Utata mhasibu kuunguzwa, kifo

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Neema Towo, ulipowasili kwa ajili ya ibada ya kutoa heshima za.mwisho iliyofanyika Kanisa la KKKT Tumbi Kibaha, mkoani Pwani jana. Picha na Sanjito Msafiri

Kibaha. Siku chache zikiwa zimepita baada ya kutokea kifo cha aliyekuwa mhasibu wa benki ya Boa, Neema Towo anayedaiwa kutekwa na kuuawa kwa kuchomwa moto, baba mzazi wa marehemu, Ndeonasia Towo ameeleza mkasa ulivyokuwa.

Mwili wa mtaalamu huyo wa uhasibu aliyeachishwa kazi mwezi uliopita, uliagwa jana na kusafirishwa kupelekwa nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro kwa maziko.

Akizungumza baada ya ibada ya maziko iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Tumbi Kibaha Mkoa wa Pwani jana, Towo amewaomba watu wapate taarifa sahihi kuhusu kifo cha mwanawe badala ya kuzungumza mambo wasiyoyajua na kuyaweka kwenye mitandao.

Alisema siku ya tukio, mwanawe alikuwa kanisani kwenye ibada ya jioni, akapigiwa simu na watu asiowajua akiwa ndani ya kanisa akatoka nje kusikiliza baada ya hapo hakuonekana tena.

“Baada ya kutoonekana nyumbani hadi usiku, wakaanza kumtafuta, baadaye baba yake alipigiwa simu kuwa mwanawe amekimbilia kwenye nyumba moja lakini anaonekana kama kauunguzwa moto, na amewatajia namba zangu ili wanipigie simu kunitaarifu,” alisema mzee Towo.

Alisema ilibidi aondoke kuelekea kwenye hiyo nyumba wakampeleka hospitali na baada ya vipimo aliambiwa na madaktari kuwa inaonekana figo za mwanawe zimeathiriwa.

“Sasa sijui kitu gani kilifanyika, sijui alichomwa sindano ya sumu na hao watesi wake, lakini ukiangalia mwili wake ni kama kilichomuunguza siyo moto wa kawaida,” alidai.

Alisema baada ya kuelezwa hivyo, mdogo wake na Neema alimueleza kusudio lake la kumtolea figo moja dada yake, “Lakini kabla hatujamaliza mjadiliano, Neema akawa amefariki dunia.”

Alisema Neema alikuwa mtu shupavu ndiyo maana baada ya kufanyiwa tukio hilo, aliweza kukimbia umbali mrefu hadi kuifikia hiyo nyumba walikomkuta akipiga kelele na kuomba msaada.

“Alipofika tu walimuuliza ni nani wanaweza kumpatia taarifa haraka akataja namba zangu ili nipigiwe kujulishwa mkasa uliomkuta, na nikapigiwa muda huo huo,” alisema.

Awali akizungumza kwenye ibada hiyo, Mkuu wa Kanisa la KKKT Jimbo la Magharibi, Anta Muro aliwataka waumini kutumika vema katika shughuli za Kanisa na za kijamii.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mharakani Kibaha ambako familia hiyo inaishi, Eliamini Mgonja alisema watu waliohusika na tukio hilo wote watapatikana kwa sababu damu ya mtu siyo kitu cha mchezo.