako ya DC ni yapi?

Shahidi: Nilieleza majukumu ya DC kusimamia shughuli zote za maendeleo, kusimamia usalama na atatekeleza majukumu mengine yoyote atakayopewa na mamlaka iliyomteua

Wakili: Kwa hiyo utakubaliana pamoja na Katiba, sheria iliyokuwa inaongoza majukumu yako ni sheria inayosimamia Tawala za Mikoa?

Shahidi: Ni moja ya sheria hizo.

Wakili: Kwa mujibu wa sheria hiyo, ulikuwa unawajibika chini ya mkuu wa mkoa Kilimanjaro.

Shahidi: Sijaisoma hiyo sheria

Wakili: Kwa hiyo ulikuwa hujui unatekeleza majukumu yako chini ya gani?

Shahidi: Sijui.

Wakili: Uliapishwa tarehe ngapi kuwa mkuu wa wilaya?

Shahidi: Tarehe 1/ 8/2018

Wakili: Uliapishwa wapi na nani alikusimamia kula kiapo?

Shahidi: Nilikula kiapo mbele ya mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Wakili: Nani aliyekupa kiapo?

Shahidi: Simfahamu.

Wakili: Baada ya kuapa ulimfahamu alikuwa ni nani?

Shahidi: Dk Anna Elisha Mghwira

Wakili: Unaieleza mahakama ulikuwa humjui mkuu wa mkoa aliyekuwa anakuapisha ni nani.

Shahidi: Kwa wakati nimeshika biblia naapa, sikuwa namfahamu ila nilimfahamu baada ya kuapa.

Wakili: Mamlaka yako ya uteuzi kuwa DC ni nani wakati huo?

Shahidi: Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Wakili: Kama mamlaka iliyokuteua ni Rais kwa nini ulienda kuapa kwa mkuu wa mkoa?

Shahidi: Aliniapisha kwa niaba ya Rais.

Wakili: Kwa hiyo moja ya misingi hiyo uliapa mbele ya mkuu wa mkoa, hiyo inaonyesha majukumu yako ulitakiwa utekeleze kupitia yeye.

Shahidi: Yeye pamoja na wengine.


Kuanza utumishi wa umma

Wakili: Lengai ulianza lini kuwa mtumishi wa umma?

Shahidi: Siwezi kulieleza hilo mheshimiwa hakimu.

Wakili: Tarehe 9/2/2021 baada ya kumaliza kikao ulieleza kuwa ulipata simu kutoka mamlaka iliyokuteua

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Na ukapokea wageni uongezane nao Arusha.

Shahidi: Nilieleza.

Wakili: Na ukawaongoza kuja Arusha kama nani?

Shahidi: Siwezi kueleza, anayeweza kujibu ni aliyenipa kazi hiyo.

Wakili: Lengai umesema miongoni mwa majukumu yako ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama.

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Utakubaliana na mimi majukumu hayo yapo kisheria na cheo hicho kimeundwa kisheria.

Shahidi: Nakubaliana na wewe

Wakili: Katika muktadha huo utakubaliana na mimi muundo na kazi ya kamati ya ulinzi na usalama, si siri?

Shahidi: Siyo.

Wakili: Na kazi za hizo kamati zimeainishwa kisheria hivyo siyo siri.

Shahidi: Ni siri.

Wakati fulani, wakili alimuuliza kuhusu baba yake na kuhojiwa kwake na Tume ya Haki za Binadamu:

Wakili: Baba yako yupo?

Shahidi: Siwezi kueleza masuala ya kifamilia. Sitajibu hilo swali

Wakili: Una uhusiano gani na Mzee Thomas Ole Sabaya

Shahidi: Siwezi kueleza uhusiano wetu

Wakili: Nikikwambia ni baba yako utakataa?

Shahidi: Siwezi kueleza hilo

Wakili: Lengai kati ya masuala uliyoulizwa na Tume ya Haki za Binadamu, ni kwanini una vijana zaidi ya wanne unaokuwa nao ofisini na nje ya ofisi na si waajiriwa wa utumishi wa umma?

Shahidi: Sikumbuki kuwahi kuulizwa swali hilo

Wakili: Jana wakati unajitetea wakili alikuuliza ukataja operesheni nyingi na ukaeleleza watu wengi wanatoka nje ya maeneo ya kazi, wakati unatekeleza kutoka Hai ulikuwa na cheo gani?

Shahidi: Nilikuwa Mkuu wa Wilaya

Wakili: Mkuu wa Wilaya ni kazi ya kiutendaji au kisiasa?

Shahidi: Civil servant (mtumishi wa umma)