Utabiri wa hali ya hewa yazikutanisha nchi 11 Tanzania
Muktasari:
Nchi 11 katika Pembe ya Afrika zinakutana hapa nchini kwa ajili ya kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa mvua za vuli kati ya Oktoba –Disemba.
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Isaack Kamwelwe amewashauri wataalamu wa hali ya hewa kutopuuza ujuzi wa asili katika kutabiri hali ya hewa kwa sababu elimu hiyo imetumika na watu wa zamani na imeonekana kufanya kazi.
Kamwelwe ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 26,2019 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa mvua za vuli kwa kanda ya Pembe ya Afrika. Kongamano hilo limehusisha nchi 11 ambazo ni Burundi, Uganda, Somalia na Rwanda.
Nchi nyingine ni Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini, Eritrea, Djibout, Sudan na wenyeji Tanzania. Kaulimbiu ya mkutano huo ni utoaji wa tahadhari kwa hatua za haraka katika kukabiliana na athari za hali ya hewa.
Kamwelwe amesema wazee wa zamani wakiona aina fulani za wadudu wanajua tayari mvua zimekaribia, hivyo wanaanza kuandaa mashamba yao mapema.
Pia, amesema kuna aina za wadudu ambao wakionekana wanaashiria kwamba mazao yataharibiwa mapema kabla ya mavuno.
“Sisi ni Waafrika, indigenous knowledge (ujuzi wa asili) tusiisahau. Tuanzie pale walipoishia wazee wetu, tuiendeleze ili iweze kutusaidia katika utabiri mzuri wa hali ya hewa. Tusidharau vitu vya kwetu,” amesema Kamwelwe.
Waziri huyo amezishauri mamlaka za hali ya hewa kuwa na vitengo vidogo vitakavyoangalia mambo hayo ya asili kwa lengo la kuboresha utabiri wa hali ya hewa na kuwaepusha wananchi na majanga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agness Kijazi amesema kuna changamoto ya vifaa vya utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za Afrika, hata hivyo, amesema Tanzania inafanya vizuri katika kuhakikisha inakuwa na vifaa vya kutosha.
Amesema Tanzania ina rada mbili za hali ya hewa na nyingine tatu ziko kwenye mpango wa manunuzi huku lengo likiwa ni kuwa na rada saba nchi nzima.
Amesema kongamano hilo litakuwa ni fursa ya kubadilishana uzoefu katika eneo hilo.