Tathmini yafichua hasara ya Sh1.6 bilioni upanuzi hospitali ya Tumbi

Muktasari:

Uchunguzi wa tathmini ya thamani ya fedha katika mradi wa upanuzi na uboreshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani-Tumbi umeonesha hasara ya Sh1.6 bilioni.

Dodoma. Uchunguzi wa tathmini ya thamani ya fedha katika mradi wa upanuzi na uboreshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani-Tumbi umeonesha hasara ya Sh1.6 bilioni.

Hasara hiyo imebainika kwa kuhakikiwa kwa baadhi ya vipimo vya kazi na kuchukua sampuli chache kwa ajili ya vipimo vya maabara.

Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima aliyasema hayo jana wakati akipokea tathmini ya awali ya mradi huo baada ya maagizo yake aliyoyatoa Desemba 24,  2020 alipotembelea hospitali hiyo na kutoridhishwa na ujenzi.

Katika ziara hiyo,  Dk Gwajima alitoa maelekezo kwa katibu tawala Mkoa kufanya tathmini ya uwepo wa thamani ya fedha  katika utekelezaji wa mradi wa upanuzi na uboreshaji wa hospitali hiyo.

"Ripoti nimeipokea na iko dhahiri kabisa mahitaji ya upanuzi na uboreshaji wa hospitali ya Tumbi yalikadiriwa kutekelezwa kwa Sh29 bilioni baada ya Serikali kuonyesha nia ya kusaidia ufadhili wa mradi huo kufuatia mpango wa awali wa uongozi wa Mkoa mwaka 2007-2009 iliokuwa na makadirio ya Sh5 bilioni,” amesema Dk Gwajima.

Amesema hadi sasa Sh9.4 bilioni zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kati ya Sh29 bilioni zilizokadiriwa ambapo Sh5.5 bilioni imetumika katika utekelezaji chini ya usimamizi wa shirika la elimu Kibaha na katibu tawala Mkoa na Sh3.9 bilioni zimehamishiwa Wizara ya Afya.

Waziri huyo amesema taarifa hiyo imebaini kuwepo kwa mikataba ya makandarasi wawili Suma JKT na MUST Construction Bureau kinyume na Sheria namba saba ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 pamoja na marekebisho yake mwaka 2016.

"Kutokana na mkanganyiko huo namuelekeza katibu tawala Mkoa kupitia kamati yako ya tathmini mfanye tathimini ya kina ndani ya siku 30  na kuniainishia  hasara halisi kwa kurejea vipimo vya jengo zima, kutathimini na kushauri kama jengo hili linafaa kwa matumizi ya umma pamoja na hali ya majengo ya zamani kama yanafaa kukarabatiwa na kutumika tena kwa gharama stahiki,” amesisitiza.