Upande wa utetezi kesi ya Sabaya waeleza haya mahakamani

Muktasari:

  • Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne imeahirishwa hadi Julai 4, 2022 kutokana na upelelezi kutokamilika.

Moshi. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne imeahirishwa hadi Julai 4, 2022 kutokana na upelelezi kutokamilika.

Sabaya na wenzake wanne walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi  leo  Juni 20,2022  kwa ajili ya kesi yao kutajwa.

Akiomba kuahirishwa kwa kesi hiyo wakili upande wa mashtaka, Verediana Mlenza ameieleza mahakama hiyo  kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba kibali kutoka ofisi ya DPP na hati ya kuipa mahakama hiyo mamlaka ya kuendelea na kesi hiyo bado hakijatolewa.

Kabla ya kuombwa kwa ahirisho hilo wakili wa upande wa utetezi, Hellen Mahuna aliutaka upande wa mashtaka kuwa makini kwa sababu mara ya kwanza washtakiwa hao walipofikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yao walieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi umeshakamilika.

"Hatuna pingazmizi na ahirisho, upande wa mashitaka mara ya kwanza kesi ilipoletwa katika mahakama hii walieleza kuwa upelelezi umeshakamlika ,mara ya pili wakaja hapa na kutuambia upelelezi bado haujakamilika sasa ni mwezi, tunaomba upande wa jamhuri wawe "serious",kwa sababu washtakiwa wanateseka," amesema.

Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Salome Mshasha ameiahirisha kesi hiyo kwa muda wa siku 14 na kuutaka upande wa jamhuri kuja na hitimisho wakati kesi itakapokuja tena Julai 4, 2022.