Tanzania, Msumbiji zatiliana saini ulinzi na usalama

What you need to know:

  • Serikali za Tanzania na Msumbiji zimetiliana saini eneo la usalama na ulinzi pamoja na eneo la utafutaji na uokoaji kwa nia ya kuendelea kulinda mipaka baina ya nchi hizo mbili.

Dar es Salaam. Serikali za Tanzania na Msumbiji zimetiliana saini eneo la usalama na ulinzi pamoja na eneo la utafutaji na uokoaji kwa nia ya kuendelea kulinda mipaka baina ya nchi hizo mbili.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano, Septemba 21, 2022 katika Ikulu ya Msumbiji jijini Maputo wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya Kiserikali ya siku tatu nchini humo.

“Ushirikiano wa kudumisha amani na utulivu kwa sababu Tanzania na Msumbiji katika eneo hili wanashirikiana na ni muhimu kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi na usalama, tulianza tangu miaka ya 1980 na kuhakikisha tunapambana dhidi ya magaidi na aina yoyote ya uharamia.

“Kama alivyosema Rais Filipe Nyusi kupitia mahusiano haya tumeweza kutiliana saini eneo la usalama na ulinzi na utafutaji na uokoaji ni hatua ya muhimu katika kusonga mbele,” amesema Rais Samia.

 “Kumekuwepo na uhalifu mwingi wa mpakani na suala la ugaidi ambao unaendelea. Mpaka huu ni mrefu zaidi kuna haja ya kushirikiana.”

Rais Filipe Nyusi amesema ili kupambana na ugaidi lazima uwepo ushirikiano na ili kufanikisha ni lazima zifuatwe taratibu za kisheria kwa kuwepo kwa mikataba.

“Inagusa mengi suala la dawa za kulevya, usafirishaji wa binadamu na mambo yanayoendana na haya, eneo la biashara kumekuwa na mdororo nchi ya Msumbiji imekuwa ikipitia katika wakati mgumu ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema Nyusi.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.